Wednesday, 26 February 2014

Katiba mpya: Mgosi kwenda na mkewe

BAADA ya kijiwe kufanyiwa mtima nyongo na kuenguliwa kushiriki Bunge la Katiba, mmoja wetu Mgosi Machungi amejipenyeza kama mzee Kimdunge Ngumaru Mwehu aliyepitia chama cha waganga wa jadi. Mgosi Machungi ametuacha hoi kwa kuingia Bunge la Katiba kupitia chama cha wapiga ramli.

Kwa vile Mgosi Machungi anaenda kwenye neema ameishaanza kudengua hata kuotesha kifriji. Anaingia akitembea kama anayecheza kidembwa kama si mdumange.
Haamkui wala nini zaidi ya kuagiza kahawa na kujifanya yuko bize akisoma mnyuzipepa wake wa Danganyana Daima. Si unajua Mswahili akiangukia!
Akiwa amekula jiwe na kujifanya mbukuzi, Mbwa Mwitu anamchokoza akisema: “Mgosi sasa hii kashfa. Yaani unatukuta waheshimiwa kama sisi unajikausha hata huamkui!”
Mgosi anajibu: “Sasa unyonge basi. Ukiendeea kutifatafata titakutoa mpaka tikubindize kabua ya kutoboa mimacho ili kujibu mapigo. Siku hizi sina mchezo. Ukinikera naamuisha wahuni wenzangu. Titakufanyia kitu mbaya kama si ku-Mwangosi au hata ku-Ulimboka.”
Mbwa Mwitu na wanakijiwe hatuna mbavu. Anasema: “Kumbe umekuja na mawazo mfu ya Njaa Kaya kichwani! Ujibu mapigo kwa lipi na unyonge upi wakati sote hapa tunaheshimiana wala hatuibiani wala kuchakachuana kama Njaa Kaya na genge lake dhidi ya wapingaji wake?”
“Usanii sasa basi. Lazima tupate Katiba mpya itakayowabana wezi wakubwa ambao wanaotuibia na kututumia watakavyo. Kila anayekuja anatajirisha ukoo wake na hata waramba makalio yake. Ushenzi na ujambazi huu hadi lini?”  Anachomekea Kapende huku akibwia tangawizi yake kwa madaha. Leo zimemtembelea.  Hanywi kahawa chungu. Hata alivyouramba kwa kuchomekea utadhani limbukeni aitwaye Pedejee!
“Hakuna cha Katiba mpya wala nini.  Ni ulaji kwenda mbele. Mambo yalivyo, wachovu wasipoingia mitaani, wataingizwa mkenge kwa Katiba mbovu kuliko iliyopo kama alivyosema fyatu Living stone Ushindwe hivi karibuni kuwa genge lake limejiandaa kuichakachua Katiba kulinda masilahi yake.” Anazoza mzee Maneno.
Msomi aliyekuwa akibofya ki ipad anakula mic. “Hakuna waliponiacha hoi kutaka eti kumpigia debe fisadi Endelea Chenga kuwa spika wa Bunge la Katiba.  This is nonsense crap and malicious! Hivi ukishakuwa na spika jambazi unategemea uwe na Katiba ya kuweza kuzuia ujambazi, bwimbwi na ujangili wakati mtu wao ndiye ameshika patamu? Hapa naona unafiki na kigeugeu cha Njaa Kaya. Amewaingiza mkenge wachovu kuwa anataka kuwapatia Katiba mpya wakati si kweli.”
Kanji anakwanyua mic na kusoza: “Somi sasa changanya sisi. Tukufu iko taka kuwa na constution zuri. Lazima shukuru yeye hata kama napinga yeye.”
“Wapashe wamezidi hawa.” Anachomekea Sofia Lion aka Kanungaembe.
“Sofia acha kumchomekea Kanji au kwa vile ni mshikaji wako?” anatania Mbwa Mwitu.
Msomi anapuuzia utani na kuamua kujibu mapingo. Anasema: “Tuwe makini tunapowahukumu wengine.  Simhukumu Njaa Kaya bila ushahidi. Hivi kama Kanji anavyodai kuwa alitaka kutupatia katiba bora, iweje ateuwe zaidi ya 75% makada wa genge lake badala ya watu wasio na upande ili haki itendeke? Kwani Katiba ni ya mama yake au genge lake?”
“Du! Hapa umemshika pabaya Njaa Kaya! Kweli haya maigizo. Hukusikia jamaa aliyeteuliwa yeye na mkewe kwenda kufaidi njuluku zetu?” Anachomekea Mchunguliaji.
Mpemba aliyekuwa kimya anaamua kuchangia: “Mie hakuna kitu kilintisha kama watu kujadili jambo moja, yaani Muuungano. Nadhani kama twataka songa mbele basi tuunganishe kaya iwe moja badala ya kuwa na sirikali tatu zitazozidi tuongezea nzigo ati au mwasemaje jamani? Hili la nke mbona kawaida hata Njengoni?”
Mijjinga anaamua kutia guu kwa vile alichelewa kufika kiasi cha kukuta mada ishaanza hivyo akalazimika kuifuatilia kabla ya kutia guu. Anasema: “Ami unfurahisha sana leo wallahi. Ila haya usemayo usiende yasema kule kwenye visiwa. Hujakosea. Watu wawezapeleka hata hawara zao mjengoni na hakuna ubaya.” Anaongea akimuigiza Mpemba ambaye anacheka tu.
Mipawa anachomekea na kusema: “Actuare hapa umeongeaga pwenti. Watu wamekuwa wakijadili muungano hadi wanasahau maulaji ya rahisi, mfumo wa kifisadi, kurejesha maadili, kuondosha madili, kupunguza utitiri wa wilaya na mikoa na madudu mengine kama vile rahisi na wakubwa kutolipa kodi na kutumia vibaya njuluku za wachovu.”
Wakati wengi wakichangia kuhusu Katiba hawakuwa na habari kuwa Mgosi Machungi alishaukwaa ubunge wa Katiba. Hivyo, naye kwa kutambua hili anaamua kutamba. Anasema: “Tisikiizane. Hapa tinapoongea mjue minaongea na mheshimiwa Mgosi Machungi Shemtwashua wa Kiango mbuge asimi wa Bunge la Katiba. Kwanza, nipigieni makofi.”  Kila mtu anapigwa na butwaa. Wengine wanadhani ni utani.
Sofi Kanungaembe anamzodoa: “Mgosi acha ulimbukeni utapigwa makofi. Uchaguliwe Bunge la Katiba una sura, dola au sera. Halo halo!”
“Kwei duniani kuna watu na viatu. Pigeni makofi siyo mnipige makofi, hujui Kiswahiii nini? Niko nafanya mpango na mke wangu Mama Andallah naye ateuliwe ili tule kuku kama yue Mkaidi aliyependekeza jina la mkewe.” Anachomoa kitambulisho chake huku akimpa Sofi ajionee mwenyewe.
Sofi anapigwa bumbuwazi na kusema: “Mwenzetu kumbe umo kwenye ulaji!  Nijuavyo, wengi hamuendi kupoteza muda kutoa mapovu kuchangia bali kufaidi posho au vipi mshikaji.”
“Sofia tiheshimiane. Hivi mama Andallah akimisikia unadhani ataacha kukupiga zongo? Tinaende kue kutetea haki zenu waa sina njaa kama chama chenu. Tinaenda kue kubomoa mfumo huu wa kifisadi ambao umeticheesha kimaisha na kumaiza rasiimali zetu.”
Mipawa anachomekea: “Kweli muendage kututetea badala ya kwenda kutafuta vidosho kama waishiwa ambao juzi juzi walifichua kuwa kila mmoja ana wake mjengoni. Je, utampa fisadi mzee wa Vijesenti au Sam Sixx?”
“Hayo matusi sasa.” Anang’aka Mgosi. “Namaanisha kura,” Anajitetea Mipawa. “Yue hata kigombea na mbwa nitamchagua mbwa kuiko yeye.” Anajibu Mgosi huku akitoa oda ya kahawa kwa wanakijiwe wote ili wafaidi neema iliyomtembelea.
Msomi kapata upenyo. Anazoza: “Tuache utani. Kama fisadi wa vijisenti atasimikwa mjue hakuna Katiba. Hapa unafiki wa Njaa Kaya ndipo utakapofichuka. Kama wachovu hawatakuwa tayari kuingia mitaani kupinga Katiba mchakachuo kama mikakati ya sasa ya mafisadi kupenyeza watu wengi itafanikiwa, mjue mtakuwa mmeliwa mara mbili, yaani mtaikosa Katiba na mtaliwa njuluku bure.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si tawi la mwembe likakatika.  Tulidhani mabomu ya ndata au al Shubbub!
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 26, 2014.

No comments: