Tuesday, 1 October 2013

Mpayukaji anusurika shambulio la kigaidi

BAADA ya kugundua wale akina Nduguy na Makidamakida tuliokuwa tunakwenda kuwatia kasheshe hawakuwapo mjengoni, nilikwenda zangu Nairobbery kwa washikaji wa vijiwe vya kule. Nilitua River Road, Muindi Mbingu, Lavington na Westgate.
Nilizurura kweli na kuwasalimia washikaji zangu akina Njoroge, Muthamaki, Mtongolya na wengine wengi.
Nilialikwa kwenye mkutano wa kimataifa wa vijiwe kujadili jinsi ya kupambana na wahamiaji haramu vijiweni. Wenzetu hata kama wana uhovyo wao, wanajitahidi. Ukikanyaga Namanga tu unaulizwa pasipoti. Nilijihami na pasipoti yangu iliyokuwa inaanza kuota ukungu. Tangu nilipotoka Libia wakati wa mauaji ya Kashaffi, sikuwa nimekwenda popote.
Leo kijiwe kimekaa kusikia mazonge na kasheshe nilizopambana nazo. Kila mwanakijiwe alikuwa amepewa taarifa za kuwapo kwangu kwenye sekeseke la Westgate. Hakuna kilichowavutia wanakijiwe kama kugundua kuwa kumbe mimi ndiye niliyeua wale magaidi watano wa al-Shabuub japo niliomba nisitangazwe ili nisijulikane nilivyo komandoo.
Mgosi Machungi ndiye anayelianzisha. Anakatua mic. “Mgosi Mpayukaji kwanza pole na hongea kwa kunusuika na shambuio la kigaidi.”
Najibu haraka. “Nashukuru japo shambulio lile lilikuwa la kitoto.” Mgosi anaendelea. “Hebu timegee hali ilivyokuwa.” Anamgeukia muuza kahawa na kusema: “Hebu mwekee kahawa kidume wa vidume na kiboko ya magaidi.”
Natabasamu kwa ujiko na kuendelea. “Nilipotoka Lavington, nilipitia pale Westgate kununua fegi. Bila hili wala lile si maguruneti na risasi vikatawala. Ghafla bin vuu nilisamasoti na kubana nyuma ya nguzo na kukaa kwenye mkao wa Jet Kune doo. Huu ni mkao hatari katika karate.”
Nakunywa tangawizi na kujifuta kijasho na kuendelea. “Bila kutarajia niliona gaidi wawili wakinimiminia risasi. Sikuamsha mikono. Nilipiga samasoti na kutua juu ya mmoja wao ambaye risasi zake mbili zilinipata moja kwenye kidevu na nyingine kwenye ukucha.  Nilitupa mateke na ngumi na kuwaangusha na kuchukua bunduki zao baada ya kuwanyonga. Sikuona haja ya kupoteza risasi kuua inzi. Ilikuwa ni hii haa woi nyii nyooo, nkupu mwisho kimya!” Wanakijiwe hawana mbavu ninavyoonyesha nilivyowanyonga wale al Shabuub.
Naendelea. “Baada ya kuweka AK 47 na revolver mkononi, nilitembeza karate na kung-fu kiasi cha kuangusha watano ndani ya sekunde chache. Kuona risasi zinaendelea kutawala huku walinzi wa jengo wakiwa wamelala chini, nilianza kuokoa watu. Niliokoa kama mtu zaidi ya 100 tukiwa na jamaa yangu toka Ukamerunini ambaye vyombo vya habari vilimtaja kama shujaa visijue ni swahiba yangu tuliyekuwa tukipata fegi na coffee pamoja pale Westgate.”
Mpemba anachomekea. “Weye Bruce Lee wallahi!” Nilijibu: “Ulikuwa hujui?”
Kabla ya kuendelea, Msomi Mkatatamaa alibwia kahawa yake na kulonga. “Hebu tueleze. Ilichukua muda gani kwa ndata na geshi kufika?”
Nilijibu: “Kaka unaulizia ndata na geshi? Walifika baada ya masaa kama mawili huku wakiwa hawana msaada kutokana na kuelemewa na vitambi vyao. Kuna wawili niliowazaba vibao baada ya kushuhudia wakilala chini kuogopa risasi.”
Mijjinga aliyekuwa na mshawasha wa kuongea anakatua mic. “Unataka kusema ndata na ndutu wa kule nao ni wajawazito kama wale wa kaya?”
“Unauliza jibu!” Nilijibu huku nikutupa kipisi cha sigara. Mipawa anatia guu. “Nyanda unadhani hawa magaidi waliingiaje wasijulikane?”
“Nadhani waliingia kama watalii au walijipenyeza kupitia mpaka wa Somalia kule Kiunga. Ni kwamba waliwahonga ndata wa mpakani na kuingia.” Nilijibu na kunywa tangawizi kisha nikaendelea: “Japo wenzetu wameonyesha udhaifu kwenye medani, hawauzi pasipoti zao kama kwetu ambako zinauzwa kama njugu. Pia, hawana simile na wahamiaji haramu. Hata hivyo, vyombo vyao vya usalama vinapoteza muda mwingi kupambana na makonda na mamantilie na mashahidi dhidi ya waishiwa wao mbele ya ICC. Tofauti na kayani ni kupoteza muda na rasilimali kwenye kukimbiza wapinzani na kulinda mafisadi.”
Kanji aliyekuwa akiongea na Sofia aliamua kukatua mic. “Payukaji pole sana. Kwanini sema polishi na geshi yetu hovyo? Hapana ona amani chini!”
“Amani kwako na wenzako siyo? Laiti ungejua kuwa mfumo ambao unalinda ufisadi na ubabaishaji ndicho chanzo na sababu ya jamaa kuzidiwa kete na wahuni na makafiri wachache usingeongea hayo.” Namjibu kwa kebehi. “Sasa gaidi na fisadi kuwa kitu moja vipi?” Kanji anajitetea.
“Bado hujui? Unategemea nini, kwa mfano, ndata na ndutu wanapoacha kufanya mazoezi wakafuga vitambi au wanapokimbizana na watu kuwatoa uchache? Unategemea nini taasisi za usalama zinapojiingiza kwenye siasa za kichovu? Au mnangoja yatufike ndipo mstuke?” Nazidi kumpigilia misumari ya mapwenti.
Niliendelea: “Baada ya kutembeza makarate na making-fu yangu nilikutana na Rahisi Kinyata aliyependekeza nipewe nishani ya juu ya ushujaa. Niliikataa na kumtaka aendelee kuwajibika. Hiyo ndiyo tuzo ambayo ningeipenda. Pia, nilishauri apambane na vikundi vya kijinga vya kihafidhina na mashehena njaa wanaotumia uhuni kupata ujiko na ulaji.”
Mzee Maneno naye anatia timu. “Umesema kuwa risasi mbili zilikupata kwenye kidevu na ukucha. Mbona sioni jeraha kwenye kidevu chako?”
“Mzee vipi? Huoni kidevu changu kilivyopungua! Risasi ilichoma ndevu tu na ule ukucha uliopigwa na risasi nimeukata tu. Hivyo sina jeraha.” Nilijibu huku kijiwe kikiwa na shaka na tukio hili kisijue mie ni komandoo niliyesomea kule Czechoslovakia na Cuba.
Bi Sofia naye anaamua kutia timu. “Mpayukaji hebu tupe ukweli. Unadhani hili lingetokea kwetu wangefanikiwa kutokana na kuwa na ulinzi wa hali ya juu duniani?”
“Go tell it to the birds Sofi. Kuna usalama gani wakati taasisi zetu za usalama zimegeuka uhasama wa taifa? Wameshindwa na mafisadi kama Kagodaa na HEPA wataweza ngoma hii? We kubali usimuliwe. Usishuhudie.” Namjibu na kuendelea kukata coffee kama sina akili nzuri.
Mpemba anaamua kurejea. “Bi Sofia acha uhafidhina na mapenzi ya kibubusa. Hapa unadhani kuna kitu au ufisadi? Watu wajiingilia mbele na nyuma hakuna anayejali. Wadhani hata hili zoezi litawamaliza? Wataisha waso na pesa ya kuhonga. Hawa wajalaana wangevamia kwetu wangeua kaya nzima.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si daladala likapata pancha. Tulidhani al-Shabuub wameingia kwetu. Kila mmoja alitoka mkuku kuokoa roho yake.
Chanzo: Tanzania Daima Okt., 2, 2013.

No comments: