Saturday, 14 September 2013

Safu ya mlevi ni moja, wengine matapeli

 Walevi huwa tuna sifa na kanuni moja. Hatuna mila ya kuzunguka, kuzuga wala kumuogopa ngurumbili. Makala hii ni maalum kujibu uvivu wa kufikiri na ughushi nilioushuhudia kwenye chombo kimoja cha habari kinachochapishwa kila siku.
Kimebeba jina la safu hii. Hivi wameishiwa hivi kiasi cha kuiba hata jina la safu? Ushahidi, hilo `jizi’ linalojifanya kutumia jina la safu hii, linaficha hata jina lake. Shame on you! 
Natamani nimjue huyu kiumbe habithi na mchovu na mvivu wa kufikiri aliyeniibia akidhani atafika mbali.   
     Leo nina hasira sana  na isitoshe `nishautwika’ ili kutongoa haya ninayotongoa kwa utuo na msisitizo. Natamani nimkamate ngurumbili aliyeniudhi hata nimfanye asusa ya mbwa kama si fisi.
Fisadi wa kiakili na hana hata akili. Sikujua kuwa kumbe kuna walevi wa kuchongwa wanaofanya yasiyostahili bila aibu! Sikujua kuwa kuna watu wenye utasa wa mawazo na vichwa vinavyohara usaha.
Najua wasomaji wangu mnajiuliza: Mbona jamaa kaanza na gea ya hatari leo au mibangi imembangua kama si mibwimbwi kumbwimbwiza hadi akakosa uelekeo.
Chonde chonde watu wangu. Hakuna kitu kiliniudhi nusu ya kukaribia kupasuka kama kusoma safu yenye jina kama yangu kwenye gazeti la Mwakaya.  Baada ya kugundua hili, niliandika maoni ya kuonya utawala wa gazeti lakini hawakuyachapisha ingawa message was sent.
Yaani watu wamefirisika kiasi hiki au ni yale waingereza huita monkey see monkey do? Hivi inakuwaje baba au mama zima unafilisika upstair hadi unaiba safu ya mwenzio?
Kwa vile nimeishatambulisha mada ya leo ambayo itatuama kwenye walevi wachovu na wa kuchonga, naomba tuvumiliane. Nipe fursa niwashukie bila huruma kama vile mwewe ashukiavyo vifaranga.
Jamani, safu si sawa na majina mnayopewa kwenye dini zenu za mapokeo. Safu ni ubunifu, utukutu na ugwiji katika fani.
Siku zote mlevi ni adui na kiboko ya mafisadi kuanzia wale wa mjengoni waliochakachukua hoja ya katiba mpya, wale wa makanisani na misikitini wenye roho mtakakitu hadi wale wa kwenye kabineti walioghushi vyeti vya taaluma. Hawa ndiyo wabaya wangu wa asili. Kwa `kikameruni’ tunaitwa `sworn enemies’.
Hivi inakuwaje mhariri hata mmilki wa chombo cha umbea wa habari unakuwa na utasa na ukame wa mawazo, kiasi cha kuwalisha wasomaji wako pumba na upupu?
Kama mna shida ya majina ya safu si mseme tuwasaidie badala ya kuchonga safu ambazo nazo hazikidhi chochote kulingana na majina mnayoipa na kuyapachika kwenye safu hizi za mpapure?
Ukisikia ufisadi wa kiakili na kimaadili ndiyo huu. Hata kama kweli hakuna mwenye hati milki ya mawazo kwa watu wa mitaani, kwa wasomi kuiba wazo la mtu ni jambo baya sana si kwa aliyeibiwa tu bali hata kwa aliyeiba.
Maana ukiiba wazo unathitibisha wazi usivyo na ubongo unaofanya kazi. Unathibitisha unavyotumia masaburi badala ya kichwa. Je ni nani huyu anayejisifia kuiba kazi za wenzake?
Nikimjua ngurumbili huyu lazima nimfanyie kitu mbaya hata kama nikumshikisha, potelea mbali. Nina hasira.
Nimevuta mibangi yangu na kushushia na gongo ili nimshukie kiumbe huyu na wenzake waliompa uwanja wa kuonyesha ujinga na ujuha wake. Sina simile na tabia hii wala siombi msamaha kusema ninayosema.
Siku zote Hekaya za Mlevi zimejitenga na kujikomba, ubabaishaji na uganga njaa. Ndiyo maana akina Makidamakida na Job Nduguy kule mjengoni wakisoma vitu vyangu hukosa usingizi. Ndiyo maana mzee Pinder hungojea kujua ninachoandika kila jumamosi.
Kuonyesha hawa walevi feki mnaopaswa kuwaepa kama ukoma na ukimwi walivyoishiwa kulhali eti wamepanga safu yao ya kuchongwa itoke ijumaa, siku moja kabla ya safu yenyewe orijinali ili kuwazuga wasomaji.
You are dead wrong my enemies. Hamtampata mtu kwa vile wapenzi wa safu hii wanajua fika kuwa I am the one and only boozer who can squeeze anything out of anybody. Again, this is a too-often ignored token. Indeed, I am a man of my own.
Wasomaji wangu wanajua vitu vyangu. Wanajua vya kuchonga na original. Hii ndiyo maana msomaji wangu mmoja alinitwngia email kuuliza kama ni mimi naandika kwenye gazeti la mwanakaya.
Baada ya kushuku kuna mchezo mchafu, msomaji huyu aliamua kunitonya akishangaa kuona mapishi ya kule mbona yanapwaya. Nilimjibu kuwa jibu analo. Mie siandiki vitu vya kuigiza wala kuunga unga kama wasomi wa kughushi. Naandika vitu vinavyoingia akilini.
Kama kuna aliyewahi kubahatika kusoma vitabu vyangu vya ‘saa ya ukombozi’, ‘wanyama wetu’, ‘nyuma ya pazia’ au ‘kwetu ni wapi’  na machapisho yangu mengine atakubaliana nami kuwa sizungushi wala kumung’unya, kuigiza wala ku-copy vya watu na ku-paste kama walivyofanya hawa walevi uchwara wa kuchongwa. May you perish!
Hawa wanaoiba maandiko na majina ya safu za wenzao hawana tofauti nah yule nguruwe wa kwenye kitabu changu cha watoto cha Wanyama Wetu.
Sina haja ya kufumba na kufunga nyama. Walichofanya hawa jamaa ni kibaya sana kiasi cha kunipa kibali kumtoa mtu roho kama nitamnyaka. Na wana bahati. Kama si da Flo kunizuia nisifanye kitu mbaya ningeisha wa-al qaida hawa jamaa kama siyo kuwa-al shabaab mchana kweupe.
Hata hivyo, ni ukweli usiopingika. Mlevi original ni mmoja tu. Ni mimi mwenyewe na ninaishi kwenye nchi moja tu Kanada.
Anayependa au kuchukia hili afanye lakini huo ndiyo ukweli mweupe unaotelewa mchana kweupe. Ni bahati mbaya hawa wanaodandia madudu yangu hawajui kuwa nimeyabukua na kuyafundisha kwa muda mrefu. 

Chanzo: Nipashe Jumamosi Sept,. 14, 2013.

No comments: