Tuesday, 25 February 2014

Ukuaji wa uchumi unapokuza umaskini

 
          Juzi nilifurahi sambamba na kuchukia. Ni pale runinga ya Afrika Kusini ilipoonyesha kuwa uchumi wa Tanzania utakuwa kwa kasi kuliko chumi zote duniani miaka michache ijayo. Baada ya kuona hili nilianza kuangalia uzuri na ubaya wa kukua uchumi kwa kasi kwenye taifa linaloongozwa kifisadi. Je uchumi wetu utakapokuwa nani atafaidi kati ya wananchi na makuwadi wa wawekezaji ambao wamehakikisha kila kitu kinawanufaisha wao na mabwana zao? Rejea kugundulia utitiri wa madini ambao matokeo yake ni utitiri wa mashimo na kashfa kiasi cha kuwaacha watu wetu maskini na wakimbizi kwenye nchi yao. Nani amesahau mauaji ya watu wasio na hatia kule Mara kwa kosa la kukatisha kwenye mgodi? Nani amesahau magonjwa ya hatari yanayowasumbua wakazi wa huko huko Mara ambao kemikali zimenyiririshwa kwenye vyanzo vyao vya maji?
          Je kuna haya ya walalahoi kushangilia habari hii au kuomboleza kwani kukua kwa uchumi wa Tanzania kwao ni chachu ya kukua kwa umaskini? Hivi unategemea nini toka kwenye nchi inayogawa raslimali zake bure au kuharibu mali za umma kama vile kuuza mashirika ya umma kwa bei ya kutupwa kama ilivyotokea kwenye uuzaji wa iliyo kuwa Kampuni ya Usafiri Dar es salaam (UDA), NBC na mashirika mengi?
           Taarifa za ukuaji wa uchumi wa Tanzania zilizotolewa mwaka 2012 na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Morrice Oyuke zilionyesha kuwa uchumi wa Tanzania ungekuwa kwa asilimia 7.1. Hili ni jambo la kujivunia. Kinachogomba ni kwamba huyu mtakwimu hakueleza ni kiasi gani umaskini utakuwa. Wapo waliosema kuwa umaskini ungeongezeka kwa asilimia 5 na ushei sambamba na ukuaji huu. Je hii inatoa picha gani? Wapo wanaoona kama takwimu tunazoletewa ni za ungo wa kawaida. Na hii inaweza kuwa kweli hasa tukizingatia jinsi takwimu zinavyoweza kuficha ukweli kama alivyowahi kusema, Joel Best kwenye kitabu chake cha Damned lies and statistics, “Mujumuisho ni hatua muhimu katika kufikiri kitakwimu. Mara chache twaweza kuhesabu matukio haya yote ya kijamii. Badala yake, tunakusanya baadhi ya ushahidi kutokana na sampli na kutoa hitimisho la jumla,” (uk.6). Sambamba na hili Benjamin Disraeli (1804–1881) waziri mkuu wa Uingiereza aliwahi kusema, “There are three kinds of lies: lies, damned lies, and statistics.” Hatuna tafsiri ya nukuu hii.  Pamoja na kwamba si takwimu zote zinaficha uongo, kuna haja ya kuwa makini na takwimu hasa katika kuzilinganisha na ukweli halisi.  Kwa wanaojua udhaifu wa takwimu, wanajua ninachoongelea hapa. Takwimu zinaweza kuonyesha picha tofauti na hali halisi kama ilivyo kwenye suala la kukua uchumi wa taifa. Ukitaka kujua uongo wa takwimu hebu nenda vijiji uangalie aina ya maisha wananchi wanayoishi. Huwezi kukuza uchumi kwa takwimu bali uzalishaji na matumizi bora na nidhamu ya pesa na raslimali za umma jambo ambalo ni msamiati mgeni nchini.  Huwezi kukuza uchumi kwa midomo au kisiasa au kwa kupika takwimu. Mwandishi wa makala hii ni muumini wa dhana tofauti na takwimu. Anaamini kuwa ukuaji wa kweli wa uchumi hauelezeki kwa takwimu tu bali unaweza kuelezewa vizuri na wakati maskini wa vijijini au mabandani mijini. Hali za maisha ya makundi haya ya wasio nacho zinaweza kutupa picha nzuri na ya kweli kuhusiana na kukua kwa uchumi. je wanapata huduma bora? Je wanaridhika na mambo yanavyokwenda? je wanashirikishwa kikamilifu? Je wanawezeshwa? je wanapewa taarifa muhimu? je wana welewa wa taarifa husika kiasi cha kuzichambua na kuzifanyia kazi ikiwamo na kuzikubali au kuzikataa? Haya ndiyo mambo ya kuzingatia katika kutoa tafsiri ya kukua kwa uchumi. Je waliotoa taarifa za ukuaji wa uchumi wetu wameyazingatia haya? Jibu ni hapana tena kubwa tu.
          Kwa wanaojua udhaifu wa uwekezaji nchini, bila shaka wanategemea ongezeko la wamachinga wanaojiita wawekezaji toka India, Pakstani, Bangladesh, China na kwingineko. Pia wanategemea utoroshaji wa mtaji na raslimali kuongezeka kutokana na mamlaka zilizopo kupoteza muda kwenye kusaka rushwa badili ya kukusanya mapato na kubana mianya ya kutorosha mitaji na mali za umma. Uliza madini kama Tanzanite yameisaidia nini Tanzania zaidi ya kuwa laana na msaada kwa nchi jirani ya Kenya na India?
          Je uchumi wetu utakuwa kiuchumi au kisiasa? Kwa wanaojua ukuaji wa uchumi wa kisiasa ambao ulielezewa na rais Jakaya Kikwete aliposema kuwa ukiona mitaa yetu finyu imejaa misongamano ujue uchumi umekuwa kiasi cha watanzania wengi kuwa na mikangafu. Tofauti, ukuaji wa kisayansi ni ule unaowezesha nchi kuongeza pato lake na kupunguza utegemezi katika misaada au kuagiza zaidi ya unavyouza. Je Tanzania nchi iliyojaa bidhaa zilizo chini ya viwango kutoka India na China kweli inaweza kuwa na ukuaji wa kujivunia kwa watanzania?
Tujalie kuwa uchumi wetu kweli utakua, je utafua dafu kwenye matumizi mabaya ya kisiasa ambapo tumezalisha mikoa na wilaya nyingi kukidhi mahitaji ya kisiasa badala ya matakwa ya wananchi?  Je ukuaji huu uliotabiriwa utaondoa au kupunguza uombaomba wa nchi yetu ambapo bajeti yetu hutegemea michango ya wafadhili kana kwamba hatukujaliwa raslimali?
Tukifie mahali tuuangalie ukweli kama ulivyo kwa kujitenga na kujipigia debe kisiasa ili wahusika wachaguliwe tena wafanya madudu tena. Swali linalopaswa kuulizwa na kujibia kwa utuo ni: Je uchumi wa Tanzania unapimwa na nani na nini katika ukuaji wake? Je ukuaji, kama upo, unamnufaisha nani na vipi?
Ukuaji wa uchumi unaowaacha nje maskini ambao wanaona umaskini na uduni wa huduma vikiongezeka hauna maana. Watawala wetu wanapaswa kufikiri kabla ya kutuletea takwimu za ajabu ajabu zilizokaa kikampeni zaidi ya sayansi. Je inakuwaje uchumi wa Tanzania unakuwa sambamba na umaskini?
Chanzo: Dira Feb., 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Miaka kumi iliyopita £1.00 ya Uingereza ilikuwa na sawa na thamani Tsh 1450.00.. Leo hii £1.00 ni sawa na Tsh 2700.00.

Je unahitaji kuwa Professor au ma-Dokota(Dr) kutafsiri hizo takwimu zinatolewa kuhusu maendeleo ya uchumi wa Tanzania...!

Mimi katika familia yangu miaka nane iliyopita ilikuwa angalau kulikuwa na watu nne wakiwa na ajira ya kudumu. Leo hii hakuna hata mmoja kwenye ajira ya kudumu.

Kama unavyojua ile kamati yetu iliyoundwa na Mr ambaye mara nyingi anawasema watanzania ni wavivu wa kufikiri ambapo yeye amekuwa madarakani katika ngazi tofauti na kupanda vyeo mpaka kufikiwa kuwa Rais.

Hivyo udhaifu wa kufikiri ninapozungumzia unaanzia wapi kama si kwake yeye mwenyewe na kuendelea hadi ngazi ya chini. Ushahidi yeye alikuwa madarakani kipindi kirefu tuu na nchi imeendelea kuwa maskini na huduma duni za kijamii siku hadi siku. Hata kamati yake aliyounda ni uthibitisho kuwa naye yeye ni mvivu wa kufikiri

Kamati iliundwa kwa jina la kurekebisha/ubinafsishaji mashirika umma lakini kilichokuwa kinafanyika ni uvivu wa kufikiria kama ambavyo Mr msataafu Rais anavyofikiri kuhusu uvivu wa kufikiri kwa sisi Watanzania...yaani kuuza kila shirika badala ya kurekebisha tena kwa bei chee au buree wakti mwingine.

Kifupi hizo takwimu za maendeleo ya uchumi ni sawa kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa! Mpaka sasa Wagonjwa wanalazwa sakafuni au kutimia kitanda kimoja wagonjwa wawili...Vyoo vya umma au hospitali imekuwa sehemu ya kuweka uchafu badala kupitisha uchafu

Au Kama Bwana JK aliposema hivi karibuni akutukanaye akuchagulii tusi(ingawa yeye alikuwa akijaribu kubishana na ukweli) kuubalisha kimaoni kuwa ni uwongo ingawa kila kitu kilikuwa katika video kuhusiana na mahuaji wanyama pori hasa tembo na faru na wahusika katika hiyo biashara

NN Mhango said...

Anon,
Wasomaji wangu wakifumba mimi hufumbua. Bila shaka huyu unayemaanisha si mwingine ila Benjamin Mkapa rais wa hovyo aliyesifika kwa majivuno, kupayuka na kutawaliwa na kutumiwa na mkewe. Ni Mkapa huyu huyu aliyetuuza kwa wawekezaji hata mafisadi alipoasisi wizi wa EPA uliomuwezesha Dr Zero kuukwaa urais ambao ameugeuza urahisi wa kufanya ufisadi. Nakubaliana nawe kuwa huyu bwana ni bingwa katika uvivu wa kufikiri na alichosema ni kama alikuwa akijipiga kijembe bila kujua. Ila kwa vile yu mvivu wa kufikiri hakujua kuwa alikuwa akijisimanga mwenywe.