Wednesday, 25 September 2013

Kijiwe chalaani uhuni MjengoniHAKUNA kitu kimewafanya wanakijiwe kuchukia kama kushuhudia ujinga unaofanywa na Jobless Nduguy Mjengoni. Kwa vile analala kitanda kimoja na Chama Cha Machakachuaji, basi anadhani kila mtu aweza kujirahisi kama yeye. Uchakachuaji wa katiba ni uchangudoa wa kimaadili unaopaswa kupigwa vita.
Kapende leo kawahi kijiweni. Ana ajenda muhimu ambayo angependa ijadiliwe kiundani na utuo. Ametungoja ili tuanze kufanyia kazi kadhia inayofanywa na watu wasiosoma alama za nyakati.
Analianzisha: “Waheshimiwa wajumbe, nini mawazo yenu kuhusiana na hii hujuma ya wazi dhidi ya katiba?”
Mpemba anakuwa wa kwanza kutia guu. “Mie nshangaa sana hasa huyu Njaa Kaya. Alipoanzisha nchakato wa katiba mpya alianza uzuri. Ila kama atasaini huu upuuzi uliopitishwa na vipofu wasiosoma alama za nyakati ajue hakutakalika.”
Mgosi Machungi anakatua mic. “Kama Njaa Kaya ataamua kujivua nguo hiyo shaui yake. Kwani hakuna aliyemlazimisha kuanzisha mchakato.  Isitoshe kwanini atumie njuuku zetu kufanyia usanii kama atakubali kusaini upuuzi?”
Kapende anazidi kuonyesha wasiwasi wake. “Mie sina imani na yeyote hadi tupate kitu kipya kinachoendana na matakwa yetu. Maana kisheria katiba ni mkataba kati ya watawaliwa na watawala na si utashi wa chama chochote hata kiwe na madaraka namna gani.”
Mzee Kidevu anamkonyeza mzee Maneno kwa jinsi Kapenda anavyojitia kujua sheria.
Mipawa hajivungi. “Beng’we, usemayo ni kweli. Tusiamini mtu hadi tuonage katiba mpya. Huwezi kujua. Huenda jamaa alitaka kupata sifa kama Beni Nkapa aliyeanzishaga Tume ya Waliboa halafu akaiua baada ya kumgusa pabaya. Umesahau wasanii wetu siyo?”
“Hata mimi siwaamini hawa jamaa. Maana nikikumbuka jamaa alivyotuingiza mkenge akidai ana majina ya wauza bwimbwi halafu akaishia kuwagwaya sina hamu,” anachomekea mzee Kidevu.
Msomi Mkatatamaa hajivungi. “Wasemaji wote mna hoja hasa wakati huu tunapoburuzwa na kutawaliwa na wababaishaji na vigeugeu. Hamkumsikia jamaa akijitapa kuwa kwa sasa watapambana na wauza unga? Je, kwa miaka nane yote walikuwa wapi kama si kutaka kutugeuza mabunga?”
“Jamaa kipindi hiki kweli atapambana na wauza unga kwa kutowasaidia wakikamatwa ughaibuni. Anajua fika kuwa hawatakamatwa kayani kwa vile wanajuana,” anaongezea Mzee Maneno.
Baada ya kukatua kashata lake Mpemba anaamua kutia guu tena. “Yakhe mie hawa watu sina imani nao pia. Hivi huyu jamaa anayejisifia kila siku haoni mtu wake Jobless Nduguy anavyonajisi na kubaka Njengo alo geuza kuwa genge la wahuni?”
“Unaongelea huyu aliyewatukana wenzake kuwa wanavuta bangi na kubwia mibwimbwi? Sijui kama havuti alijuaje wenzake? Mwenzenu napanga siku moja timtokee Mjengoni timzabe vibao. Kwani Mjengo ni wa familia yake? Jitu limeshindwa kulhali. Linaongoza jimbo lenye wachovu kuliko wote kayani bado linajitia ubabe. Kama mbabe si akapambane na matatizo jimboni mwake,” anaongea mgosi Machungi kwa hasira. Kijiwe hakina mbavu jinsi anavyoongea kwa usongo.
“Si matusi tukisema Mjengo umeingiliwa na mdudu mbaya anayeunyevuanyevua.  Unavyoendeshwa utadhani baa. Jobless anakuja na hili huku Makidamakida akija na lile. Umefilisika. Si Mjengo ule tuliozoea wa viwango tena,” anachomekea Mijjinga.
“Mlitegemea nini baada ya kusimikwa Makidamakida ili kunusuru mafisadi?” Anazoza Kapende ambaye leo amechukua tuzo ya kumwaga mipwenti.
Kanji aliyekuwa akinong’ona na Bi Sofi Lion anaamua naye kutia guu. Anasema: ”Hii Dugai mimi jua yeye. Hapana kosa. Kama Bunge naenda piga kelele tatoa nje yeye.”
Bi. Sofi anampa tafu mara moja, “Mnamuonea mheshimiwa bure. Hivi mlidhani angeruhusu wahuni kufanya bungeni mahali pa kufanyia rap?”
“Kumbe Kanji na Jobless lenu moja!  Kama unaongelea Mista Two umemuonea. Yeye si bwege wa kutumikia chama badala ya kaya. Alichofanya walipaswa kufanya wenzake wote ili kulinda heshima ya wachovu.”
Msomi aliyekuwa akiandika ujumbe mfupi kwenye simu yake anaamua kurejea tena. “Hii ndiyo hasara ya kubambikiwa kanyaboya. Kwani hatujui kuwa mzee wa viwango, Sam Sixx aliondolewa ili kuruhusu tunachoshuhudia. Wasioeleweka wanapewa mamlaka ya kusimamia taasisi nyeti kama Mjengo? Nashauri mwakani tujiunge pamoja na kuhamasishana kuhakikisha wote waliounga mkono huu uhuni wapigwe chini wajue kaya si mali ya mama zao wala chama chao.”
“Hata Sam Sixx ni fisadi tu. Hamkuonaga alivyopewaga zawadi ya ulaji na kutelekeza kaya hasa pale walipokubalianaga na Mwakiwembe na Matomatoes wachukue ulaji na kumnusuru Njaa Kaya kwenye soo ya Richmonduli?” Anapayuka Mipawa.
Kapende anaamua kumjibu Bi Sofi kinamna. Anakwanyua mic. “Hivi yule bi mkubwa wa kucheza Makidamakida ashaolewa au ni open check?  Inakuwaje tunawaweka watu kama hawa kwenye nafasi nyeti kama hizi?”
Bi Sofi kapata meseji yake. Anauliza kwa hasira akimkazia macho Kapende. “Hivi mtu akioa au kuolewa wewe yakuhusu nini?”
Kanji naye anaamua kumuunga mkono kada mwenzake. “Kama oa muhimu kwani vatu nyingine naoa au olewa nazini?”
“Wanazini kama wewe siyo?” Anachomekea Mbwa Mwitu.
“Mimi pana zini dugu yangu.” Kanji anajitetea.
Msomi anaamua kurejea kuokoa jahazi. “Kanji uzini usizini hiyo shauri yako. Muhimu hapa ni kujadili jinsi ya kunusuru kaya yetu toka kwenye mikono michafu ya wahuni. La muhimu kijiwe kimwandikie barua Njaa Kaya kumshauri asikubali kugeuzwa bozi na wahuni kusaini mswaada uliochakachuliwa. Nadhani ule wa kwanza aliosaini unatosha na lazima atakuwa amejifunza. Awapuuzie akina Chikwawe wanaobembeleza ulaji chamani mwao.”
“Yakhe usemayo kweli. Badala ya kulalamika lazima tufanye kitu lau dunia ijue. Napendekeza tuandamane kwenda Mjengoni kushinikiza Jobless na  Makidamakida watimuliwe.” Mpemba anachagiza.
“Nendeni mpigwe na kutimuliwa kama mbwa koko. Kama wamepigwa wakubwa zenu itakuwa nyinyi?”  Anafoka Bi Sofi huku akiwakazia macho Kapende na Mijjinga.
“Huyu kanunga hawezi kutuchokoza na kutudhalilisha hivi. Sasa nasema tuanze safari ya kuelekea mjengoni tuwaonyeshege tulivyo vidume.” Anapayuka Mijjinga kwa hasira.
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si tukalianzisha kuelekea Dom kwenda kuwalaani Jobless na Makidamakida na kutaka waondoke Mjengoni. 
Chanzo:Tanzania Daima Sept., 25, 2013.

No comments: