How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Thursday, 16 August 2012
Kwa hili la majaji tunamuunga mkono Lissu
Baada ya kuingia serikali zinazoongozwa na watu wasio makini, baadhi ya nyadhifa zilizokuwa zikiheshimika zimeshuka hadhi, kukosa hata kuchafuliwa. Mojawapo ya nyadhifa zilizochakachuliwa na kukosa hadhi ni ujaji. Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliliona hili kiasi cha kulitolea ufafanuzi baada ya kuonekana kama anashambulia mahakama. Heri Lissu ameliona hili na kujitoa mhanga kulizungumzia. Watanzania si kwamba hawakuliona wala kulijua hili. Waliliona na kulijua sema waliogopa makahama. Kwenye mabaa hata kwenye madaladala watu wanaongelea uoza huu. Siku hizi kumuona jaji na kumalizana naye si jambo la ajabu. Zamani cheo cha jaji kilitisha na kuheshimika hakuna mfano. Ila siku hizi, ujaji hauna tofauti na ukuwadi wa kawaida baada ya kuona watu wachafu wakipewa hadhi hii. Si uongo wala uchochezi. Majaji wengi walioteuliwa kwa wingi na utawala wa sasa kwa kuzingatia kujuana au kulipana fadhila wamechafua sifa ya ujaji. Wapo majaji wenye kila aina ya madoa kiasi cha kushangaza umakini gani ulitumika kuwateua. Wapo walioshiriki kikamilifu kwenye wizi wa fedha za umma kama vile EPA. Wapo wenye tuhuma za wazi wazi za kutoa rushwa au kuingilia mahakama katika kutoa haki. Wapo ambao ni vihiyo wasio na ujuzi wa kutosha kuwa majaji. Wapo ambao ni wazee waliovuka umri wa utumishi lakini wakapewa ajira kishikaji. Wapo walioteuliwa si kwa sifa bali dini, jinsi zao hata mitandao yao. Hawa pamoja na baadhi ya mabalozi, wakuu wa wilaya na mikoa hata mawaziri, wamechafua hadhi ya utumishi wa umma. Hili licha ya kuwa pigo kwa haki na utumishi wa umma, ni kashfa kwa serikali na ofisi za umma. Kama kuna jambo ambalo wananchi wanaweza kufanya, ni kushinikiza mfumo huu mchafu wa kishikaji na kifisadi unateketezwa huku walionufaika nao wakiwajibishwa. Lissu amewataja wengi. Tunangoja kusikia wakienda mahakamani kumshitaki. Kwa wale wenye udhu wa kutosha tutasikia wakijiwabika. Maana kwa madai na utetezi uliotolewa na Lissu wamechafuka kiasi ambacho hawawezi kusafishika. Sasa nini kifanyike? Tuondokane na tabia ya kumpa rais madaraka ya kufanya uteuzi wa majaji maana imeyatumia vibaya kuwafadhili na kuwalinda marafiki na washirika zake. Badala yake iundwe tume ya kuajiri majaji kama inayofanya kazi nchini Kenya kwa sasa ambapo nafasi za majaji kuanzia jaji mkuu hutangazwa na wanaozihitaji huwasilisha maombi na kuhojiwa na kupitishwa au kukataliwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment