The Chant of Savant

Wednesday 11 September 2013

Eti watanibana hadi niwataje wauza bwimbwi

NIKIWA nadhani yamekwisha kumbe ndiyo yanaanza! Baada ya kuwayeyusha wanywa kahawa kwa sanaa za kutaja wauza bwimbwi na kutoka zangu mkuku baada ya kunizomea nilidhani mambo yamekwisha. Sikujua kumbe ngoma ndiyo inaanza yarabi!
Naona Mijjinga anaingia akiwa na gazeti lake la Danganyika Daima. Anavyoonekana kwa hesabu za haraka haraka ni kama ana maya nami.
Hajiungi. Anaanza: “Mheshimiwa Mpayukaji juzi hukututendea haki. Yaani uaahidi ungemwaga tama halafu unaishia kujikanyaga na kuufyata kama Daktari Mwakiwembe na Bill Lukuvi! Mbona huko nyuma hukuwa hivi nini kimekusibu ndugu yangu?”
Mgosi Machungi hangoji nijitetee. Anakwanyua mic: “Muishiwa, soe, mhishimiwa Mpayukaji tilikuwa tinakuheshimu lakini sasa naona kama tilifanya makosa.”
Ili kumtia mkwara naamua kuchimba mkwara: “Mgosi tuheshimiane. Usitake nawe nikuchukie kama Mijjinga aliyenilinganisha na hao wababaishaji wakubwa. Yaani mgosi umefikia mahali unanilinganisha na hao waishiwa wazi wazi! Shame on you!”
Kutokana na mkwara niliomchimbia Kanji kuwa ningemtaja yeye, anaamua kunitetea kinamna, anakwanyua mic: “Gosi Chungi hapana sumbua Payukaji.” Ananigeukia na kunitazama na kusema: “Hishimiwa Payukaji sasa taja Chungi kama yeye ona taja uza bimbi rahisi.”
“Subutu! Hata akinitaja haitamsaidia. Kwani mimi nina nini kama ushahidi? Sina ghoofa wala shangingi zaidi ya bi mkubwa wangu. Kanji tiheshimiane.” Mgosi anachimba mkwara naye.
Kanji kuona hivyo anaamua kuchomoa kinamna. Anasema: “Chungi veve elewa baya mimi. Mimi tania tu.”
Mgosi haridhiki. Akiwa amechukia baada ya kutupa kipisi cha sigara kali yake anasema, “Kama utani isinitanie. Nenda utanie akina Mwakiembe, Lukuvie na mkuu wanaoogopa kutaja wauza unga na mali zao za wizi.”
Msomi hajivungi. Anampa Mipawa gazeti kwa vile alikuwa amelikodolea mimacho na kuendelea: “Jamani let’s be a little bit serious. Hivi mlitegemea hawa wasanii wangewataja wauza bwimbwi halafu wao wawe salama?
Hili la mkuu kutaja mali zake au kuwashughulikia watu wake wanaouza unga mie nshalikatia tamaa. Nani amtaje nani wakati wote ni kambale? You know what I mean. Au siyo?”
Kapende ambaye alikuwa akibofya bofya kisimu chake anaamua kutia guu: “Wazee, japo huwa simpendi mzee Kimdunge Ngumbaru Mwehu, pamoja na kupinga kauli yake kuhusu Muunganiko, namuunga mkono alipomtolea uvivu Lukuvie kuwa ataje majina ya wauza bwimbwi hata kama na bosi wake yumo.”
Msomi anaamua kurejea: “It needs the courage of the mad to say what mzee Kimdunge said.
Muhimu ni kwamba, kama alivyosema Philip Zembardo: Kuna kipindi watu wanaodhaniwa kuwa wa maana hufanya vitu vya hovyo. Niliisoma hii wakati nikifanya PhD yangu isiyo ya kughushi.”
Kabla ya kuendelea mzee Maneno anaingilia: “Msomi naona leo una hasira sana hadi unaongea ukameruni mtupu ukijua fika wengine shule haipandi.”
Msomi anagundua kosa lake na kuomba msamaha na kuendelea: “Kwa ufupi ni kwamba inahitaji roho ya mwendawazimu kusema aliyosema Kimdunge. Maskini, sijui ni kutokana na uzee au usanii. Amesahau kuwa chama chake kilikatwa masikio na mafisadi miaka mingi iliyopita. Anataka watajane bila kujua kuwa sera yao ni kulindana?”
“Hichi kibabu kinafiki. Kimesahaugi kuwa hao hao wanaowalindaga wauza unga ndiyo hao hao waliolindaga ufisadi wa mke wake pale alipohujumu kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo?” Anachomekea Mipawa.
Sofia Lion, huyu ni mwanakijiwe ambaye huja na kupotea, anaamua kumwaga itikadi: “Kusema kuwa Kimdunge ni mnafiki ni kumkosea adabu. Hizi tuhuma za mkewe mpelekee mkewe na isitoshe kama kuna mwenye ushahidi apeleke Takokuu badala ya majungu.”
Kapende anamponda Bi Sofia kwa kusema: “We mama ninakuheshimu. Unataka kumdanganya nani eti tupeleke ushahidi Takokuru? Tangu lini mbwa akamng’ata aliyemfuga? Kama ni siasa zako uchwara na za kisanii wafanyie kina mama wenzio si sisi.”
Bi Sofia siku zote ni mbishi kweli kweli. Hakubali. Anakatua mic: “Kwanini nyinyi watu hamna shukurani jamani? Yaani juhudi zinazofanywa na mtukufu rais hamzioni?” “Juhudi gani?” anauliza Msomi kwa mshangao.
Sofia anajibu: “Hivi hamkusikia kuwa ameleta mwekezaji toka Oman kuja kupambana na unga pale Uwanja wa Ndege wa Mwalimu, mnaishi dunia gani?”
Mpemba aliyekuwa kimya akitafuna kahawa yake anaamua kuingilia: “Weye bibi usitake kuntibua miye. Wewe wadhani kwa kuleta huyu mmanga ndovu wetu watapona ukiachia mbali unga kuendelea kupitishwa kihalali?”
Huku akionesha kebehi ya wazi, Msomi anasema: “Ameleta muarobani eeh! Loliondo nyingine hii.”
Baada ya bi Sofia kuona maji yanazidi unga anaamua kujikata kisilesi. Anasema: “Kumbe niliacha chungu mekoni! Ngoja niwahi nisije unguza mboga.”
Mbwamwitu hamkawizi. Anamsindikiza kwa kejeli: “Ushaunguza kaunguza na hiyo mboga ya mumeo.” Sofia hajibu. Anatokomea kwa aibu.
Baada ya bi Sofi kujikata kinoma, Mijjinga anaendelea kuning’ang’ania. Anasema: “Mzee Mpayukaji, wanene wameshindwa kutajaga basi wewe tajaga.”
Anaendelea kwa utani, “Tutakuminya hadi utaje.”
Kupoteza mada naamua kumjibu: “Mtaanzia wapi kuniminya? Nenda kawaminye kina Mwakiembe na Lukuvie woga lakini si mimi.”
Kanji ambaye ashaanza kuniogopa anaamua kujipendekeza: “Hapana minya Payukaji. Taumiza yeye bure.” “Basi tutakuminya wewe utaje wenzio,” anasema Mijjinga.
“Hapana minya mimi, iko innocent dugu yangu. Sisi sote dugu moja, hapana haja minyana minyana.” Kanji anajitetea. Kijiwe hakina mbavu jinsi Kanji anavyobukanya Kiswahili na hofu yake ya kuminywa.
Msomi kama kawaida yake anataka kuokoa jahazi. Ananigeukia na kusema: “Hebu mheshimiwa Mpayukaji tupe ukweli. Je, unayajua majina ya wauza bwimbwi au nawe ulitaka kutufanyia majaribio ya siasa za sanaa kama wale?”
Nami simkawizi. Nampa laivu: “Kwani wewe huwajui wauza unga?” Nauliza nikiwa namtazama Kanji ambaye anatoa mimacho kwa hofu kuwa huenda nitamtaja.
Kanji anaamua kujitetea: “Naona angalia mimi dugu yangu. Siminye mimi hapana uza bimbi. Mimi uza guo na spea parts bwana.”
Mijjinga hafichi uchu wa kutaka kujua majina ya wauza bwimbwi. Anasema: “Heri tuminyane majina yatajwe kuliko kuminyiana yakaishia kapuni.”
Kijiwe kikiwa kinapamba moto, si kunguru alinaswa na umeme na kusikika sauti ya mlipuko mkubwa. Acha kila mtu akitoe kuokoa roho yake!
Chanzo: Tanzania Daima Sept.,11, 2013.

No comments: