Saturday, 5 October 2013

Mlevi akutana na JK New York

 
Mwenzenu ninapoandika waraka huu niko New York, makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Jiji ambalo hujulikana kama apple.  Na ni apple kweli. Sikuja hapa kwa kudandia wala kubebwa na mzito yoyote wala kuunguza kodi ya walevi. Mie si mtu wa kubebwa wala kuteketeza kodi za walevi. Nina huruma na maono ya mbali. Pia sikuja na bi mkubwa kufanya matanuzi, kutoa tongotongo na shopping trips na mashoga zake. Wala sikuja na vitegemezi vyangu wala nyumba ndogo wala wadandizi kama wale. Uzuri ni kwamba familia yangu imeishatanua sana jijini New York kiasi cha watoto wangu kutolipenda kutokana na sekeseke na wakati mwingine misongamano hasa msimu wa vikao vya umaoja wa mataifa.
Ilikuwa nije na bi mkubwa. Ila baada ya kugundua kuwa alikuwa amepangiwa kuongea na baadhi ya taasisi za hapa, tuliamua kuchomoa hasa ikizingatiwa kuwa kimombo hakipandi. Nani anataka kusikia kiinglish chamimi ni Maimuna? Nani anataka kusikia Zetherefore badala ya therefore au tense zilizopinda kama mikono ya pweza? Nani atakuwa tayari kukaa na kusikiliza upuuzi wa mama aliyehitimu darasa la saba na kuungaunga? Hivyo, bi mkubwa aliamua kutokuja nami. Sikupenda nimpoteze mke wangu kipenzi kwa presha. Huwa akisoma hotuba za kiinglish presha humpanda na kulowa jasho kana kwamba anakuwa amefungiwa kwenye oven. Bado nampenda mtu wangu jamani. Hata hivyo ni kosa lake. Nilimshauri atumie muda wa ukuu wangu wa walevi kujiongezea elimu akagoma na kuendekeza kusaka ngawira kupitia NGO yake ya MAWAWA yaani Maujali ya Wanawake wa Wazito. Hayo tuyaache si muhimu hapa.
Mzee mzima nilifikia mitaa ya North Pearl ambako nilitia timu nikitoka mara kwa mara kwenda zangu Brooklyn na maeneo mengine ya Manhattan. nilitembelea Ground Zero, Madison Avenue,  Knox Street, Northern Boulevard,Henry Johnson Boulevard na mitaa mingine mingi ya New York.
 Nilialikwa na bwana Bank in Moon katibu mkubwa wa Umoja wa Mataifa  tuyelisoma wote pale Harvard University zama zile.  Nilimtangulia mwaka. Isitoshe, yeye ni mlevi mwenzangu ambaye husoma madudu yangu ambayo hutafsiriwa na wasaidizi wake.  Nilialikwa kushuhudia shoptalk za wanasiasa wakichezea kodi za walevi wao.  Nikiwa nafaidi vinono alivyoandaa Bank si akanistukiza kwa kunikutanisha na J K.
Tuliongea sana kwa vicheko na ari vya hali ya juu. Sikuamini kuwa ni yule niliyekuwa nikimdhania kuwa kichwa maji asiyependa kutoa majibu ya masuala mbali mbali muhimu.  Niligundua kuwa kumbe Jake ni mpoa tofauti na niliyekuwa namsikia magazetini na kumuona radioni. Kama atasikiliza ushauri wangu na wengine kuhusiana na katiba mpya basi ni mtu ambaye atawaumbua wale wasiomfahamu pale atakapokataa kusaini upuuzi uitwao katiba iliyochakachuliwa na mafisi na mafisadi waliowakilishwa na MPigs wao.  Katika maongezi yetu ambayo mengi ni top national security issues ni kwamba aliposema atawaumbua wengi, alishanusa harufu ya mafisi na mafisadi wanaodhamiria kulirejesha taifa kwenye zama za utwana na ukoloni mkongwe wa genge la watu kuwaburuza walio wengi.
 Baada ya kukaribishwa kwenye hotel tulipokutana kwenye mtaa maarufu wa 42nd Street nilitaka kujua anavyonichukulia kabla ya kumueleza nilivyokuwa nikimchukulia. Alikiri kuwa kweli huwa anasoma vitu vyangu na mimi ni mmoja wa watu anaowaheshimu na kuwagwaya na kuwamaindi sana hasa kutokana na uwazi na ukweli wangu. Aliniambia kuwa balozi wake kwenye Umoja wa Ulaji aliponiona alimtonya akisema, “Yule ndiye mlevi Nkwazi Mhango anayekupiga madogo mara nyingi.”
Mie sikuzungusha. Sikuwa na muda wa kufanya hivyo. Niliamua kulianzisha kwa kudai anipe mawazo na mipango yake kuhusiana na katiba mpya. Alicheka na kushusha pumzi akisema nimpe muda ili siku moja wale wanaomuona hafai wasutwe. Alinihakikishia kuwa tutapata katiba mpya na wale wambea na washenzi wanaodhani yeye ni hamnazo watashindwa na shetani atashindwa. Nilimshauri awafukuze wale wote walioteuliwa naye wanaotaka kumuingiza mkenge huku akiwakaripia wale wanaojitia kimbelembele kutetea upuuzi wasijue katiba ni zaidi ya chama na mtu. Nilimpa orodha ya watu anaopaswa kuogopa kama ukoma. Hawa ni Kimdunge Ngumbaru Mwehu, Mathias Chikwawe, Salvo Rwependekeza,  Nipe Mapepe Ninaye, Mwegulu Michemba, Pita Kisumu na wengine wengi wanaojikomba na kudhani yeye hana akili kiasi cha kumshauri mambo ya kijinga na kikale.  Nilimkumbusha msemo wa mzee Mchonga kuwa anayekudharau hukushauri mambo ya kipumbavu. Alinielewa.  Alisema atafanyia kazi ushauri wangu kutokana na uzito wa aliyeutoa na jinsi alivyogundua kuwa kumbe hata Bank ananizimia na kunitumia kama mshauri wake kisirisiri.
Nilimuuliza kwanini anawatetea wale wahuni wa Uhuruto kuhusiana na ICC. Alisema kuwa alisema hivyo kutafuta ujiko na kuogopa kuonekana anapingana na wamangi meza wa AU.
Pia nilimuuliza kuhusiana na habari za kuongezeka kwa mshiko wa wizi kule Uswizi. Alisema wazi kuwa naye anashangaa kuona wenzake wanamzunguka na kuiba njuluku za walevi. Aliniomba nimpe muda apate data ili tuweze kuongea vizuri next time tutakapokutana nitakapotua Bongo kumpa kampani kwenye uzinduzi wa katiba mpya.
 
 Tukiwa tunakata kilaji na Bank huku yeye maji, nilimuuliza kuhusiana na majina ya wauza bwimbwi akasema kuwa alipayuka tu hakuwa amepewa anasema ilikuwa ni vunga ya kisiasa ili kukubalika na kuwatia jamba jamba ili wanywee ingawa hawakufanya hivyo. Nilipomuuliza kuhusiana na waziri wake mmoja Bill Luku-vi kudani kuwa serikali isingetaja majina ya wauza unga kwa vile kulikuwa na ya waheshimiwa alisema kuwa lolote linawezekana na yoyote anaweza kuuza bwimbwi usawa huu. Nilipomuuliza aibu waliyotia wauza bwimbwi hivi karibuni, alisema haya magumu sana hivyo asingependa kuyachimbuachimbua yasije yakamchimbua.
Suala la katiba lilijirudia rudia kwenye mazungumzo yetu.  Niligundua kuwa kumbe jamaa anajua mambo mengi. Niligundua kuwa kumbe anawajua hata wale waliomzunguka wanaotaka kumtumia kwa ajili ya njaa na tamaa zao. Pia alionyesha kufahamu hata uzembe unaofanywa na baadhi ya taasisi ambazo ziko chini yake kama vile Takokuru, Uhasama wa Taifa na nyingine nyingi. Pia alionyesha wazi kuwa anajua fika mchecheto unaoikabili Nambari Wani kiasi cha kuhangaika ili isiteme ulaji. Nilimkumbusha ushauri wake wa kuwaambia waliozoea kubebwa kuwa wajiandae kisaikolojia. Alicheka sana na kusema kuwa ushauri wake bado uko pale pale na ambao watafanya makosa kutomuelewa atawashangaza sana siku si nyingi.
Pia nilimpa pongezi kwa niaba ya bi mkubwa Sally kupewa tuzo mbali mbali za kusaidia elimu. Alifurahi kujua nafahamu kuwa bi mkubwa huyu ambaye si msomi ameamua kutokwenda shule ili awasaidie wengine ingawa wapo wanaodhani kuwa kutafuta njuluku ndiko kunakomhangaisha asijue pesa si kitu cha kudumu kama elimu. Hayo ni yao.
  Chanzo: Nipashe Okt., 5, 2013.

No comments: