The Chant of Savant

Sunday 12 August 2012

Kashfa ya meli za Iran: Ni rahisi kuinunua na kuiuza Tanzania kinyemela


An Iranian oil tanker - archive shot, 2004

Ingawa watanzania hawakushupalia kashfa ya Tanzania kuiruhusu Iran kupeperusha bendera yake kwenye meli zake za mafuta baada ya kuwekewa vikwazo kimataifa, kashfa hii inafichua uoza wa serikali yetu. Ni jambo la hatari na kujidhalilisha kuruhusu bendera ya nchi kutumiwa na nchi nyingine kufanya biashara hatari. Bendera ya taifa ni alama na kitambulisho cha taifa chenye thamani kuliko hata urais. Ni ajabu kuwa watanzania, hata waliposikia habari hii ya kuudhi, hawakuhamanika kuiwajibisha serikali inayojiita yao. Hili lingetokea kwenye nchi zenye watu wenye mwamko na kujua heshima na stahiki ya nchi yao, lilitosha kuiondosha serikali iliyoko madarakani. Maana hata ukiangalia utetezi uliotolewa na serikali ni kwa kichovu na uongo mtupu. Eti wanasema kadhia hii imesababishwa na wakala aliyeko Dubai! Ala! Huyu ajenti hata hawasemi atachukuliwa hatua gani wala hawana mpango wa kuchunguza kadhia hii. Wameshindwa hata kuomba msamaha wala kulaani uchafu na ufisi huu. Je namna hii hayajajengeka mazingira ya kuipiga mnada Tanzania hata kwa makundi ya jinai kama inavyoanza kubainika baada ya vigogo wa vita wa Somalia kuanza kuwekeza nchini?  Kesho utasikia kuwa makundi ya kigaidi ya Al Shabaab, Al Qaeda hata Boko Haram yanatumia bendera ya Tanzania kwenye makambi yao ya kuandalia magaidi wa baadaye. Huu ni ushahidi kuwa kwa uongozi huu nchi yetu si salama hata kidogo. Maana tangu serikali ya sasa iingie madarkani imekuwa na sifa ya kufanya madudu na kukumbwa na kashfa. Kashfa ya kwanza ilikuwa Richmond ikifuatiwa na Dowans na sasa Iran. Tunapelekwa wapi watanzania? Je tunaogopa nini kuwawajibisha watawala wetu ambao wamethibitisha kuwa madarakani kwa bahati mbaya na kwa ajili ya maslahi binafsi. Sitashangaa kesho nikisikia kuwa ajenti wa kununua mafuta toka Iran ni kampuni ya mwanamke Rahma Kharoos Kasiga anayehusishwa na Jakaya Kikwete naye asikanushe. Sitashangaa kusikia kuwa kampuni ya mwanamke huyu ya RBP Oil ikifanya biashara na Iran. Kimsingi, serikali yetu inaongozwa na watu wasio na uzalendo wala visheni ukiachia mbali kutochelea kinachowakuta baada ya kuachia madaraka. Viongozi wetu ni fedhuli na wagumu wa kufikiri na kuelewa hasa kutokana na kutanguliza matumbo yakiwaelekeza kwenye maslahi binafsi badala ya mstakabali wa taifa. Kwa habari zaidi BONYEZA hapa.

No comments: