Wednesday, 12 February 2014

Vita ya CCM neema kwa watanzania

HAKUNA ubishi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeingiliwa au tuseme kuvamiwa na kansa mbaya.
Hakuna kitu kinakitafuna chama hiki kama mdudu wa kupenda madaraka huku wanaoyatafuta wakiwatumia makada wa chama sehemu mbalimbali kuwapigia kampeni jambo linalosababisha migongano na hata malumbano yanayokiua chama taratibu.
Hali ni mbaya sana. Watu wamefikia kuvuana nguo hadharani kuhakikisha yule “wanayemtaka”, huku naye akiwataka na kuwatumia nao wakimtumikia anapita hata kama ni kwa watu wazima kufanya mambo ya kitoto kama kuvuana nguo hadharani.
Ni bahati mbaya kuwa CCM imeishiwa na kufilisika kiasi cha kutokuwa na kiongozi mwenye uthutubu wa kukaripia mitandao hii inayodhoofisha na kuua chama.
Asikudanganye mtu. Wote sasa ni sawa na kambale. Wana sharubu, tena ndefu sana. Mitandao ya kifisadi, kiulaji na kimaslahi imechukua nafasi ya chama kiasi cha kukiangamiza taratibu kama kansa inavyoonekana na kila mtu ana mtu wake na maslahi yake.
Hata Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete naye yumo kiasi cha kuhojiwa. Naye ana mtu wake anayeweza kulinda maslahi yake. Haya si maneno yangu. Rejea karipio la Malecela aliyekaririwa hivi karibuni akisema: “Kinachonishangaza ni ukimya wa viongozi wa juu wa chama, akiwemo Mwenyekiti wa chama wa taifa, Rais Kikwete. Naitaka Sekretarieti ya CCM kutafakari, kumjadili kwa kina na kumwajibisha Lowassa, ikiwezekana atimuliwe uanachama.”
Mtifuano wa Malecela na Mgeja unanikumbusha kisa cha ugomvi wa washirikina waliokuwa wakigombea kila mtu na kinyago chake ndicho kiabudiwe hadi wakataka kutoana roho ilhali vinyago vikiwa salama.
Mwisho wa yote, walipogundua kuwa vinyago vyao havina lolote wala maana, waliamua kuvichoma moto na kumtafuta Mungu wa kweli. Je, Malecela na Mgeja watafikia hatua ya kuachana na mitandao na maslahi binafsi na kukirejea chama?
Hata hivyo, mchezo huu unaoelekea kusababisha mauti ya CCM ni ukombozi kwa Watanzania kama wataweka kumbukumbu. Pia mchezo huu ni faida kwa wapinzani kama wataamua kuvalia njuga haya madudu yanayofichuliwa na makada wa CCM wenyewe. Hakika mitandao imetandawaza kila aina ya sababu ya kuanza kuiaga CCM taratibu.
Leo hii ni zamu ya makada, Hamis Mgeja, Mwenyekiti wa CCM wa Shinyanga na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu na Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela. Baada ya Malecela kuita waandishi wa habari hivi karibuni na kukaripia tabia ya baadhi ya wana-CCM kuanza kutangaza kugombea urais hata kabla ya muda, amejichongea.
Malecela katika mkutano wake na waandishi wa habari alimtaja Edward Lowassa, mbunge wa Monduli na waziri mkuu aliyetimuliwa kutokana na kashfa ya Richmond wazi wazi kuwa hafai kuwa rais.
Siku mbili baadaye, Mgeja aliamua kumtolea uvivu Malecela jambo ambalo limetufanya kuuliza kulikoni Mgeja kumsemea Lowassa kana kwamba yeye ndiye wakili wake? Je, ametumwa au amejituma? Je, ana nini cha mno na Lowassa au ndiyo huku kutumiwa na kutumiana?
Mgeja alikaririwa akisema: “Huyu Malecela amesahau huko nyuma yeye alishawahi kutuhumiwa kuwa alipewa fedha kutoka nchi za Uarabuni na mpaka kubadilisha dini na kuitwa Jumanne ili aungwe mkono kupewa nguvu za kugombea urais.”
Laillah ila allah! Hatukuyajua haya na kama ni ya kweli basi kuna namna. Je, inakuwaje kwa Mgeja Muislamu aone kitendo cha Malecela kusilimu kama kitu kibaya kama hakuna namna? Pia Mgeja alisema kuwa Malecela alikataliwa na baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere hadi kumtungia kitabu.
Ajabu Mgeja huyo huyo sijui kwa kusahau kwa kutojua kuwa alitumia mfano mbovu, alisahau kueleza kuwa hata huyo Lowassa alikatiliwa na Nyerere huyo huyo.
CCM imeoza kwa rushwa jambo ambalo kumbe wananchi hawakujua. Kwani Mgeja aliongeza: “Malecela, Makonda na washirika wenzao wanajua kuwa wako baadhi ya wanachama wanagawa kalenda nchi nzima, wanagawa simu huku wakitumia magari ya serikali kugawa hizo takrima na inawezekana na wao pia walishawahi kuzipokea na wana-CCM wengi walishazipokea, hata mimi nilishapokea, mbona hizo hawasemi, nazo zinakivuruga chama?”
Je, hapa kinachogomba baina ya Mgeja na Malecela ni uchungu kwa chama au uchungu kwa mitandao? Je, Malecela ni kama Yusuf Makamba aliyeonyesha wazi wazi anamtetea na kumuunga mkono Lowassa? Wapo wanaosema kuwa anatumiwa.
Ni aibu kiasi gani kwa makada wa chama kuanza kuhongana na kutumiana kama nepi? Je, chama cha namna hii chenye uoza kuanzia kichwani hadi miguuni bado kina udhu na hadhi ya kuongoza taifa linalohitaji mkombozi toka kwenye rushwa ufisadi na majanga mengine ambayo CCM imeyasimamia na kuyatekeleza siku zote? Je, wananchi wanajifunza nini kutokana na vita hii ya mitandao maslahi?
Rushwa kwa sasa inatembezwa wazi wazi na waasisi madaraka wa ndani ya CCM. Watu wanauliza haya mabilioni yanayomwagwa yananunua nini na wahusika waliyapata wapi? CCM inanuka rushwa kiasi cha kutisha.
Rejea karipio la Malecela aliyekaririwa akisema: “Naomba niseme kuwa bila karipio au tamko la chama, hawa wanaotumia fedha hadharani kwa lengo la kutafuta umaarufu na ushawishi kwa vijana ili kupata madaraka, wataharibu misingi bora ya uongozi iliyowekwa na waasisi wetu ndani ya chama.” Kwa rushwa kama hii ya wazi wazi kumebaki kitu cha kuweza kuweka madarakani?
Watanzania wakifanya kosa wakarudia makosa kwa kuchagua chama fisadi na kinachoongoza katika rushwa wasijute wala kumlaumu mtu. Hawa watu wapo kwa maslahi yao fichi na si ya Watanzania. Laiti Watanzania wangewabana hawa watoa rushwa wakaeleza walikopata hizo pesa na wanataka kununua nini!
Tumalizie kwa nukuu ya Paul Makonda, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi, aliyekaririwa akisema: “Lowassa amekuwa akiwatumia watu kusema ovyo, kwanza mwenyewe hana sifa ya kuwa rais wala kuwa amiri jeshi mkuu wa nchi, na kama wapo vijana hapa mjini wanaotaka fedha kwa haraka wamtafute.”
Kwa halli hii, Watanzania waliokuwa wemelewa mapenzi na imani kwa CCM wamejikuta mbele ya kinyago cha mpapure walichodhania ni Mungu. Kazi kwao. Wazee wazima wanafanya kile Waingereza huita, washing your linens in the agora.
Ukifikia hapo umeisha na kuishiwa. Watanzania wanapaswa kuifungisha virago CCM ili wenye uwezo waingie na kutawala. Hakuna tena sababu ya kuendelea kuiamini CCM isiyojiamini wala kuaminika.
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 2014.

10 comments:

Anonymous said...

Tatizo Watanzania hawapendi mabadiliko
Wamezoea mazoea na yatawapeleka kuzimu kwa uvivu wa kuchagua,Leo mpe mzungu ungali ale kesho ataupika ugali kwa ladha nyingine
Lakini Tanzania ugali ule ule unga na maji moto imetoka mboga tu inabadilishwa , amkeni wabongo

Anonymous said...

Walivyokuwa wapumbavu na wajinga kabla ya mkuu kuondoka kwenda kwenye kong amino UK
Anazinduwa kampeni kupinga ndovu kuuuwa, aliitajiwa kigogo mkuu wa biashara hiyo Yuko CCM Long time ago

NN Mhango said...

Anon wa kwanza nimejinza toka kwako kuwa watu wanapaswa wabadilike wenyewe na kuthuthubut badala ya kusishikilia mazoea. Jana kwenye uzi fulani Jaribu alibainisha kuwa waswahili hatupendi kujifunza hata ipite miaka 1000. Japo sikubaliani naye mia kwa mia ana hoja.
Anon wa pili umenigusa hasa pale unaposema anazindua kampeni wakati wahusika wanaweza kuwa watu wake anaowajua fika lakini asichukue hatua. Uenikumbusha kelele na ulimpyoto wake juu ya kupambana na ujambazi, ufisadi (ugamba) mihadarati na mabalaa mengine. Badala ya kupambana navyo alivipamba na kuwaongopea wananchi kuwa ana orodha ya wahusika. Kwanini hakuwakamata na kuwachukulia hatua? Nani akatae mkono unaomlisha? Nani awakamate wafadhili wa CCM ambap wengi wao ni waovu wa kawaida kama akina Madabida Rostam na majambazi wengine wengi?

Jaribu said...

Kama huyo Anonymous alivyosema Mhango, mimi huwa nasema hivyo kwa uchungu, siyo ni kama napenda kufikiri hivyo, lakini huwa naona uchungu hasa kwa wageni wakisema kuwa maisha hayajabadilika sana nchi za kiafrika hasa vijijini. Hamna tofauti maisha ya kijijini ya sasa na yale ya enzi za jiwe.

Sasa kama hawa jamaa wa CCM, toka enzi za Mkapa huu wizi na ujambazi umekuwepo, lakini watu bado wanawang'ang'ania tu. Mimi hata kuna jamaa yangu fulani amebadilika anawatapeli watu hata akienda nyumbani. Ukiwaambia Waswahili kuwa jamaa huyo atakuliza watabisha mpaka watoke povu, "Huyu jamaa ni mkubwa namheshimu sana!" Mpaka wakitapeliwa ndio wanarudi tena, "Ungejua tungekusikiliza."

Kitu nilichogundua ughaibuni ni kuwa jamaa hawaoni aibu kujiokoa. Ikitokea disaster watu wanatoka mbio hata wakiwa uchi, ambapo Mswahili atakuambia kuwa anaona aibu kutoka uchi na Waswahili kwa kweli watajali sana mtu alitoka uchi kuliko kuwa mtu amejisalimisha maisha yake. Mara ya mwisho nilipokuwa Dar nilikuwa mwoga wa madereva machizi mpaka jamaa wakawa wananicheka kuwa ni "mshamba." Lakini jamaa hao hao kila siku ni stori za watu waliogongwa na magari, huwezi ukapigana na tani ya chuma.

Na hizi dini za kuletewa ndio zimezidi kutupumbaza, jamaa wanaona wanyonge ndio wataokwenda peponi. Ndio maana wenyewe wa magamba kila siku wanang'ang'ania viongozi wa dini wawaambie waumini wao hivi au vile. Watu inabidi tuboreshe maisha yetu hapa hapa duniani hasa Tanzania na siyo ahera.

Jaribu said...

.....wanarudi tena, "Ungejua tungekusikiliza."

Hapo nilikuwa namaanisha, "Tungejua tungekusikiliza."

NN Mhango said...

Jaribu umemaliza yote. Imekuwa kama umeona woga wangu. Huwa najiuliza. Hawa vitegemezi wangu waliozaliwa hauku siku wakikua wakaenda Bongo itakuwaje? Maana wao wamelelewa kwenye mazingira ambapo wajibu, haki na kuaminiana ni vitu vya kawaida. Hawajui rushwa woga utapeli wala kujigonga. Kuna kipindi napanga kuacha kila kitu niwapeleke kule lau kwa mwaka wa mwisho atakapotimiza lau miaka tisa ili wajionee na kujifunza.
Kusema ukweli watu wetu ni wa kuonea huruma. Ajabu wanatusema sisi tuliko huku kuwa tulikimbia maisha magumu na sasa yamebadilika ila hawaachi hata serikali zao kusema wanataka tuwekeze kule ili nao wahomole.
Watu wetu wamejisalimisha kwa mtekaji kiasi cha karibu kila mtu kugeuka tapeli na mwenye chuki ya maendeleo,
We acha tu.

Anonymous said...

Na wazungu si wajinga wanaijuwabongo kupita wabongo
Hata hiyo hotuba ya mkuu kashauriwa na waua Tembo

Anonymous said...

Haingii akilini denge inakuja bongo at international airport inachukuwa wanyama hai
Umewasikia eti kuna jengo karibu ya ikulu
Ghorofa 16 eti livunjwe kwa usalama wa ikulu
Jamani ghorofa 16 zinajengwa karibu ya ikulu
Si mkuu hata maafisa wausalama waliona tangu msingi wa jengo
By way makao makuu si Dodoma mbona hamhami
How much it's to have captical cityes in Tanzania
It's strange it's the only country in the world who have two captical city's. Poleni wabongo walalahoi mtalipa kodi hadi kuzimu

Anonymous said...

Na Kila mwaka ukarabati wa ikulu mabilions
Angalia ukumbi wa bunge Kenya simple lakini jengo la bunge Tanzania haliendani na halisi ya Tanzania matanuzi wakati nchi ni maskini wa kutupwa duniani
Ukitaka kuwajua wabongo tena wanasiasa wa juu nenda blog ya mashughuligob utashangaa
Ndo unga na Tembo rukhusa bongo

NN Mhango said...

Anon hapo juu mmeonyesha usongo wenu kwa taifa lenu. Sina cha kuongeza zaidi ya kujifunza kuwa mambo yanayofanywa na watawala wetu yanatia kichefuchefu kuliko hata kinyesi ashakum si matusi.