How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Wednesday, 22 August 2012
Waliouza bendera yetu Iran watajwe
INGAWA Watanzania hawakushupalia kashfa ya Tanzania kuiruhusu Iran kupeperusha bendera yao kwenye meli zake za mafuta baada ya kuwekewa vikwazo kimataifa, kashfa hii inafichua uoza wa serikali.
Je, hili nalo limefanyika kwa ridhaa na heshima yao au dharau na hujuma kwao? Ni jambo la hatari na kujidhalilisha kuruhusu bendera ya nchi kutumiwa na nchi nyingine kufanya biashara hatari.
Hii ni biashara hatari ikizingatiwa kuwa, jumuia ya kimataifa ilipitisha azimio la kuiwekea vikwazo Iran, nayo ikakubali hatua hii, vinginevyo ingeshupaa na kutaka itendewe haki kama kweli haki yake imekiukwa kuliko kujificha chini ya bendera za nchi nyingine.
Bendera ya taifa, ni alama na kitambulisho cha taifa chenye thamani kuliko kitu chochote, ikiwemo hata taasisi ya urais.
Hivyo, anayechezea alama hii awe mtu binafsi, shirika na hata mamlaka, anapaswa kuchukuliwa kama msaliti na mhaini ambaye adhabu yake, ni kifo chini ya sheria ya Tanzania.
Kiongozi yeyote asiyejua umuhimu wa bendera yetu kiasi cha kuiruhusu ichezewe na kuuzwa kama karanga kukidhi tamaa za kipumbavu na kifisi za baadhi ya maofisa wa serikali, hafai kuendelea kuwa hata kuitwa kiongozi wa taifa.
Kuendelea kuwa na watawala wa namna hii, hakuna tofauti na kulibaka taifa.
Asiyechukizwa na kitendo cha bendera yetu kutumiwa na taifa jingine kuficha uchafu wake, hapaswi kuitwa hata Mtanzania achia mbali kuwa kiongozi.
Kwa kuzingatia umuhimu wa bendera ya taifa, si vibaya kuwataka wananchi waamke na kuwawajibisha viongozi wasiolinda maslahi ya taifa kiasi cha kuruhusu bendera yetu kutumiwa na taifa jingine kuepuka kuumia kiuchumi wakati sisi tunaweza kuumizwa na upogo huu.
Kwa kuzingatia umuhimu wa bendera kama alama ya taifa, ni ajabu kuwa Watanzania, hata waliposikia habari hii ya kuudhi, hawakuhamanika kuiwajibisha serikali inayojiita yao.
Je, haya ni matokeo ya ujinga, ukosefu wa uzalendo, woga au ufisadi wa kimawazo kiasi cha kushabikia kila upuuzi unaoingiza pesa hata kama hiyo pesa hawaipati?
Rejea imani kuwa ujanja ni kupata na hapendwi mtu. Je, Watanzania tumekubali kuwa wa hovyo kiasi hiki hata kwenye maslahi ya taifa na vizazi vijavyo?
Hili lingetokea kwenye nchi zenye watu wenye mwamko na kujua heshima na stahiki ya nchi yao, lilitosha kuiondosha serikali iliyoko madarakani.
Maana hata ukiangalia utetezi uliotolewa na serikali, ni wa kichovu na uongo mtupu.
Kinachokera na kuamsha hasira, ni utetezi uliotolewa na serikali baada ya kubanwa kuhusiana na kashfa hii.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Bernard Membe alikaririwa akisema kuwa kama serikali itagundua kuwa meli 36 za Iran zilisajiliwa, basi itafuta usajili huo!
Hii ni ajabu. Kumbe wanajua hata idadi ya meli zilizobebeshwa bendera ya taifa letu halafu wanajifanya hawajui!
Eti wanasema, kadhia hii imesababishwa na wakala aliyeko Dubai! Ala!
Huyu wakala hata hawasemi atachukuliwa hatua gani wala hawana mpango wa kuchunguza kadhia hii.
Ni ajabu kukuta serikali na mamlaka yake zinajua kuwa wakala huyu aliyetambuliwa kutoka visiwani, bado hajakamatwa na kufunguliwa kesi ya uhujumu na uhaini haraka sana iwezekanavyo ili kurejesha heshima ya serikali na taifa.
Wameshindwa hata kuomba msamaha wala kulaani uchafu na ufisi huu. Je, namna hii hayajajengeka mazingira ya kuipiga mnada Tanzania hata kwa makundi ya jinai kama inavyoanza kubainika baada ya vigogo wa vita wa Somalia kuanza kuwekeza nchini?
Kesho utasikia kuwa makundi ya kigaidi ya Al Shabaab, Al Qaeda hata Boko Haram yanatumia bendera ya Tanzania kwenye makambi yao ya kuandalia magaidi wa baadaye.
Huu ni ushahidi kuwa, kwa uongozi huu nchi yetu si salama hata kidogo.
Maana tangu serikali ya sasa iingie madarakani, imekuwa na sifa ya kufanya madudu na kukumbwa na kashfa.
Kashfa ya kwanza ilikuwa Richmond ikifuatiwa na Dowans na sasa Iran.
Tunapelekwa wapi Watanzania? Je, tunaogopa nini kuwawajibisha watawala wetu ambao wamethibitisha kuwa madarakani kwa bahati mbaya na kwa ajili ya maslahi binafsi?
Sitashangaa kesho nikisikia kuwa, baadhi ya mawakala wa kununua mafuta toka Iran ni makampuni yenye ushawishi kwa wakwasi watu walioko madarakani kuchuma badala ya kupanda. Sitashangaa kusikia makampuni ya mafuta yaliyoibuka hivi karibuni yakifanya biashara na Iran.
Kimsingi, kama hatua hazitachukuliwa kwa wahalifu walioweka maslahi na mustakabali wa taifa, hatari itathibitisha dhana kuwa tunaongozwa na watu wasio na uzalendo wala visheni ukiachia mbali kutochelea kinachowakuta baada ya kuachia madaraka.
Hii itajenga picha kuwa, watawala wetu ni wagumu wa kufikiri na kuelewa, hasa kutokana na kutanguliza matumbo yakiwaelekeza kwenye maslahi binafsi badala ya mustakabali wa taifa.
Kwa hili la kuuza bendera yetu kwa taifa lililowekewa vikwazo, ni ushahidi kuwa sasa Tanzania inaweza kuuzwa na kila jambazi kiholela na kwa yeyote bila kuchukuliwa hatua.
Tulianza na ujambazi wa rada, tukaja kwenye wa EPA na hatimaye wa IPTL, Richmond, Dowans na sasa tunauza bendera ya nchi yetu kana kwamba hatuihitaji!
Yuko wapi rais kutoa maelezo ya kina na kutoa msimamo wake na serikali yake juu ya kuwashughulikia hawa wahalifu? Kiko wapi chama tawala kutoa maelezo tena yanayoingia kichwani au kuwa tayari kuwajibika?
Jamani, wako wapi Watanzania kutaka maelezo na uwajibikaji? Je, tumekuwa wa hovyo kiasi cha kuuzwa na kila jambazi kwa amtakaye na bei atakayo?
Tubadilikeni haraka kabla hatujabadilishwa na mahitajio ya wakati huu, tena kwa nguvu na aibu.
Waliouza bendera yetu kwa Iran lazima watajwe na kushughulikiwa haraka, vinginevyo serikali iwajibike.
Vinginevyo, itajenga dhana kuwa hao ni mawakala au washirika wake katika hujuma hii kama haitawashughulikia.
Je, Tanzania imekuwa rahisi hivi kiasi cha kuchezewa na kila kibaka?
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 22, 2012.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment