Saturday, 28 September 2013

Mlevi aanzisha dhehebu la UFANISI


Baada ya kugundua siri ya utajiri wa kutisha wa baadhi ya mapatepeli wanaojiita watu wa Mungu, mlevi `nimesukuti’ sana.
Kwa vile mimi si tapeli (ni mtu wa Mungu) basi nitaanzisha dhehebu liitwalo Super Uncontaminated Clerical Congregation of Enligthened  and Saved Souls (SUCCESS) kwa `Kimakonde’ sema UFANISI (Ufufuko wa Nabii Aliyejuu Neema wa Isiyokwisha Salama na Idumuyo) ili kuwakomboa walevi wanaonyonywa na kuibiwa na matapeli.
`Wakameruni’ huita hii kitu ‘All Faiths Organized under One Leader’ (AFOOL).  Sina ubaguzi wa dini wala uduni uitwao udini. Nafanya hivyo ili kuhudumia watu wa dini zote.
Hili ni dhehebu la uhakika.  Si kama yale ya akina Life Changer International yaliyokuwa yakiendeshwa na matapeli wa ki-Nigeria kabla ya kugundulika kuwa kumbe ni wahamiaji haramu waliokimbia njaa kwao na wengine kesi mahakamani.
Ingawa iliitwa Life Changer International maana yake ni Life Ruiner Intentional. Hata na wachovu wetu wamezidi. Yaani mnatapeliwa kama hamna akili!
Badala ya kuchapa kazi kwa bidii mnaendekeza ushirikina. Mtaliwa na mtakwisha hata kama mmezoea kuliwa. Matapeli wa kisiasa wanawatapeli. Matapelil wa kidini wanawatapeli.
Kwanini msitapeliwe au muache uvivu wa kufikiri? Je, serikali nayo inayosajili huu upuuzi tuiweke kapu gani? Kwangu ni rahisi kukubaliwa. Kwanza natokea Ukanadani siyo nchi maskini kama hawa matapeli.
Kwa vile huku Ukanadani nimepigikia, basi njia ya kujipatia `fweza’ ni kurejea `Bongolalaland’ na kutengeneza ukwasi kwa jina la Mungu. Lazima nije kupambana na matapeli waliojaa roho mtakakitu kwa roho Mtakatifu.
Nitahubiri kwa kiingereza kiswahili na kiarabu ili kuwavutia wote. Lazima nitafanikiwa `kuukata’ haraka kama jamaa ambao wengi ni `vihiyo’ na walikuwa apeche alolo sasa wanaishi kwenye mahekalu.
I will be working under Holy Ghost but not working under gory ghost like them.
Nina PhD za Saikolojia na Maandika Matakatifu (Psychology and Sacred Writings) nilizopata kwenye Chuo Kikuu cha Guelph---kile kilichompa shahada ya `dezo’ Rahisi wenu hivi karibuni, na Chuo kikuu cha Al Azhar huko Masri. Hivyo mambo yangu yatakuwa mswano within no time.
Nitahubiri utajirisho miujiza na uponyaji kwa wote bila kujali dhambi zao. Vyangudoa wataombewa wapate wateja. Nitafanya miujiza kiasi cha `ndata’ wanaowasakama wageuke wateja wao.
Nitaponya hata kwa kugusa picha yangu au kusikiliza kanda niliyorekodi sauti yangu. Onyo, maombi na uponyaji wangu vitafanya kazi kwa wenye imani nami tu. 
Hivyo, njoo ufaidi miujiza utapona kwa kusoma machapisho yangu, uhitaji kwenda Mwanyamala au Muhimbili kutolewa upepo na madaktari feki waliotamaliki kaya nzima.
Kwa vile dini yangu ni ya kweli na wote, sitatumia magazeti wala runinga kutangaza mahubiri yangu kama wanavyofanya wale wafanyabiashara wa roho za wajinga na makapuku waliokata tamaa kiasi cha kutapeliwa kirahisi.
Watapeliwa nawashauri wasikilizie ujumbe wa Profwesa Anna Kajuamlo Tiba ya Ijuka, aliyewaambia akina mama waliotapeliwa kwa jina lake kuwa wanapenda kutapeliwa. Kuweni wajanja. Njoo kwangu.  Msikubali kutapeliwa na wezi waliojificha kwenye dini.
Kama alivyosema Yesu kwenye Matayo 7:15-16, hao ni fisi waliovaa ngozi ya kondoo. Pia someni tena kwa makini Matayo 24:3-5 isemayo kuwa watakuja wengi kwa jina langu na kupoteza wengi.
Kwa wanasiasa ukitaka uongozi njoo kwangu utashinda uchaguzi bila kuhangaika na kutoa takrima, kujikomba kwenye chama chako wala kupiga kampeni. Hata hao wanasiasa waliofanikiwa walikuja kwangu na mambo yao yakanyooka hata kama hawasemi kwa kuogopa kumwamsha aliyelala wakalala wao.
Makapuku, ukitaka utajiri jua umefika huna haja ya kuua mazeruzeru, kutakiwa ulete ndevu za bibi wa bibi wa bibi wa babu yako na kubaka watoto wala kutembea na waganga wa kienyeji kwa akina mama.
Wanandoa au waliokuwa wanandoa wakapigwa karata, ndoa yako imevurugika njoo hasa akina mama ulale kwangu siku saba ndoa yako itanyooka.
Wale wanaosaka uzazi na watoto, umeshindwa kushika mimba? Njoo nikufanyie dawa upate mtoto. Je una tatizo la kupata mchumba?  Dada njoo ulale kwangu kwa siku 14 utapata mchumba tena mwenye pesa.
Kama unataka kushinda mtihani bila kusoma wala kupoteza muda kwenye shule za kata we njoo kwangu mambo yako yatanyoka. Je, unasumbuliwa na majini? Dua zote ziko kwangu. Naongea na majini na kula na kunywa nayo.
Je, unataka kumsomea mbaya wako albadir? We njoo tu shida yako itageuka historia.Tuache utani. Dhehebu langu ni kiboko ya matatizo. Siyo kama yale madhehebu ya watu wenye majina ya ajabu ajabu kama vile Rwakatarehe, Gamanyua. Ka-tortoise, Mwaka wa Senger, Lusekelelo na matapeli wengine wengi wanaosukumwa na uroho mtakakitu wanaosaka utajiri.
Nina uwezo wa kuombea hata uchumi wa kaya ukawa mswano kama ule wa China. Hivyo, rahisi na waziri wa `njuluku’ waje kwangu wapige goti nitaombea uchumi na kila mtu atapata maisha bora.
Mimi ni tofauti na wale wanaoanzisha vijidhehebu uchwara halafu wakataka kujipatia umaarufu kwa kudai wanaombea amani kayani na upuuzi mwingine.
Wengine wanatunga nyimbo za kusifu chama tawala na viongozi wake ili wawe karibu na ufisadi watajirike. Mie ni tofauti kabisa ingawa msitu ni ule ule lakini nyani tofauti.
Nafanya miujiza ya kweli na si mauzauza kama ya wale wanaojaza viwanja vya Jangwani na kuondoka na mshiko. Kwa wale wote waliovuruga na kubomoa ndoa zenu kwa midomo na mikono yenu na tabia chafu, waliokata tamaa za maisha, wenye tamaa za kuukata njoo kwangu yote yatakuwa historia.
Chunga usiingizwe mkenge. Naona mama mchungaji anakuja. Acha niishie nisijevuruga ndoa yangu nikaanza kutapeliwa kama hawa ‘ninaowaombea.’ wahenga walisema:
Wajinga ndiyo waliwao na mwalimu wangu usinibaini nikipata kumi tano zako. Wenye macho na wajionee. Wenye masikio na wasikie na wenye akili na watafakari. Mambo yakiendelea hivi mtajikuta mateka wa matepeli kaya nzima. Tasfsirini sura hii tukufu: Inna a'taynaka al-kawthar, Fa-salli li-Rabbika wanhar, Inna shaani-aka huwal abtar.

Chanzo: Nipashe Sept., 28, 2013.

No comments: