Friday, 20 December 2013

Mlevi alaani walevi kujichukulia sheria mikononi


Kwanza nawasalimu na ‘kuwakaripia’ walevi wa kule Ng’wanza kwa kuchukua sheria mkononi japo ni haki yao kutoa onyo kuwa mafisi, mafisadi na kila vinyama vya mwitu kuwa wajiandae kupata saizi na stahiki yao yaani kuwaishwa kwa aliyewatengeneza wakampuuzia, si vizuri kudedisha watu.
Nilishasema mara si nyingi kuwa kubebabeba mibunduki kwenye kaya inayoitwa ‘kisiwa cha amani’ ya imani ni uwendawazimu na kujitafutia balaa.
Sasa tazama hata wino haujakauka mmoja wa wabeba silaha na wajivuni ananyotolewa roho! Kisa? Alidhani kumiliki silaha na kuwa kiongozi ni kuwatisha walevi na kuwaibia hata kuwazuia kupita wanakopaswa.
Heri kulewa kanywaji kuliko dhuluma na madaraka. Sasa mnaona?
Kwa vile nilishatangaza nia ya kugombea urais, natoa angalizo na onyo. Siku nikichaguliwa, wale wote wenye tabia ya kutumia vyeo vyao kupora na kukatisha maisha ya walevi wakae mkao wa kuliwa. Nitawatia sana adabu na kuhakikisha wanashika adabu kabla ya adabu haijawashika.
Hatuwezi kuishi kwenye kaya ya shamba la chizi ambapo majizi fulani yanayojiita wazito yanawatesa walevi wale wale walioyapa ulaji. Hatuwezi kuendelea na hii tabia ya mijizi kula kwa mikono na miguu tena bila kunawa kama mainzi mafu.
Pia hatuwezi kuendelea na kujichukulia sheria mikononi. Naapa kwa jina la bibi wa bibi wa babu nitaondoka na mtu katika sakata hili.
Leo naleta salamu za walevi ambao juzi walikata kanywaji kama hawana akili nzuri tokana na kupata habari kuwa kondoo wameweza kumuua fisi aliyetaka kuwararua asijue wamejijua na kujitambua na kuutumia umoja wao kama nguvu yao. Sitavumilia jinai hii. Wale jamaa zangu wa Chama Cha Maulaji (CCM) waliozea vya kunyonga, sasa wajiandalie vya kuchinjwa.
Nadhani wanachopaswa kufanya ni kuacha mchezo wao mchafu wa kudhani kuwa kila mlevi hana akili wala ushupavu wa kuweza kujipigania yeye na mali yake.
Najua jamaa zangu wameishiwa na udhu kiasi cha kubaki na uchu tu wa kuiba kila waonacho.
Hivi tunayo majizi mangapi yanayojiita viongozi yaliyoiba mali za walevi na bado yakaendelea kujiona majanja wakati ni majambazi tu?
Nadhani wale majizi wakubwa waliogawana nyumba za walevi na kuingiza kaya kwenye ubinafsishaji wa kifisi, wananipata hata wakijifanya hawanipati.
Tunawajua. Wamejiuzia mashangingi ya walevi kwa bei ya kutupa toka kwenye wizara zetu. Tunawajua waliopeana UDA yetu na mashirika mengine aliyoasisi mzee Mchonga (MAMPP). Hata kama Mchonga ametoweka, walevi hawajatoweka. Idd Lion na Simon Gang mnanideku siyo? Akina Kagodamn, Richmonduli, IPtL, EpA, NbC, Meremetuka na wengine kaeni mkao wa kuliwa na kunyotolewa roho zenu mchana kweupe. Tutawashikisha ukuta, sorry, adabu muda si mrefu. Mijitu imeiba ofisi za walevi kiasi cha kuzirithisha vitegemezi vyao. Joseph Makamba unanipata mshirika?
Sasa mnatuibia hata ardhi ukiachia mbali njuluku yanazoficha ughaibuni! Sasa kwa vile mimi ni kamanda wa walevi, natoa amri kuwa atakayepora mali yenu chomeni moto kama kibaka.
Pia nitoe onyo kwa ndata wanaopenda kulinda na kukingia kifua mafisi wanaopora mali za walevi, mtachomwa hasa ikizingatiwa kuwa walevi sasa hawana woga wala subira tena.
Acheni ujuha wa kutumika kama nepi kusafisha uchafu wa mafisi. Mijitu ina tamaa utadhani haitakufa.
Walevi wakiamua hata ushike bastola wanaweza kukunyotoa roho bure hata kama si jibu. Kwanini ufe kama kibaka kwa kila aina ya aibu majonzi na vilio?
Huwezi kuwa mjanja siku zote especially unapodili na walevi ambao waliishakufa wakibakia kuzikwa. Watakunyotoa roho ufe wakati si wako.
Najua wapo wajinga watakaoniona mlevi wa ajabu kuwa na huruma hata kwenye misiba ya wengine.
Kwanini nifurahi hata kama misiba yenyewe ni ya kujitakia? Japo nilipiga kanywaji na bangi kwa sana ninaposikia kuwa ‘mpendwa’ wangu amenyotolewa roho ni kwa huzuni tu. Mie sina unafiki na sanaa kama za Chama Cha Majangili ambacho juzi juzi eti kilikuwa kinakionea huruma Chakudema kwa kuwa na kidudu mtu aliyetaka ulaji hata kwa kuwala wenzake? Japo adui yako muombee mauti ili akuondolee mbu, kwangu si hivyo. Kama kiongozi wa walevi, huwa ninajali linapokuja suala la ukombozi wa walevi.
Ukiwachokoza wakakutoa roho sitasherehekea kwa vile umejitakia mwenyewe, ninawaonya wote.
Wapo wanaouliza, hivi hawa wanaojifanya kuwa na huruma na kansa kama hii wana akili kweli? Leo kaya yetu imepoteza wanyama tena kwa kusafirishwa hai mchana kweupe. Tukiwakamata hawa majangili tukawanyotoa roho zao tuambiwe tumevunja sheria! Sheria gani inayolinda uoza na ufisi?
Mmeigeuza kaya yetu shamba la chizi na pango la majambazi tukiwa tunaona.
Hakuna kitu kilimuudhi mlevi nusu ya kujitia kitanzi kama kuona baadhi ya mafisi makubwa makubwa yakitoa eti salamu za rambirambi badala ya karipio na kujirekebisha kwa mafisi yanayouawa kutokana na kuwadhulumu walevi.
Mnavuruga kaya na kuifanya kama dunia ya samaki mkubwa kumla mdogo na mdogo kumla mdogo zaidi halafu ukweli ukifichuka mnajifanya mna huruma.
Huruma gani ndani ya dhuluma? Walizoea kujisemea kuwa mali ya umma haiumi. Sasa inauma sana na kuua. Leo salamu ni kwa mashujaa wote wa Kanyamaa waliokataa kunyamaa wakalaani mauaji. Mwabeja sana. Ila siungi mkono kunyotoa uhai. Kuna njia mbadala jamani. 

Chanzo: Nipashe Jumamosi Desemba 21, 2013.

No comments: