Friday, 21 March 2014

Idadi ya serikali haiamuriwi na Shein

          Maneno makali ya hivi karibuni ya rais wa Baraza la Mapinduzi Zanziba (BMZ) Dk. Ali Mohamed Shein si ya kupuuziwa. Shein kwa makusudi mazima, anajua fika kuwa uamuzi wa Tanzania itakuwa na serikali ngapi baada ya kupitishwa Katiba Mpya ni wa watanzania. Ajabu pamoja na kujua hilo, Shein ameamua kujipotosha na kuupotosha umma kuwa yeye ndiye mwenye kauli ya mwisho juu ya ni serikali ngapi Tanzania iwe nazo.
Shein alikaririwa akisema, “…Serikali mbili tulikubaliana, nataka nirudie serikali mbili tulikubaliana… Sisi kwa pamoja tulikubaliana kuunda tume maalumu itakayoratibu mambo ya kutunga Katiba Mpya, sote tukakubaliana, ikapitishwa bungeni ikawa sheria, Serikali mbili tulikubaliana.”
Kwanza, ingekuwa vizuri Shein kutueleza walikubaliana wao na nani na lini na wapi na kwa amri ya nani? Kama anaongelea makubaliano yao ya CCM amenoa. Tanzania ni zaidi ya CCM. Kama kuna makubaliano ya siri basi ajue ikifichuka na kutowashawishi wahusika bado wataunda hizo serikali tatu.
Kimsingi kama tutaacha usanii na kuendekeza maslahi uchwara ya pande, hapakupaswa kuwapo na serikali isipokuwa moja tu ya Tanzania. Hichi kiini macho ambacho kimeendelea kwa miaka 50, kama tunataka kusonga mbele lazima kife. Hatuwezi kujaza utitiri wa serikali ili kuwapa ajira wanasiasa wakati wananchi wakiendelea kuwa maskini. Kwa vile Shein ni mnufaika wa utitiri wa serikali sawa na CCM bila shaka atatetea serikali zaidi ya moja. Kimsingi, watanzania hasa wa bara hawataki serikali nyingi. Kwani ni mzigo kwao. Visiwani wapo wanaotaka serikali mbili ili waendelee kutawala na wanaotaka kila mtu aende kivyake ili watawale nao. Kimsingi, kinachogomba kwenye muungano ni mgongano wa maslahi ya kimakundi zaidi ya watawaliwa.
Kwa safu hii, wanaotaka serikali mbili na tatu, wote hawaitakii mema nchi yetu.  Shein alikairiwa akisema kuwa muungano wa Tanzania ni tunu ya Afrika. Alisema, “Muungano huu ni fahari ya Afrika na unatumika kama mfano na kigezo kwa nchi nyingine za bara hili katika kuleta umoja na muungano wa kweli.”  Si kweli. Kama muungano huu ni fahari ya Afrika, kwanini basi tusiungane tukawa nchi moja badala ya kujilinganisha na nchi ambazo hazina hata huo mpango wa kuungana hasa baada ya kujaribu zikashindwa kutokana na kutokuwa tayari kufanya mizengwe kama tunayofanya?  Nani hajui kuwa kwa mfano Senegal na Gambia ziliungana na kuunda Senegambia lakini muungano ukafa ndani ya kipindi kifupi kutokana na kuepuka mizengwe?  Tujalie muungano ni fahari ya Afrika, kwanini Afrika kwanza na si Tanzania kwanza?  Nadhani watanzania wanataka muungano si kuwa kuifurahisha Afrika bali kukidhi mahitaji yao na kudumisha uhusiano wao wa kihistoria. Hata huu muungano ambao kwa wingi wa serikali zake ni mgongano si tunu. Tunu ipi yenye mizengwe na migongano?
Japo wahusika hawataki kusema ukweli, kinachoendelea si muungano kitu bali zengwe na kutumiana. Utashangaa kuona kwa mfano, watu kutoka Zanzibar wakiteuliwa kwenye kila aina ya vyeo kuanzia vidogo hata vikubwa. Wanaishi kila mahali wakifanya kila wanachotaka. Ajabu hawa hawa wanaodai kuungana, wanawekeana masharti kwenye wapi pa kuishi na serikali gani kushiriki. Si hilo tu. Zanziba imekuwa ikiumomonyoa muungano kwa kuzidi kuondoa baadhi ya mambo ambayo kimsingi yalipaswa kuwa ya muungano. Rejea kwa mfano kuanza kulalamikia mafuta baada ya kugunduliwa. Mungu si Athumani walipoambiwa kuwa wanaweza kugundua mafuta kwenye eneo la Zanzibar si Tanzania, Mungu akatoa neema ya gesi kule Msimbati jambo ambalo kwa kiasi fulani limetia maji malalamiko ya Zanziba na mafuta yao ambayo hayajachimbwa hata tone. Huu ni umimi mimi na chako kitamu changu kichungu. Hatuwezi kufika mbali namna hii.
kama watanzania watakuwa wakweli wakaachana na unyonge na udhalili wa kutaka serikali ya Tanganyika na upuuzi mwingine kama kuogopa kumezwa, basi Tanzania kama inataka kuionyesha mfano mzuri Afrika basi iwe na serikali moja rais mmoja katiba moja na watu wamoja badala ya maigizo ya sasa ya kuwa na raia watanzania na wazanzibari. Huu ndiyo upogo udhaifu na hata unafiki wa watawala wetu.
Uzoefu wa visiwa kama Comoro ni kwamba Zanziba pamoja na kudai serikali mbili ili wabaki na mamlaka yao, wanajua fika kuwa wanautaka muungano kuliko bara kwa vile wao wana manufaa zaidi. Nani hajui kuwa bila kuingia kwenye muungano, serikali ya Abeid Aman Karume isingedumu hata miezi mitatu? Nani hajui kuwa nje ya muungano Zanziba haitaonja amani kutokana na mgawanyiko na uhasama uliopo baina ya wazanzibari na wapemba? kimsingi ukisema Zanziba chukua hamsini zenu kesho yake utawasikia CUF wanataka ima uchaguzi kesho ili waishinde CCM ambayo ushindi wake siku zote unatokea Dodoma au hata kuingia mitaani kuondoa utawala wa CCM ambao kimsingi kwa baadhi ya wazanzibari ni pandikizi.
hivyo, viongozi wa  Zanziba hasa wa CCM kama watapewa wachague moja kati ya kuwa na serikali moja au kuchukua hamsini zao, watachagua serikali moja ili kuwa nusura na salama yao. Kwa vile wanajua udhaifu huu, huwa wanajitahidi kujifanya kuwa haupo na kushikilia kile kinachowapa uwepo kwenye ulaji. Shein analifahamu hili fika.
Tumalizie kwa kumtaka Shein na CCM waache kuwapangia watanzania nini wafanye kwa vile wakifanya tofauti itakuwa tofauti na maslahi yao. Kama Shein na CCM ambao wana msimamo wa serikali mbili wakitaka kuwanyamazisha wanaotaka serikali tatu basi wakubali kuunda serikali moja na kuifanya Tanzania kuwa nchi moja badala ya ilivyo sasa.vinginevyo mvutano wa idadi ya serikali ambazo kimsingi ni mzigo kwa watanzania utaendelea. Kwani hawa wanaotaka serikali tatu wanalazimishwa na mizengo na unyonyaji uliopo.
Chanzo: Dira Machi, 2014.

2 comments:

Jaribu said...

Nakubaliana nawe. Iwe ni serikali moja au tuwaambie WaZanzibar wasisahau kufunga mlango wakiondoka.

NN Mhango said...

Jaribu, wengi wanapenda hili ila wanaogopa kulisema tokana na woga tu.