Saturday, 19 October 2013

Waraka wa Mlevi kwa Mwalimu Nyerere

Najua wengi watashangaa busara ya kuandika barua kwa marehemu. Heri kufanya hivyo kuliko kuwaandikia watu walio hai lakini wasiosikia. Hivyo, hata kama nasukumwa na mibangi na gongo kuandika waraka huu kwa gwiji Mchonga meno, ujumbe utamfikia yeye pamoja nanyi hasa walengwa.
Mwalimu, najua fika ulikuwa mlevi. Ulipenda sana kanywaji kaitwacho Philosophy Lager kalikokuwezesha kuwapayukia mafisadi na majambazi bila woga wala unafiki. Sisi walevi wenzako wa kanywaji haka tunakukumbuka kwa majonzi vilio na simanzi. Tunakukumbuka kwa mengi sana mwalimu.
Kwanza, tunakumbuka sera zako za ukombozi usawa na haki. Tunakumbuka elimu, matibabu na vinono vingine kwa umma. Elimu kwa sasa imebakia kuwa stahiki ya wenye nazo ambao huua shule zetu. Wanajali nini iwapo wana pesa na jeuri ya kupeleka watoto wao kusoma nje kwenye shule za maana? Wametujazia shule za kata ambazo nyingi zimekuwa viwanda vya kuzalisha wajinga badala ya wasomi.  Pia mwalimu, kumezuka mchezo wa kughushi na kununua shahada kiasi cha wasio nazo kutengwa kabisa. Wale watoto wa makapuku uliowapa elimu bure sasa ni matajiri wa kutupwa wenye jeuri ya kuweza hata kubaka elimu.  Zimeanzishwa shule za academia na international ambazo si academia wala international kitu bali vitega uchumi vya kueneza ujinga na kuajiri wageni. Nakumbuka mwaka jana wanafunzi wa kidato cha nne walifeli wote kiasi cha wizara kulazimika kupika matokeo kwa namna waliyojua. La kuchekesha japo linasikitisha ni majibu ya waziri mhusika alipoambiwa aachie ngazi. Alisema tena kwa nyodo kuwa hawezi kukjiuzulu kwa vile yeye siye aliyefanya mtihani na kufeli. Wewe ulisotea shahada zako Makerere na Edinburg.  Uliowaacha wanapwakia za kupewa ili waonekane wasomi hata kama siyo.
 Mwalimu, waweza kuamini kuwa wale uliowakomboa wamewauza watu wako uliokufa ukiwakumbuka na kuwalilia? Kinachoumiza si kuuza watu tu bali kuwauza na kaya yao. Maana, kwa hali ilivyo, kama hatatokea mkombozi, kuna siku watu wako watapaswa watafute pa kwenda wasipate.  Hata hivyo, nina wasi wasi kama watampata mkombozi kutokana na kuzuka jinai ya kutafuta na kupata uongozi kwa pesa huku wenye nazo wakirithisha madaraka watoto wao. Kwa sasa tuna wabunge, mawaziri, maafisa ubalozini, na kila sehemu yenye mshiko ambao ni watoto wa wakubwa. Hali ni mbaya. Ilifikia mahali ikafichuliwa kashfa ya watoto wa vigogo kuajiriwa benki kubwa huku makapuku wakiendelea kuhangaika toka ofisi hadi ofisi bila kupata hiyo kazi.
Mwalimu, usawa uliohubiri uliota mbawa zamani. Watu wetu si sawa kama ilivyokuwa mwanzo.
 Mwalimu, tunaomba utuombee. Tunaomba utuombee tuweze kujitambua na kutambua wajibu wetu kwa taifa letu lililoko msambweni likigugunwa na mapanya na mafisi kila aina kutoka kila sehemu.
Mwalimu, tunakulilia na kujililia hasa wakati huu ambapo matapeli na mafisi wamejivisha majoho eti ya kukuenzi wakati yanakusanifu. Sijui kama waliovuruga mema yako kama wana udhu wa kukumbuka. Wanajifanya wanakupenda wakati wanakuponda. Ni wanafiki wanaonuka unafiki wa kuchusha. Huwa tunawaona wakiandamana kwenda Mwitogo kunajisi kaburi lako. Tangu lini wazizi na wenye dhambi wakafagilia makaburi ya watakatifu kama siyo ghilba?
Mwalimu, amini usiamini yanatokea na yatazidi kutokea ambapo fisi waliojivisha majoho ya kondoo watasimama mimbarini kuimba utukufu wako.  Watakusanifu kwa kila lugha tamu wakati matendo yao ni machukizo makuu kwa watu wako.
Mwalimu, naomba unisikilize kwa makini. Je unaweza kuamini kuwa wale uliowaamini walikuangusha vibaya kwa kuwauza watu wako? Hakuna kilichotuudhi walevi kama yule kijana wako uliyemchonga. Najua unamkumbuka. Pia unakumbuka wakosoaji wako walipokuwa wanasema eti ulijibebesha kinyago cha mpapure. Sitamtaja kwa jina ingawa unamfahamu. Nakumbuka mwalimu. Ulitushauri hasa watumikiao umma kutosikiliza ushauri wa wake zetu. Ni ajabu kuwa wale uliowaamini nchi waliingia kwenye mtego uliomnasa Samson hadi wakatawala kwa sera za kitandani na nyingine za kuazima toka ughaibuni chini ya dhana ya Uchukuaji ulioitwa uwekezaji. Yale madini yote uliyotunza yalishakwapuliwa kiasi cha kuacha mashimo na watu hohe hahe wakilia na kusaga meno huku waliowauza wakiwasanifu na kuwaita wavivu wa kufikiri.
Mwalimu huwezi kuamini kuwa vibaka siku hizi wanaitwa waheshimiwa huku vigogo wa mihadarati wakiitwa wafanya biashara maarufu.  Tumefikia pabaya kiasi cha ule uwanja uliopewa jina lako kupitisha tani za mihadarati bila wasafirishaji kubainika. Ajabu kuna mashine kila aina lakini watu wanapitisha kago kama hawana akili nzuri. Ni hatari mwalimu. Kwa sasa watu wako wanasifika kuwa makontena ya kusafirishia madawa ya kulevya. Wanasifika kwa kuchuuzana na kuuzana tena kwa bei ya kichaa. Watu wamefikia mahali hata kuhongana masuti na upuuzi mwingine. Ajabu hao hao ndiyo wanaosimama bila aibu kusema eti wanakuenzi na kufuata nyayo zako wakati walishazifuta zamani. Najua mwalimu kuwa unamkumbuka yule mhuni aliyewaita wahuni wenzake kule Zenj na kulizika Azimio la Ukombozi la Arusha kwa kutubambika mkenge wa Azimio la Zenj lililosheheni siasa ya Uhujumaa na Kujimegea. Ujamaa na Kujitegemea uliwekwa msalabani Zenj na kuja na Uhujumaa na Kujimegea ambapo kila kinyama cha mwitu hutula kitakavyo bila ya kukaripiwa achia mbali kuchukuliwa hatua.
Mwalimu, huwezi kuamini kuwa tumefikia pabaya kiasi cha kuwa na watuhumiwa serikalini. Tuna mawaziri waliotuhumiwa kughushi shahada zao na bado hawajawajibishwa. Watoto wa mjini husema eti wanaendelea kupeta. Kwa sasa miiko na maadili ya uongozi vilishazikwa kiasi cha nafasi yake kuchukuliwa na madilI, kujuana na kulipa fadhila. Siku hizi hakuna anayeyaongelea na akifanya hivyo anachekwa na kuonekana mshamba wa kutupwa.
Kile chama chako ulichoanzisha na kukipenda kilishatekwa na wenye nazo. Nakumbuka. Kabla ya kuondoka kwako uliwahi kuwapayukia ukisema kuwa chama kimetekwa na wasasi wa ngawira kiasi cha kuwatelekeza wanyonge. Kwa sasa kinachoendelea ni mnyonge mnyongeni na haki yake ichukueni.
Siku hizi wenye madaraka wanashindana kwa magari na majumba ya bei mbaya bila kujali kuwa hawa maskini wa kusikinishwa kuna siku watalipuka. Maana wao ni bomu linalongoja kulipuka saa yoyote. Nani anajali iwapo kila mtu ameshikilia, “ni zamu yetu kula sasa”?  .  Narudia ili unielewe. Wao husema, “Ujanja kupata” bila kujali umepataje hata kama ni kwa kushikishwa ukuta.
Mwalimu naona niachie hapa. Kwani una mengi ya kufikiria na kujifunza.
Kila la heri na salamu nyingi toka kwa walevi.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Okt. 19, 2013.

No comments: