The Chant of Savant

Wednesday 16 October 2013

Kijiwe chamshukia Steve Waasiraa

Leo kijiwe kina ajenda moja kuu, kumkaripia mhuni mmoja aliyetukana wenzake kuwa ni waroho wa juisi.
Dk Msomi Mkatatamaa leo amrauka na makabrasha yake. Kanji hayupo. Amekwenda India kupeleka fweza na kuangalia kama bi mkubwa wake ameishaongeza faida ya mtoto mwingine. Maana hawa jamaa kwa faida hata mtoto wa kubambikiziwa ni faida. Utamsikia akisema, “Mimi fika Bombei na kukuta bibi ongeza toto mbili.”
Msomi analianzisha? “Jamani mmemsikia mlevi wa madaraka Steve Waasiraa na nyodo zake za kizamani? Ama kweli nyani haoni nonihino lake!”
“Mbona yeye alipokimbilia Chakudema hakuambiwa kuwa alikuwa anafuata kunywa juisi au alipojirejesha Nambari Wani kwa aibu hakuna aliyesema alikuwa akihangaishwa na njaa? Huyu chinga Chikwawe ni wa kuonea huruma. Hana adabu wala maana kabisa. Hana jipya la kujadili zaidi ya kumpuuzia kama bosi wake alivyowapuuzia.” Anazoza Mijjinga.
Kapende hajimamasi, anamwaga pwenti, “Hakuna upuuzi uliniudhi kama kusema eti wapingaji wanakwenda ikulu kunywa juisi. Kwani hata wakinywa juisi huko ikulu hiyo juisi si ni matokeo ya kodi zao kama wanakaya? Mbona hata hapa kijiweni juisi zimejaa kama juisi ni dili? Mbona hata inzi wanakunywa juisi. Hebu angalia yale mainzi yalivyozunguka juisi pale.” Anaonyoosha kidole kuelekea kwa muuza juisi jirani na kijiwe. Anaendelea, “Hivi wangekwenda kule kunywa bia huyu jamaa si angejinyotoa roho?”
Mchunguliaji ambaye siku nyingi haudhurii kijiweni anaamua kutafuna mic, “Huenda Waasiraa aliaanisha mainzi yaliyomzunguka rais yakifaidi juisi kule ikulu na mawizarani. Who knows?”
Mzee Maneno anang’aka, “Kumbe ikulu siku hizi inaweza kudhalilishwa hivi tena na wale inaowafuga? Tunakwenda wapi?”
Mbwa Mwitu ambaye alikuwa kimya muda wote tofauti na kawaida yake aliamua kukwanyua mic, “Nyie hamumjui huyu mura. Aliwahi kuwarushia kimondo wapingaji kuwa ni malaya akakutikana kuwa kumbe yeye ndiye mwalimu wao. Jamaa ana ugonjwa wa kuongea bila kufikiri ukiachia mbali kulala lala mjengoni au mmemsahau yeye na Joni Kombaaa?”
Sofi hajivungi. Anaonyesha usongo wake, “Pamoja kuwa mimi ni mwanachama na mkereketwa nambari wani, kauli za hawa wenzangu zimenikera sana. Hata hivyo, msijali. Huyu Waaasiraa operesheni kimbunga itamkumbwa kwa vile ni mkimbizi haramu wa kisiasa. Sijui hata kama Chakudema watampokea. Maana hana sera tena zaidi ya mitusi ya nguoni.”
“Mwagie Sofi. Mmwagie kahawa, kumbe hata wenzao wameishawastukia siyo? Mshaurini huyo anayewafuga awapige chini tuwaone wakila majani kama ng’ombe wahuni hawa.” Anapayuka Mijjinga ambaye huwa haivi na bi Sofia.
Msomi, “Hebu niwakumbushe maneno ya nyodo na ukosefu wa busara ya Chikwawe.” Anafungua mkoba wake na kutoa gazeti liloandika habari za Chikwawe kumshangaa bosi wake na kusoma, “Nitamshangaa sana Rais Kikwete kama atashindwa kusaini muswada huo kwa sababu ya kelele za wapinzani.”
 
Anapekua mkoba na kutoa gazeti jingine na kusoma maneno ya kifedhuli ya Steve Waasiraa. Anasoma, “Hawa tumewalea siku nyingi na sasa wanafanya mazoea, ninachotaka kuwaeleza wasitarajie tena kuitwa Ikulu.” Anamalizia, “Kunywa juisi.”
Kabla ya kuendelea Mgosi Machungi anaingilia kati, “Kwani huyu waaasia ikulu ni mali ya mama yake. Tinapaswa kwenda huko kwenye ofisi timtoe kwanza haafu timuejeshe kwao Chakudema. Kwani hatumjui hata kama anawaponda Chakudema wenzake?  Bosi wao awapige chini wakamshangae vizuri. Hata hivyo, kwa alivyowapuuzia, wangekuwa na akili wangeachia ngazi wenyewe. Maana hata naye anawashangaa kwa wasivyotumia akili bali masaburi.”
Mpemba naye hangoji mwenzie amalize, “Huyu yakhe asumbuliwa na usingizi na madawa anayokula ati. Wategemea jitu lilalavyo hovyo hovyo liwe na kumbukumbu na hekima? Wallahi hawa si wazalendo hata kidogo.”
Mipawa, “Yeye mwenyewe Waaasiraa anafugwaga kiasi cha kujisahau na kuwaambia wenzake eti wanawafuga. Haya ni matusi ya nguoni yasiyopaswa kutoka kwenye kinywa cha mtu anayeitwa waziri. Kwanini tusimtokee na kumtolea uvivu kama anadhani hiyo ofisi ni yamama yake?”
Kapende anachomeka pwenti nyingine, “Nilisikia eti naye anajiandaa kugombea urais. Ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi. Yaani urais umekuwa rahisi kiasi hiki hadi kugombewa na watu ambao midomo yao ina mgogoro na vinywa vyao?”
Msomi akatua mic, “Tusipokuwa makini such sick, skinny and bankrupt dudes are going to wreck our ship. Loh! Samahani jamani. Nimechukia hadi naongea kikameruni,” Anajitetea na kuendelea. “Hata hivyo, siwalaumu wao bali yule aliyewafunga wasijue wote wanafungwa kwa kodi zetu.  Kuna haja ya kuwakumbusha hawa vimbelembele kuwa hata kama bosi wao aliwatuma wanapaswa kufahamu mahesabu ya mbayuwayu. Mara hii wamesahau kilichompata Nipe Mapape Ninaye aliyeambiwa awatukane mafisadi asijue lao moja. Si jamaa alimalizana nao na kumuacha Mapepe na aibu zake.”
“Kumbe hata wakameruni wanajua hawa jamaa walivyo na kuwaita madude kama sisi!” Anashangaa mzee Kidevu.
Kapende anakoleza, “Waache wajisahau wasijue kiama chao kinakaribia. Jamaa alishawaambia wajiandae kisaikolojia kila mtu kufa kivyake lakini inaonekana hawajaelewa somo. Shame on them!”
          “Msimlaumu Waasiraa. Tangu ajitoe chamani na kujiejesha kama mtalaka anapaswa apige kelele sana ili wenzake wamuamini. Huyu hana tofauti na yale mabuda kama Chibuda na Lyatongolwa Mlemavu ambao huchonga hadi mapofu yakawatoka ndiposa watupiwe mabaki wapwakie. Nawajua sana watu hawa mangungaembe wa kisiasa na wachumia tumbo.” Mgosi Machungi anakandia kwa sana.
Kusikia nungaembe Sofia anaamua kutia guu, “Sasa hapa unungaembe unatoka wapi mgosi?”
“Soe dada Sofi. Hapa tinamaanisha manungaembe wa kisiasa si wengine. Ngoja tibadili. Hawa ni mafisi na mafisadi wa kimawazo au vipi? Tabasamu sasa dada yangu.” Anajitetea Mgosi huku akimtania bi Sofi ambaye naye anatabasamu kuonyesha kuwa amemuelewa.
Kumaliza mgogoro Mgosi anasema, “Hebu kijana titilie kahawa mimi na Sofia tinywe na tifurahi,”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likatokea shangingi la Waasiraa tukaamua kulirushia mimawe huku yeye akionekana wazi kustuka na kutoa mimacho kana panya aliyenaswa mtegoni.  Kama si ndata kuingilia kati huenda tunge nyotoa mtu roho na kuacha wanaofuga upuuzi wakishangaa kama waasiraaa anavyowashangaa asijishangae.
Chanzo: Tanzania Daima Okt., 16, 2013.

No comments: