Wednesday, 30 October 2013

Kikwete akiamua anaweza kuondoka shujaa
RAIS  Jakaya Kikwete, ingawa  wapo wanaomuona kama dhaifu tangu aingie madarakani, anaweza kubadili mwelekeo wa mambo na kuwa shujaa. Anaweza kufanya hivyo kama atafanya yafuatayo.
Mosi, kukiacha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijifie kutokana na kuishiwa kulhali. Anaweza kufanya kama alivyofanya rais wa mwisho wa lililokuwa Shirikisho la Kisoviet la Urusi, Michael Gorbachev. 
Pia anaweza kufanya kama rais wa zamani wa Romania, Ion Iliescu aliyekataa kuunga mkono uimla na umwagaji wa damu wa imla wa zamani wa Romania, Nicolae Causescu.
Pili, anaweza kufuta kile wakosoaji wake wanachoona kama ni makosa kwa kubadili aina yake ya utawala. 
Ingawa amebakiza muda mfupi madarakani, anaweza kuamua kuweka mfumo na mazingira ya watakaofuatia kurekebisha makosa ambayo mengi aliyarithi toka kwa mtangulizi wake aliyeiuza nchi kwa wawekezaji uchwara huku akihujumu kila rasilimali ya Taifa.
Tatu, anaweza kuendelea kuiandaa CCM kisaikolojia tayari kukabidhi madaraka kwa wengine wenye uwezo na kukubalika kwa wananchi.
Nne, anaweza kuachana na kile ambacho wakosoaji huita kuwafumbia mafisadi macho chini ya dhana mbovu ya ‘huyu ni mwenzetu’ ambayo kimsingi ndiyo imetufikisha hapa tulipo.
Tano, Kikwete anaweza kutumia mbinu mbadala ya kulibadili Taifa kwa kufanya mabadiliko kwa njia ya kupinga na kukataa mazoea ya kutawala kwa kuegemea kwenye maamuzi ya chama ambayo ndiyo silaha kubwa ya CCM.
Sita, anaweza kuangalia utaifa zaidi ya ukereketwa wa chama kama ambavyo imekuwa siku zote ambapo watu hufanya madudu na kutenda jinai kwa kisingizio cha kulinda maslahi ya chama. Rejea kwa mfano kuhusishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba na makosa ya kigaidi kwa kubambikizia wenzake makosa anayotenda.
Saba, anaweza kuamua kupingana na makada wote waliomzunguka wakimshawishi aendeleze uhohehahe kisiasa ili kuinufaisha CCM ambayo kimsingi ilishachokwa na Watanzania kutokana na kuendelea kuwazamisha.
Nane, anaweza kutumia miaka miwili iliyobaki ya kuwa madarakani kufanya yote mazuri na ya lazima aliyoacha kufanya kwa miaka nane iliyopita.
Tisa, anaweza kuanza kuandika historia mpya ya urais wake kwa kuendelea na mageuzi ya kweli ya kisiasa badala ya maigizo na sanaa za CCM. Mfano, anaweza kuzuia CCM kuendelea kuamrisha tume ya uchaguzi wakati wa uchaguzi kama ilivyotokea kwenye uchaguzi mkuu uliopita ambapo baadhi ya wabunge walioshindwa waliidhinishwa kwa mtutu wa bunduki.
Kumi, kwa vile ameishawaambia wazi CCM kujiandaa kisaikolojia, anapaswa kuendelea kuwaandaa akipangua wale wote wenye mawazo mgando na kufanya yale ambayo wasingetaka yafanyike kwa vile yatakiumiza chama.
Kwa mfano, anaweza kuamua kupambana na ufisadi, ujambazi, rushwa, matumizi mabaya ya fedha za umma, kutowajibika kwa watendaji wa umma. Kwa mfano, Kikwete anaweza kuanzisha vita dhidi ya wezi wa pesa za umma ambao wizi wao huripotiwa karibu kila mwaka na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Hesabu za serikali (CAG). 
Anaweza kuibadili Tanzania toka kwenye kuwa shamba la bibi na kuwa mali ya Watanzania ikiwanufaisha badala ya kunufaisha genge la watu wachache wanaotumia chama kushika hatamu kuliangamiza Taifa.
Anaweza kuachana na mfumo wa kujuana na kulipana fadhila. Kama ni kulipa fadhila, nadhani alizokwishalipa na aliowalipa wanatosha.
Kwa vile Kikwete haruhusiwi kugombea urais tena kisheria, hana cha kupoteza bali kufaidika kwa kuleta mapinduzi tena ndani ya kipindi kifupi. Hili linawezekana, linamfaa na asipoteze fursa hii ambayo Waingereza huita golden chance.
Kikwete si mjinga kiasi ambacho wale wanaomdanganya wanamdhania. Anajua fika kuwa kuna maisha baada ya kutoka Ikulu. Ameona wazi jinsi mtangulizi wake asivyo na heshima wala mashiko kwenye jamii ya Watanzania. Amesikia, kuona hata kusoma jinsi wachambuzi wanavyomtumia mtangulizi wake kama kielelezo cha maovu hasa yatokanayo na ufisadi. 
Rejea jinsi mtangulizi wake alivyoandamwa na jinamizi la kuua NBC, kujitwalia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, kufanya biashara akiwa Ikulu, kuruhusu mkewe atumie Ikulu kuunda NGO ya ulaji, kuruhusu uingiwaji mikataba ya kiwizi ya uwekezaji ambao umegeuka uchukuaji na mengine mengi.
Pia Kikwete anajua kuwa Watanzania si wasahaulifu kama CCM ambavyo imekuwa ikifanya makosa na kuwachukulia. Tutoe mfano wa mbali kidogo. Nani, kwa mfano, amesahau kashfa iliyokabili utawala wa rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ya Loliondo?
Kikwete anafahamu fika kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho. Amesoma na kushuhudia historia ya maanguko la vyama kama UNIP (Zambia), KANU (Kenya), MCP (Malawi), NP (Afrika Kusini) na vingine vingi barani Afrika. Ameona machungu ya marais wa zamani hasa wale waliojisahau wakaendesha nchi kama mali binafsi na mali ya vyama vyao. 
Anajua yaliyowapata akina Fredrick Chiluba, misukosuko ya Bakili Muluzi, Laurent Gbago, Hosni Mubarak, Muammar Gaddafi, Zein ElAbedeen Ben Ali na wengine watakaofuatia ambao asingependa awe miongoni mwao. Kama kusoma alama za nyakati basi ndiko huku. Kufanya hivyo humkomboa mhusika na kumpa hakikisho la nafasi katika historia ya Taifa.
Tuhitimishe kwa kuendelea kumpa moyo na changamoto Kikwete asijipeleke mwenyewe majilini wakati ana njia ya kuachia madaraka na kuacha historia ya maana kwake. 
Sidhani kama Kikwete hayajui yote haya wala kama angependa awe muathirka wa mambo ambayo anayajua fika. Sidhani. Afahamu kuwa ataendelea kuishi baada ya urais. 
Pia afahamu kuwa mambo huenda yakibadilika. Yeye aliweza kumkingia kifua Mkapa jambo ambalo limembebesha lawama kwa kusema muache mzee Mkapa apumzike. 
Je ana uhakika gani kama atakayekuja atamkingia kifua wakati mazingira ya kufanya hivyo yanazidi kutoweka kutokana na hamu ya kuwa na Katiba Mpya ambayo ni zao la mabadiliko ya kifikra ya Kikwete? 
Afahamu kuwa kubadili katiba kutampa utajo katika historia ya Taifa na kuwa baba wa katiba na mabadiliko vinavyoweza kunusuru Taifa letu. Hakika Kikwete ana sababu ya kuchagua kumaliza urais wake akiwa shujaa na si mtuhumiwa wa matumizi mabaya ya uongozi. 
Akifanya hivyo, Watanzania watamsamehe makosa yake yote na kuanza ukurasa upya. Kwani naye ni binadamu. Ila asipofanya hivyo, ajue atakuwa rais mstaafu mwenye wingi shaka na misukosuko.

Chanzo: Dira ya Mtanzania Oktoba 2013.

No comments: