Thursday, 12 December 2013

Mgimwa hana ubavu wa kuzungumzia EPA

  
Hivi karibuni waandishi wa habari walimbana waziri wa fedha Dk. William Mgimwa kueleza ni kiasi gani cha fedha kimesharejeshwa na majambazi wa EPA. Mgimwa alijikanyaga na kshindwa kutoa jibu sahihi na badala yake alikaririwa akisema, “Kwa sasa siwezi kuwaeleza ni kiasi gani kimerejeshwa hadi nipitie mafaili ndipo ninaweza kutoa jibu sahihi.”  Sitegemei kama kuna siku Mgimwa atawaita tena waandishi wa habari awape hizo taarifa anazodai kwenda kuzihakiki ofisini kwake.  Kwa mtu asiyetafuta kujaza tumbo lake, kwa nafasi yake asingekubali ufuska huu wa EPA. Ila kwa vile anayetafuta kujaza tumbo lake ni suala jingine.
Hata hivyo, waandishi wa habari licha ya kumchokonoa na kutaka kumuaibisha Mgimwa walimuonea. Nani aongelee EPA iwapi mtuhumiwa mkuu aliyedaiwa kutumia fedha ya wizi wa EPA kutafutia madarakani amekuwa akiogopa kugusia suala hili na kuliogopa kama ukoma? Mgimwa angekuwa mtu safi basi angegoma kupokea pesa hiyo na kushauri wahusika wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria. Kwa vile lao ni moja ameamua kunywea na kuwa msemaji wa uchafu huu.
Kwa matendo ya watu wanaoitwa wasomi tena wenye shahada za uzamivu kama Mgimwa kufanya vitu vya namna hii, ni ushahidi kuwa kumbe kusoma si kuelimika. Inashangaza ni kwanini mtu mwenye hadhi hii kisomi kukumbatia upuuzi usioweza kukumbatiwa na hata mbwa aliyendaye lindo bila malipo? Tunazidiwa na hata hayawani wanaujua ukweli kuliko sisi. Wanatuzidi hata mahesabu raisi kwa kujua kuwa mwizi si mtu wa kushirikiana naye. Siku moja rafiki yangu aliniacha hoi aliposema eti aliposema kwa kukata tamaa: Laiti mbwa angejua kusoma na kuandika akaaminiwa benki kuu yetu kuliko wasomi wa hovyo kama hawa wanaofanya mambo ambayo hata mnyama hawezi kutenda achia mbali mjinga.” Hii ilinikumbusha swali la : Nani anaweza kuamini kuwa mjinga aliyeitwa msomi tena Daktari kama Daudi Balali angeingizwa mkenge na wajinga wachache akaamua kusaliti kiapo cha kazi yake? Ajabu wajinga hawa hawa wanaendelea kuwahenyesha wale tunaodhani ni wasomi kumbe bure.
Sikujua kuwa bado ujambazi wa EPA unaendelea. Yaani nchi inayojisifia utawala wa sheria bado inaendelea kulala kitanda kimoja na mafisadi kwa kuwataka warejeshe chumo la wizi badala ya kuwafunga? Je ni kweli pesa hiyo inarejeshwa au ni danganya toto? Je ni kwanini wezi hawa wanaorejesha fedha hawawekwi wazi ili umma uwajue hata kama serikali imeamua kulala nao kitanda kimoja? Je serikali inayowaficha kwa sababu inazojua inaweza kuwanyang’anya tonge mdomoni au ni kuendelea kutufanya hamnazo?
Je hawa ni akina nani wenye uwezo wa kuilazimisha serikali kufanya wanavyotaka hata kwa kupinda sheria? Je hawa si washirika wa serikali? Serikali inayoficha majina ya wezi wa fedha za umma inaweza kufichua majina ya wauza unga kweli?
Je Mgimwa anaridhishwa na kitendo hiki cha jinai cha wezi kurejesha fedha? Je kufanya hivyo hakumfanyi Mgimwa kuwa mwizi kama wezi anaowakubalia kurejesha chumo la wizi? Maana sheria iko wazi kuwa asirikianaye na mhalifu naye ni mhalifu na adhabu yao ni ile ile iwe ametenda au kushiriki kwa namna yoyote. Je hawa si mibaka tunaoalalamikia ambao wana uwezo wa kuiba na kulazimisha serikali iwalinde? Je namna hii nchi iko salama mikononi mwa majambazi kama hawa? Ukimuuliza mwanasheria mkuu wa serikali na hata mwendesha mkuu wa mashtaka wa serikali na TAKUKURU juu ya ujambazi huu utagundua jinsi huu ulivyo mchezo wa kuigiza. Wanatupotezea muda kupambana na vidagaa wakati wakifua nepi za majambazi wa kubwa. Kwangu wote naona ni wezi tu hata kama wana madaraka.
Tukisema serikali ya Kikwete ni ya ubia kati yake na mafisadi hata majambazi tunaambiwa tunamchukia. Nani anaweza kueleza mantiki ya Kikwete kutoa ‘amri’ kwa wezi tena wa mabilioni ya umma warejeshe chumo la wizi? Mbona hawaambii wezi wa kuku kurejesha kuku? Je tangu lini Kikwete akawa hakimu au jaji kama si ufisadi wa kunuka? Nani hajui kuwa kwa mfano Kagoda iliishia mlangoni mwa mshirika na swahiba mkuu wa Kikwete aitwaye Rostam Aziz na hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi yake? Nani hajui kuwa hata Richmond ni Rostam Aziz huyu huyu na hakuna anayethubutu kumgusa? Wapo wanaodhani kuwa kuna ufisadi mwingine unaoishia kwa mtu huyu huyu haujawekwa wazi. Wapo wanaodhani kuwaRostam si bosi wa Kikwete. Wapo wanaotamani Kikwete ajitete ili kutua zigo hili ambalo limemng’ang’ania shingoni miaka yote ya utawala wake. Je Kikwete anaogopa nini kujitetea kama hakuna namna? Je kuna siri ambazo Kikwete asingetaka ziwekwe hadharani. Wapo wanaoona kama habari za EPA ni kaa la moto hata kurugenzi yake ya propaganda za kichovu haiwezi kuligusa bila kumuunguza bosi wao. Natamani waandishi wa habari wazidi kumchimba Mgimwa ili tuone kama atakuwa na jipya kuhusiana na kashfa ya EPA.
Chanzo: Dira Desemba, 2013.

No comments: