Wednesday, 19 March 2014

Barua ya wazi kwa Godfrey Mgimwa

BWANA mdogo Godfrey William Mgimwa, Kwanza nina kusalimu kwa kusema, habari za kampeni dogo?
Baada ya kusoma mahali ambapo ulikaririwa ukisema kuwa unataka kuwaletea maendeleo watu wa Kalenga ambao baba yako hakuwaletea hayo maendeleo, imebidi nikuandikie waraka huu ili walau upate kukumbuka la kusema na la kuacha.
Kwa mfano ulikaririwa ukisema, “Kipaumbele changu cha kwanza ni elimu, cha pili kilimo, cha tatu miundombinu na mawasiliano; hizo ni baadhi ya kazi nitakazofanya ili kuwaletea watu wangu maendeleo.” Je, hiyo pesa ya kufanikisha haya utaipata wapi wakati baba yako unayetaka kumrithi aliruhusu pesa ya umma kuibiwa na kufichwa Uswisi? Nakumbuka aliwahi kusema, “Sisi hatutakaa kimya, tunafuatilia wote walioweka fedha nje ya nchi, tunaangalia namna fedha hizo zilivyohamishwa na tumeanza kazi hii kwa kushirikiana na nchi ambazo, inasemekana fedha hizo zimefichwa. Yeyote atakayebainika kuhamisha fedha kinyume na utaratibu, tutamchukulia hatua.”
Kauli hii aliitoa mwezi Desemba 2012. Habari tulizopata hivi karibuni ni kwamba kumbe alichoahidi baba yako ni kuwawezesha walioficha pesa Uswisi kuichota na kuihamishia maficho mengine ambayo hayajafichuka.
Rejea taarifa iliyotolewa hivi karibuni na balozi wa Uswisi nchini Olivier Chave aliyesema, “Hadi mwisho wa 2012, fedha zilizopo kutoka Tanzania zimebaki Faranga za Uswisi 160 milioni (Dola za Marekani 182.2 milioni) na si zile za awali ambazo ni Faranga za Uswisi 180 milioni (Dola za Marekani 327.9 milioni)……. hivyo ndiyo kusema kuwa fedha hizo zinapungua.”
Je, Mgimwa mdogo unaweza kuwaambia watu wa Kalenga ni wezi wangapi walikamatwa au hata kutambuliwa na kile alichosema marehemu baba yako kuwa kilikuwa kinafanyika?
Swali jingine dogo, Bwana Godfrey, hebu tuwe wakweli. Kama unavaa viatu vya baba yako kuboresha elimu na mambo mengine, ilikuwaje baba yako alishindwa kuiboresha hiyo elimu hadi akakukimbizia Uingereza kusoma badala ya kusoma hapa?
Je, una habari kuwa kukiri kuwa elimu, kilimo na miundombinu ni duni ni ushahidi kuwa baba yako hakuendeleza vitu hivyo pamoja na kuwa waziri wa fedha kwa muda mrefu?
Maana kama angeendeleza vitu hivyo, basi visingekuwa kipaumbele chako. Ama kweli wahenga walisema: Nyani haoni nonihino lake.
Mwanzoni mwa mwezi huu ulikaririwa na vyombo vya habari ukisema, “Maendeleo ya jimbo hili yataletwa kwa kutekeleza Ilani ya CCM ya 2010 lakini kuna ahadi zilitolewa na Dk. Mgimwa nje ya Ilani hiyo; niaminini nitazifanyia kazi.” Tuache utani Bwana Godfrey na tuwe wakweli. Kama hauna maendeleo ina maana marehemu baba yako hakufanya lolote hasa ikizingatiwa kuwa hadi anakufa hakutekeleza ahadi zake. Wengi wanashangaa. Ukiangalia muda uliobaki bila marehemu kutekeleza ahadi zake, je, angezitekeleza lini wakati muda umekwisha? Kitu kingine ambacho kinanifanya nikune kichwa na kuuliza, unaposema utazifanyia kazi ahadi alizotoa baba yako bila kuzitekeleza una maanisha nini zaidi ya kukiri kuwa alitoa ahadi sawa na chama chako bila kuzitekeleza?
Je, ni kwanini hukueleza jinsi utakavyotekeleza hizo ahadi? Ni kwanini ukiziorodhesha au uliogopa ukubwa na unyeti wake ili wapiga kura wasigundue janja iliko nyuma ya ahadi za jumla bila kueleza jinsi ya kuzitekeleza?
Ukiwa katika Kijiji cha Magubike ulisema wakati wa uhai wake, Dk. Mgimwa aliahidi kutoa mabati 400 kwa ajili ya ujenzi wa shule na zahanati ya kijiji hicho. Ulikaririwa ukisema:“Pamoja na ahadi hiyo aliahidi pia kutoa sh milioni moja kwa kikundi cha wajasiriamali wanawake, nazichukua ahadi hizo na nitazifanyia kazi.”
Je, ni kwanini hukueleza ni kwanini baba yako hakutekeleza ahadi hiyo? Je, kama aliahidi pesa kidogo kiasi hicho hasa ukizingatia cheo na uzoefu wake, wewe mtoto utaitekeleza vipi? Kama kawaida, kweli mtoto wa nyoka ni nyoka. Umetoa ahadi kama alivyofanya baba yako bila kueleza ni vipi na lini utaitekeleza?
Utani mbali, je, ungeahidiwa wewe kitu kama hiki bila kuambiwa lini na vipi kitatekelezwa ungemwamini anayefanya hivyo hasa ikizingatiwa kuwa hata baba yako alikudanganya hivyo?
Hebu nikurejeshe kwenye habari hii iliyokukariri wewe hapo Januari mwaka huu ikisema: “Godfrey alitaja miradi minne ambayo baba yake alimweleza kuwa alikuwa anataka kuwatekelezea wakazi wa jimbo hilo kuwa ni pamoja na umeme, minara ya simu, uanzishaji wa ushirika wa kuweka na kukopa na barabara.”
Wow! Hii ni siasa ya aina gani zaidi ya kuwa ubabaishaji? Haiingii akilini kwa mtu aliyechaguliwa kuwa mbunge eti kukaa zaidi ya miaka mitatu eti atekeleze kilichomshinda ndani ya miaka mitatu katika miaka miwili. Baya zaidi, ni uongo usio na kifani kwa mwanae kusema eti atakeleza kwanza, yaliyomshinda baba yake na pili ndani ya mwaka  na ushei wakati baba yake alishindwa ndani ya kipindi kirefu mara mbili ya muda huu. Are you serious Godfrey?
Hakuna uliponiacha hoi kama uliposema: “Mimi ni mtaalamu wa biashara, masoko na fedha; na mpaka nakuja kugombea ubunge nilikuwa mwajiriwa wa benki, kwa hiyo marehemu mzee (Mgimwa) alikuwa anaujua uwezo wangu kichwani na alikuwa akitaka ushauri wa mara kwa mara kutoka kwangu.”
Godfrey unamdanganya nani? Una maana kuwa wewe ulikuwa mshauri wa baba yako wakati alikuwa na wataalamu waliobobea kwenye hizo nyanja tena wenye uzoefu na shahada za juu walioajiriwa kufanya kazi hiyo? Unweza kutupa faida mojawapo ya ushauri wako ukiachia mbali kujisifia kwa vile unajua hakuna jinsi ya kuhakikisha ukweli wa usemi wako?
Tumalizie kwa kukushauri kwa ufupi tu. Kusema ule ukweli, malezi yako hasa kielimu na chama chako havifanani na wale unaowahadaa kuwa unataka kuwakomboa kwenye hali ambayo ilisababishwa na baba yako na chama chenu.
Kazi ni kwa wana Kalenga kuepuka kuingia mkenge. Maana ukiangalia usemayo, historia yako na ukweli wa mambo, kuna mengi unaficha au kushindwa kuyatolea majibu mfano: Ni kwanini baba yako hakutimiza hizo ahadi alizotoa tena kwa muda mrefu mara mbili ya huu unaoahidi kufanya hivyo bila kueleza ni vipi utafanya hivyo.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 19, 2014.

No comments: