The Chant of Savant

Saturday 15 February 2014

Mlevi ataka 'amri' 10 zinazomhusu rais ziingizwe kwenye katiba

Rahisi Jakaya Kikwete

Mzee Vasco da Gama
Baada ya mlevi kugundua kuwa hayumo kwenye bunge la kujadili na kupitisha rasimu ya katiba mpya, amekuja na janja nyingine ya kushiriki kwa njia ya safu.
Hivyo, baada ya kutoka kuupiga unywaji na kugundua kuwa kumbe kitendo cha kuniengua nisishiriki kwa kuogopa vitu vyangu hakifui dafu! Nitashiriki watake wasitake.
Rais azuiwe kutumia njuluku za wachovu na walevi kwenda kutanua ughaibuni au kuzurura kama wasemavyo wabaya wake wao hupenda kumlinganisha na au kumuita Vasco da Gama.
Mie namheshimu sana. Siwezi kumuita majina ya kikoloni hata kama ikulu anamoishi ilijengwa na ina mambo ya kikoloni.
Kwanza, napendekeza rais aruhusiwe kutoka nje ya kaya mara moja kila miezi minne vinginevyo kama kuna ulazima aombe kibali cha kufanya hivyo toka kwa walevi aone tunavyoamua. 
Walevi tusibanwe. Ingekuwa si bunge kumilikiwa na chama kimoja, basi tungependekeza ndiyo liwe linampa rais ruhusa ya kwenda nje inapotokea lazima ya kufanya hivyo.
Kwa vile bunge linamilikiwa na chama kimoja, rais anaweza kulitumia kwenda kutanua na kuzurura.
Hivyo basi, walevi turuhusiwe kuwa na mamlaka ya kumruhusu rais kwenda nje kwa ulazima si chini ya mara mbili kwa mwaka.
Hii itaokoa njuluku ya walevi ukiachia mbali kumlazimisha rais kukaa ofisini na kufanya kazi badala ya kuzurura na kutanua huku akilipwa kwa jinai hizi.
Pia katika hizo safari atakazofanya ughaibuni, asiandamane na misafara mikubwa wala bi mkubwa wake.
Maana ukiangalia watu wanaokwenda na rais ughaibuni kushangaashangaa na kupiga picha unashangaa mantiki ya rais kuandamana na walaji wasio na sababu wala umuhimu.
Pili, rais alazimishwe kulipa kodi na mshahara wake uwe sambamba na ujuzi wake.
Kama ni ticha alipwe kama ticha na kama ni mlevi basi apewe michupa yake ya ulabu.
Tatu, rais ashurutishwe kutaja mali zake ili asije kutuibia njuluku kama ilivyo.
Kwenye siasa hakuna cha kuaminiana. Ukicheza na nyani unavuna mabua au siyo?
Isitoshe, kama rais hatuamini hadi anajizungushia mabaunsa kibao, tutamwamini kwa lipi?
Hakuna haja ya kumwamini mtu usawa huu ambapo urais umegeuka urahisi wa kutengeneza utajiri wa haraka.
Huoni unavyogombaniwa kiasi cha watu kutaka kutoana roho? Unafanya mchezo na ulaji wa dezo nini!
Nne, rais ashurututishwe kutoandamana na misururu ya magari kila aendapo. Wasiojua watasema misururu ya magari mia ya rais huwa ni kwa ajili ya usalama wake.
Urongo, mbona akistaafu hatumuoni akiwa hatarini kiasi cha kuandamana na misururu ya mikwara?
Kwa vile rais wetu si kibaka wala mhalifu, hana haja ya kuwaogopa watu anaodai kuwapenda kiasi cha kumwamini ulaji wao.
Kimsingi, mambo ya misafara mirefu ni ‘hangover na carryover’ za ukoloni. Gavana wa kiingereza alipenda kuandamana na misafara kwa sababu ya kutuchimba mkwara na kuogopa tusimfanyie kitu mbaya kutokana na alivyokuwa akituibia.
Je! rais wetu anogopa nini? Pia rais asiruhusiwe kuandamana na utitiri wa walaji aendapo ziarani.
Ili kuondoa ujambazi huu, katiba imlazimishe rais kutaja orodha ya watu anaoandamana nao kama ilivyokuwa wakati wa mchonga.
Walevi wamechoka na wadandizi hata waganga uchwara wanaoweza kupenyezwa kwenye msafara wa rais.
Kwa vile waswahili hupenda sana kutanua, hili lazima nife na mtu kuhakikisha linapita ili kuokoa pesa ya walevi ambayo imekuwa ikitumiwa kugharimia wadandiaji wanaofanya siri wakati wa matanuzi kama haya.
Tano, rais ashurutishwe kuwazuia watoto au wake zake kutumia madaraka yake kwa namna yoyote ile.
Mfano, ndugu za rais wasiruhusiwe kujiingiza kwenye siasa kwa kutumia jina au mamlaka yake.
Sita, rais ashurutishwe kuwa anatoa taarifa ya maendeleo ya serikali mbele ya bunge kila baada ya miezi minne.
Pia katika kufanya hivyo, bunge lazima limkague na kujiridhisha kuwa anachosema ni kweli ili kuepuka sanaa za kuja na ‘inflated stats’ kama ilivyo.
Saba, mlevi anapendekeza pia kuwa katiba imlazimishe rais kutangaza maslahi yake kwenye kila uteuzi atakaofanya.
Mfano, kama atataka kumteua mtu ambaye ama ni mshikaji, mshirika au rafiki au mtoto wa rafiki yake hasa wale wenye majina makubwa aeleze wazi kuwa ana maslahi katika mtu huyo.
Ikitokea rais akamteua mtu anayetia shaka, bunge limuondoe mara moja na kumuonya rais mara mbili ili mara ya tatu limsimamishe urais hadi atakapotia adabu.
Nane, rais ashurutishwe na katiba kutimiza ahadi atakazotoa kwenye uchaguzi.
Kama ataahidi maisha bora kwa wote na akatoa maisha balaa kwa wote, atimuliwe kabla hajachafua hewa.
Haiwezekani tukawa tunatapeliwa kila baada ya miaka 10 ati.
Pia ifanyike tathmini kuona kama rais anafaa kuendelea kula na kulala bure.
Baada ya mwaka mmoja wa kuwa madarakani, umma umpime kama ametimiza ahadi zake.
Kama ameutapeli, basi umtimue haraka ili wenye uwezo wa kutoa ahadi za ukweli wachukue nafasi yake na kufanya kweli.
Tisa, rais alazimishwe kutoa maelezo/utetezi atakapokabiliwa na shutuma zozote za kufanya kinyume na sheria.
Mfano, kama rais atatuhumiwa kukwapua pesa za HEPA au kushiriki kashfa kama za Richmonduli, basi aitwe mbele ya bunge ajieleze.
Kama maelezo yake hayataingia akilini wala kuliridhisha bunge, basi litoe idhini afikishwe mahakamani.
Kumi, katiba itamke kuwa hakuna aliye juu ya sheria ya kaya hii hata awe nani.
Nani malaika awe juu ya sheria asiitumie kuwakomoa wabaya wake? Nani anataka kesi za kugombea mabibi na upuuzi mwingine kumalizwa kwa kutumia madaraka ya rais? Tunataka rais muajibikaji.
‘So long guys’. Nakula ung’enge’ kuonyesha kuwa sikughushi kama wale wanaokula uswangilish mjengoni.

Chanzo: Nipashe Jumamosi Feb.15, 2014.

5 comments:

Jaribu said...

"Mikata Mibovu" iondelewe kwenye kamusi, iitwe kama ilivyo "wizi" na ifutwe pinde itakapojulikana. Vibaka na majangili wa kutupwa wasiitwe "Waheshimiwa", waitwe kwa namba zao za jela, kama Mfungwa Ukonga Ba-2224, n.k

Jaribu said...

Nahitaji kozi kama ya "Mheshimiwa" waziri wa fedha Mkuya, typing study.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Jaribu umeniacha hoi. Yaani una maana Saada Mkuyati Salum amesonga English na Typing Course siyo stashahada shahada na madude mengine kama hayo yenye majina ya kutisha? Nakubaliana nawe kuwa badala ya kuwaita waheshimiwa tuwaite kwa nambari zao. Mie huwa nawaita waishiwa bila kujali kama wana vyeo vikubwa au vya kughushi.Ndiyo maana blog hii ni machukizo kwao kwa vile huwa sirambi viatu wala makalio ya mtu zaidi ya kueleza usongo nilio nao.
Hata hivyo mapendekezo yako kwenye katiba mpya nitayafanyia kazi wakati nitakapoandika mengine maana huu sio mwisho bali mwanzo.

Jaribu said...

Mhango mwenyewe unajua kama kweli una stashahada ya biashara, huwezi kuiita "Business Study".

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Jaribu hujakosea. Huenda kwa lugha ya vihiyo maana ya maneno hubadilika na hutumika kukidhi matakwa yao. Natamani niende nikamoji huyu manzi mambo ya kitaaluma ili nimuumbue. Nijuavyo hawawezi kunikaribisha na wakifanya hivyo basi mwishowe watani-Kolimba kama siyo kuni-Mwangosi au nikinusurika basi wani-Kibanda.