Wednesday, 12 February 2014

Kijiwe chafaidi mipasho ya CcM

    John MalecelaBAADA ya kulishughulikia li-Rweyependekezamu, tulisikia eti lililalamika na kulaani sana likitishia eti kumuona Mkamiawaandishi wahujumu gazeti. Hilo limeishiwa tu. Baada ya Chama cha Mipasho (CcM) kuamua kutoa burudani ya bure, kijiwe kimeamua kukaa na kutafakari na kufanyia uchambuzi hatua hii ya kupigiwa mfano na kushangiliwa, hasa na wale waliokuwa wakitatizwa na kitu hii.
Yote haya yalianzishwa na Mpemba ambaye inaonekana ni mfuatiliaji mzuri na mpenzi wa mipasho ya walevi hawa wa madaraka.
Anaingia akiwa na gazeti la Danganyika Leo. Anaamkua na kuagiza kahawa huku akiwa anatembeza uso wake kuzunguka kijiwe kizima kuona watu wanajisikiaje.
Anasema: “Mwafahamu kuwa kuna kijana aitwaye Maakondaa kwenye chama cha mafisadi aliyekonda kuona wazee wote wa chama yake wanatumiwa kiasi cha kutoamini kama hiki ni kitu cha kufumbia macho? Hivo, bwana ndogo aliamua kupayuka kiasi cha kuwakwaza wakongwe. Nanhusudu huyu kijana walllahi.”
Mbwa Mwitu anaamua kumtania Mpemba akisema: “Shehe unhusudu huyu dogo ili umfanzeni?”
Mpemba hajali. Badala ya kumjibu Mbwa Mwitu anamgeukia Mchunguliaji aliyekuwa akimezea gazeti na kusema: “Najua wapenda sana habari na magazeti weye. Basi tukua utusomee ili hata hawa wanolote utani kwenye mambo yaso ya utani wafahamu kinioendelea.” Anampa gazeti huku akimuonyesha pa kusoma.
Mchunguliaji naye anachukua gazeti na kuanza kusema: “Hebu sikia dogo alivyozoza. Haya si maneno yangu.”
Anasoma gazeti linalosema: “Lowa-sir sasa amekuwa akiwatumia watu kusema ovyo, kwanza mwenyewe hana sifa ya kuwa rais wala kuwa amiri jeshi mkuu wa nchi, na kama wapo vijana hapa mjini wanaotaka fedha kwa haraka wamtafute.”
Mijjinga anaonyesha mshangao. “Kumbe fisadi huyu ni kitega uchumi cha wachumia tumbo siyo!”
Kapende anajibu: “Ulikuwa hujui? Hukusikia Maakondaa akisema kuwa kama unataka ulaji wa dezo nenda kwa Lowa-Sir?  Hukumsikia mgosi akiapa kufanya lolote kuhakikisha anamtetea na kumlinda fisadi huyu Ewassa? Sijui amemfanya nini yarabi hadi anapagawa hivyo baba zima!”
Mgosi Machungi anakwanyua mic haraka na kujihami. “Niombe msamaha haaka kabla sijapiga mtu zongo. Siwezi kujizaiisha kwa vijipesha kidogo isitoshe kwa mtu anayetumiwa na hao waiomnunua kuja kuwanunua Wadanganyika wenye uchu. Jamani tiwe makini tinapoongeea haya mambo. Mimi si wa kujiuza kwa Owassa.”
Kapende hakawii. Anamnyang’anya mic Mgosi na kudema: “Mgosi nawe una papara. Kwani mgosi ni wewe pekee duniani? Namaanisha mgosi Joseph Makambaa si Machungi.”
“Hapo time understand. Maana tiishangaa kuona tinahusishwa na fisadi wakati sisi tinapambana na ufisi na ufisadi,” anajibu Mgosi Machungi huku akitabasamu kuonyesha kuridhika na majibu ya Kapende.
Mpemba anaingilia: “Nyie mwashangaa haya! Sie tushazoea hasa wakati wa yule kamandoo uchwara Salimuni Amri ambaye sasa ashasalimu amri. Walitokea hata magabacholi wakamramba viatu hadi wakawa matajiri. Alipotimka sasa mwawasikia hawana ladha tena. Wahaha kama mbwa koko.”
Kanji kaudhika kusikia neno gabacholi. Anakatua mic: “Choli iko mizi hapana ita dugu yako choli bwana. Sisi sote dugu.”
Kapende anachukua gazeti toka kwa Mchunguliaji na kunukuu maneno ya Malisera akisema: “Kinachonishangaza ni ukimya wa viongozi wa juu wa chama, akiwemo Mwenyekiti wa chama wa kaya, Rahisi Kikwe… Naitaka sekretarieti ya chama kutafakari, kumjadili kwa kina na kumwajibisha Ewassa, ikiwezekana atimuliwe uanachama.”
Msomi anakwanyua mic na kuzoza: “Anashagaa nini iwapo lao moja? Hakuna aliyeniacha hoi kama yule habithi toka usukumani aitwaye Mjega ambaye alisema kuwa agwe alikataliwa na Mchonga asijue hata huyo bwani wake Lowa-Sir alikataliwa pale aliposhindwa kueleza alivyopata huo ukwasi ambao sasa anawahongea hata wanaume wazima wakajidhalilisha.”
Mipawa anakwanyua mic: “Usinikumbushage Mchonga alipowakataa Ewassa na Kikwekwe wake kiasi cha kuokoa kaya asijue watarudi na kuizamishaga.”
Mijjinga aliyekuwa anabofya ki-ipad chake anadandia mic na kuzoza: “Huyu Mjega namfahamu sana. Ni mtu mzima hovyo ambaye anajigejuza a barking dog that does not bite.”
Msomi anampa tafu kwa kuzoza ukameruni kwa kusema: “They guy is but a lapdog that can’t become a watchdog.  Muhimu ni kwa wapinzani kutumia mwanya huu. Maana underdog can become top dog. Au vipi?”
“Waheshimiwa mlivyoamua kutuadhibu kwa ukameruni wenu sina hamu. Mmekuwa kama jamaa zetu waishiwa wa mjengoni wanaopenda kuchanganya Kiswahili na kikameruni!” Analalamika mzee Maneno.
“Samahani mzee mwenzangu. Nilichotaka kuonyesha ni uhovyo wa huyu Mjinga sijui Mjega sijui nini. Ukisikia kutumia, kutumiwa na kutumiana ndiyo huku. Hamkumsikia mgosi Makambale akiapa kwa miungu yote kuwa atakufa na Ewassa as long as naye anamkatia ili afaidi?”
Mbwa Mwitu anachomekea: “Urahisi si mchezo ndugu zanguni. Mtu anakula kuvaa na kutanua bure ndani na nje ya kaya.”
“Rais iko zuri sana. Kama nakuwa rais iko kula kunya, sorry, kunywa bure hadi toto na bibi yake. Mungu akupe nini dugu yangu?”
Machungi huku akiwa ameinamisha kichwa anasema kwa kunyong’onyea: “Imitisikitisha sana kuona mgosi mzima anajizaiisha kwa mwanaume mwenzake. Sisi kue Ushoto tishakubaiana akikanyaga tinamtia adabu kwei kwei sitanii.”
Bi Sofi aka Kanungaembe ambaye alikuwa kimya muda mrefu naye anaamua kukatua mic: “Mimi sioni ubaya watu kupashana kama wanalo la kupashana. Nadhani wale ambao si wanachama wangeachana na mambo ya chama na kushika yao.” Anamalizia akiwa amemkazia macho Kapende.
Kapende hangoji. “Haya si mambo ya chama bali kaya. Tuwapige chini ili wakapashane vizuri.”
Mpemba anakubaliana na Kapende. “Hawa kama siyo kusaidiwa na uchakachuaji, tungekuwa tushawasahau zamani wallahi. Maana walivoishiwa na kutifuana nadhani kila mtu aone ubovu wao.”
“Heri Mpemba umesema. Pia ongezea kuwa kama si njaa za wachovu na wendawazimu wao wa kupwakia takrima tungekuwa tushaanza kuonja matunda ya ukombozi. Hukumsikia baba yao Pio Msekua akisema kuwa wapingaji wakijiandaa vilivyo wakaungana wanaondoa manyang’au haya once and for all?” Anadakia Msomi.
Anakatua kashata na kuendelea: “Mie naona tatizo hapa si chama wala wakubwa zake wanovuana nguo hadharani. Hapa tatizo wachovu wenyewe kushindwa kutimua hichi chama kilichogeuka zigo tena la kunuka.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si likapita shumbwengu la Lowa-Sir akiwamo anamnong’oneza mgosi Makambaaa. Tuliwazomea na kulimwagia kahawa na kila mtu kutimka kivyake.
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 12, 2014.

No comments: