Tuesday, 17 September 2013

Kijiwe chashangaa mipasho ya Njaa Kaya

JAPO  siku zote Mpemba ni mtu wa utani na bashasha, leo kuna jambo limemtatiza. Maana alivyoingia akiwa na ndita usoni, si haba. Kuna jambo tena kubwa tu.
Anaingia akiwa anajifuta kijasho na kuamkua, “Asalaam alaykum jamia.” Wote tunajibu, “Alaykum wasalaamu.
Hakawii wala kungoja kuulizwa kilichomsibu. Anakwanyua mic right away, “Yakhe mmesikia hayo matusi ya nguoni tena nchana ya huyo mtu wenu?” “Yupi kaka mbona sikuelewi?” Anajibu Kapende.
Mpemba hazungushi, “Si huyo Njaa Kaya anayesema eti wale wote tusokubaliana na ahadi hewa, mihadarati, ufisi na ufisadi tutaja umbuka akimaliza. Au hamkusikia alipokuwa kule kwa kina Mipawa na Mijjinga akitamba?” “Alaa! Kumbe unaongelea jamaa aliyesema kuwa atakapokuwa ameondoka ulajini watu wasiokubaliana naye wataumbuka kwa vile anaona amefanya mambo makubwa?” Anajibu Kapende huku akibwia kahawa yake.
Msomi Mkatatamaa hakawii, anatia daruga na kuzoza, “Atakayeumbuka yeye. Hata hivyo, aumbuke mara ngapi iwapo kutaja wauza unga na kutaja mali zake vilishamuumbua zamani? Hivi huyu jamaa anadhani wachovu wote ni majuha kama wale aliojizungushia wakimsifia? Ana lipi la kujisifia iwapo kaya imejaa wauza unga, mafisadi, majambazi, wala rushwa na wahalifu wengine kila aina?” Bi Sofia Lion ambaye ndiyo alikuwa anaingia akiwa ametinga kimini kiasi cha kumfanya Mpemba amkate jicho huku akilalamika kuwa anamuondoa udhu alikamua mic, “Hivi tuseme mara ngapi muelewe kuwa mtukufu amefanya mambo mengi makubwa? Hivi hamuyaoni au hamna macho kama wapingaji ambao hupinga kila kitu?” Kanji anadandia mic kumpa tafu mkereketwa mwenzake. Anasema, “Kweli tukufu fanya mambo mingi sana. Ona amani, pendo, tajiri na tulivu kona yote.” Sofia kupata kampani anaamua kumwaga radhi tena, Kanji wapashe hawa wenye wivu wa kike wapashike. Hivi mlitaka awaletee pesa ya kula jamani?” Mgosi Machungi anaamua kujibu kwa utani, “Kwani si aliahidi maisha bora kwa sote. Hatikumlamisha. Yako wapi maisha boa iwapo kila mtu anajiibia atakavyo na asifanywe kitu?” “Kumbe hata wewe Chungi iba?” Kanji anatania.
“Kitoe hapa Kanji na kanungaembe kako haka ambako siku zote mnnatetea ujinga,” Anajibu Mijjinga huku akimkazia macho Kanji na kukwepa macho ya Sofia ambaye amenuna kuitwa kanungaembe.
Anaendelea, “Kuna siku nitawafanyie kitu mbaya msipoacha huu mchezo mbaya wa kutumiwa.” Kabla ya kuendelea, Mipawa anaamua kuchomekea, “Wanatumiwa vipi na kwanini wajirahisi kutumiwa tena vibaya mbona huko nyuma hawakuwa hivyo?” Mgosi Machungi ambaye alikuwa akichezesha saa yake anayojisifia kuwa ya bei mbaya aliamua kutia buti. “Jamani tiseme ukwei. Mimi nilimiona jamaa huyu kwenye uninga yangu ya bei mbaya jana usiku.” Kila mtu hana mbavu jinsi mgosi anavyojisifia kuwa na runinga.
Anaendelea wala hajali, “Nilimisikia akisema eti atavunja ekodi kwa kupeeka umeme vijijini na kujenga baabaa. Upuuzi mtupu. Umeme unaupeeka kwenye tembe huku ukijisifia kujenga baabaa ambazo zinabomoka hata kabla ya kuzinduiwa? Mbona kue kwetu Ushoto sijaona huo umeme?” Mzee Maneno anaamua kukwanyua mic na kudema kama hana akili nzuri, “Jamaa ameonyesha kutugwaya sisi tunaompa vipande vya kishua tukimshushua tusijue naye atatustua na kutushushua kwa kujisifu. Inaonekana hana kumbukumbu. Mara hii kasahau alivyoshindwa na kusema kuwa raha jipeni wenyewe? Sijui kama wachovu wanaweza kula huo umeme ukiachia mbali umeme wenyewe kuwa wa kulanguliwa na migawo.” Mbwa Mwitu anaamua kutupa kijembe, “Sijui kwanini bado mnataka awape raha wakati raha hana bali karaha kama EPA? Kama mnataka raha bwieni bwimbwi. Jamaa kisharuhusu na mkishakuwa mateja atawapa mwaliko mwenye kunywa naye chai.”   Msomi leo ana usongo sina mfano. Anaamua kurejea kwa kejeli, “Jamaa anajua kuwa alipiga mzigo uwe wa hovyo au vinginevyo who cares guys? Kweli wataumbuka wanaodhani kuwa barabara za kiwango cha lami lakini chini ya viwango ni mali kitu.” Mzee Kidevu anaamua kuchomekea, “Wachovu hawahitaji viwango na isitoshe huenda rahisi ajaye atazuia watu kufanya biashara ya miunga na kukwapua njuluku za kaya kiasi cha wanufaika kumkumbuka mtu wao. Nadhani aliongea kwa mafumbo akimaanisha hili.” Sofia aliyekuwa amenuna anaamua kujivuvumua na kumwaga pumba sorry pwenti, “Acheni roho mbaya. Mtukufu aliahidi maisha bora na kila mtu ana maisha bora ndiyo maana mnaweza kuja hapa kunywa kahawa bila kusikia milio ya risasi. Isitoshe kila mkoa sasa utafaidi umeme.” Anaongea akimtazama Mipawa.
Mipawa hajivungi. Ameipata na kuamua kujibu, “Ingekuwa ni amri yangu ningenyonga wapuuzi wote wanaosifiana. Huyu jamaa hana adabu. Yaani anakwendaga kwetu kutangazaga upupu eti ni mafanikio!
Msomi leo amepania. Anakwanyua mic, “Bi Sofi tuache utani. Kama ameleta maisha bora basi ni kwenu wakereketwa na waramba viatu lakini si kwa wote kama alivyoahidi. Maisha bora hata kama yanatokana na jinai kwa wote itakuwa ndoto ya mchana. Jinai haiwezi kuwa mkombozi wa wanyonge. Huenda amesema vile kwa vile anajua uchaguzi wa kuchakachua na takrima utakausha mshiko wa kaya kiasi chamaisha kuwa magumu zaidi. Hivyo serikali ijayo kuishia kubeba lawama zake.” Kabla ya kuendelea Machungi anachomekea, “Hata hivyo, tinampongeza kwa kutitonya mapema ili tujue la kufanya na kujiandaa kisaikoojia. Hata hivyo, mie naona hatitaumbuka isipokuwa yeye na sanaa zake na wenzake.” Anamalizia akiwatazama Kanji na Sofia.
Kuona jinsi kijiwe kilivyowasakama Kanji na Sofi wanaamua kuondoka bila kuaga. Mbwa Mwitu anawasindikiza kwa utani, “Kanji leo umeopoa siyo?” Kanji hajibu.
Mpemba naye anachomekea, “Huyo andanganya bi Sofi. Kama wenzake wakimuona naye watansusa wallahi. Maana hawa jamaa kwa ubaguzi sina hamu miye. Hawa wabagua kila kitu chetu isipokuwa vyakula na nyumba na pesa yetu.” Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si mwenye nyumba wangu katokea!  Kwa vile nilikuwa nampiga chenga asiniumbue kutokana na kutolipa kodi ya ubavu wa mbwa, niliamua kujikata kama vile nakwenda msalani ili kisiumane. 
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 18, 2013.

No comments: