Tuesday, 8 October 2013

Kijiwe chataka katiba mpya si hotuba mpya

Baada ya wachovu kushikwa mateka na wanasiasa kwa kuchakachua mchakato wa katiba mpya na kuleta mchecheto, Kijiwe kimeingia full masnonda kutaka katiba mpya.
Mgosi Machungi, anaingia akiwa amekunja uso kutokana na kukosa baadhi ya magazeti mitaani. Anasema, “Wagoshi, mnasemaje kuhusiana na hii jinai ya kufungia magazeti?”
“Waache watapetape. Watafungia magazeti lakini si mawazo yetu. Hata hayo wasiyotaka tujue tunayajua hata bila magazeti,” Anajibu Mijjinga ambaye ameuramba ile mbaya utadhani anafanya kazi benki!
Mpemba aliyekuwa akibwia kahawa anaamua kukatua mic, “Yakhe mie nshawadharau hawa jamaa. Hili la kufungia makaratasi mie halinishughulishi sawa na katiba. Hivi mliisikia khutba ya jamaa yetu?”
“Hotuba gani ami? Wiki iliyopita nimesikia hotuba nyingi sana.” Anauliza Mbwa Mwitu.
“Naongelea khutba ya muishiwa, sorry, mheshimiwa rahisi.” Anajibu Mpemba.
“Kumbe unaongelea hotuba michosho yenye wingi wa maneno lakini ukame wa vitendo? Nadhani tunachotaka hapa ni katiba, si hotuba safi ndefu na zenye kuchosha. Kama ni hotuba tumeishasikia nyingi na hakuna kilichofanyika. Essentially, what we heard was nothing but pre-emptive efforts aimed at a goofy end. "Show not Tell." Simple,” Anasema Msomi kwa hasira.
Bi Sofia Kanunga anaamua kukatua mic, “Hivi nyie watu mfanyiwe nini ndiyo mridhike jamani?”
Kabla ya kuendelea, Mipawa anachomekea, “Tupewe katiba mpya inayotokana na mawazo yetu na si sanaa na mizengwe ya mafisadi.”
Kanji naye anaamua kuingilia kati, “Kwanini fanya haraka? Tukufu kwishasema taleta constitution safi. Kwani hapana amini tukufu?”
“Peleka uzezeta na watukufu kwako huko! Hapa kayani kuna mwanasiasa wa kuaminika au njaa ya kujikomba ndiyo vinakusumbua?” Anajibu Mijjinga kwa hasira.
Kanji hakubali. Anaamua kujitetea, “Jinga kwanini tukana mimi? Hapa sema kuwa vatu sigombee katiba. Kwanini nafanya haraka hivi?”
“Jinga wewe mwenyewe na niombe radhi kabla sijakufanyia kitu mbaya Kanji,” Anachimba mkwara Mijjinga.
Sofia anaamua kuchomekea, “Haya tushayazoea. Watapiga kelele na katiba itachakachuliwa na hakuna kitakachofanyika. Halo halo!”
Inaonekana nyodo za Sofi zimemuudhi sana Kapende ambaye alikuwa bize akibofya kamera yake. Anaingia kwa kinoma noma, “Mijitu mingine sijui imerogwa na nani? Tunanaongea mambo ya maana inatuletea mipasho na uhuni uchwara. Kama unaridhika na upuuzi unaoendelea si uende huko huko badala ya kuja hapa kutujazia mbu. Katiba ni haki yetu.”
Msomi kagundua kuwa mambo yenda ndiyo siyo. Anaamua kuingilia kati, “Wapendwa, kwanza tuache jazba na mipasho visivyo na tija kwa kaya yetu. Nadhani Kapende hajakosea. Katiba mpya ni mali yetu na si mali ya yeyote awe na madaraka au mizengwe. Wanaodhani kuwa hakuna kitakachofanyika wajiandae kisaikolojia kuniona mitaani nikilianzisha hata kama nitakuwa peke yangu.”
Mgosi Machungi anaamua kuongezea utamu, “Kama wataendelea na haya mazingaombwe na sanaa mie nitapiga mtu zongo ohoooo! Timechoka na usani. Show not Tell. It is simple philosophy. Hapa lazima tife na mtu. Lazima katiba mpya ipatikane.”
Mpemba aliyekuwa akinong’ona jambo na mzee Kidevu anasema, “Mwenzenu huenda najipa matumaini. Niliposikia khutba ya bwana nkubwa nilidhani mambo yatabadilika kwa vile ataona aibu kujifedhehesha mbele ya kaumu.”
Mzee Kidevu anatia guu, “Tukubaliane. Hapa kama tutapata katiba mpya basi itatokana na juhudi zetu. Ami hao unaodhani wataogopa kufedheheka mbele ya umma wakati waliishafedheheka unapotea. Wanasiasa wetu hasa wa chama twawala hawana aibu wala kumbukumbu. Walituahidi maisha bora wakatuletea maisha balaa na hawakuona aibu. Wataona aibu kwa kubaka katiba?”
Mipawa anaamua kuingia kwa pawa, “Nadhani kosa kubwa tunalofanya ni kuwabembeleza wababaishaji wetu. Sina ugomvi na mheshimiwa rahisi kusema aliyosema. Ninachojua, wenzake wanataka kumtumia wasijue naye ana akili. Huu ndiyo wakati wake angalau kuonyesha njia na kusahihisha makosa ya chama chake ili aache historia inayong’ara badala ya mauzauza.  Guys, there is tomorrow.”
Kijiwe hakina mbavu jinsi Msukusi anavyobukanya kiingilishi kwa lafudhi ya kikwao. Leo ni kama wanakijiwe wameamua kuonyesha usomi wao usio wa kughushi.
Mgosi anaamua kumuunga mkono Mipawa, “Mipawa you are right. Hatina haja ya kubembeeza kupewa haki yetu. Hii kaya ni yetu sote bila kujali cheo au madaaka.  Kwanini Kenya waling’ang’ana wakapata katiba na sisi tishindwe? Kwani timelogwa na nani?”
“Kama kulogwa umelogwa wewe. Mimi sijalogwa na naahidi mbele yenu kuwa atakayeendelea kuchezea katiba ajue anachezea kijinga cha moto. Wakati umebadilika na watu pia. Lazima nao wabadilike. Kwa vile wameanza na katiba, basi wafuatie na vitendo ili tuelewane ndipo tuheshimiane vinginevyo ni upuuzi mtupu.”
Sofia kaguswa pabaya! Anaamua kurejea kwa hasira. Anasema, “Kama lugha yenu mnayotumia ni hii basi anzisheni chama cha siasa vinginevyo tutaonana wabaya kama nitaamua siasa hizi za kichovu za kijiweni ziishe. Mkiendelea na upuuzi huu nawaitia polisi. Nimechoka ati.”
Kabla ya kuendelea, Mijjinga anaamua kumtolea uvivu Sofi. Anasema, “Sofi, Sofi, Sofi nakuheshimu. Nani unamtishia nyau? Kama unawashwa washwa na kwenda polisi basi acha nikutie mabao upate sababu ya kwenda huko vizuri.” Mipawa anaamka na kutaka kumkabili Sofia ambaye anaonyesha woga wa wazi huku akijaribu kusogea nyuma.
Mara Mgosi Machungi anaamua kumzuia Mijjinga huku Kapende akimtoa Sofia akisema, “Bibie usifanye masihara huyu njemba hatanii. Anaweza kukutia ngeu na uumie bure.”
Huku akihema, Mijjinga anazoza, “Mwambie huyu changu ashike adabu kabla sijamtia adabu.”
Anamgeukia Sofia na kusema, “Naweza kukufanya lolote na nisifanywe kitu.” Anaingiza mkono mfukoni na kuibuka na bulungutu la noti mpyaaa!
Anaendelea kung’aka, “We mama usiye na adabu. Angalia huu mshiko. Unadhani nikienda kituoni nikakata kitu kikubwa kuna atakayekuwa tayari kusikiliza ujinga wako? Shika adabu na adabu ikushike vinginevyo utaumia. Tena nasema ondoka hapa uende ukawalete hao ndata zako.” Anasonya na kukaa chini huku akihema.
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si Mijjinga alimnasa kibao bi Sofi!  Nani abaki ndata wamkute na kumbambikizia kesi kama si kumpiga sachi?

No comments: