Saturday, 29 March 2014

Mlevi kutua Dodoma kutoa darasa la Katiba

Najua wengi, hasa wale wanaoshabikia mambo ya ajabu ajabu kayani, hawatapenda utume huu. 
Najua fika kuwa wengi wa wanaonicheka kwa ulevi na mibangi yangu wataona kama ninavuka mipaka kutaka kufanya mambo ambayo si ya kilevi.  
Sasa nifanyeje kama wale tunaodhani kuwa watu wazima tena wasiolewa ulabu wanapoanza kuonyesha wazi kulewa maulaji kiasi cha kufanya mambo ya ajabu ajabu? Heri walevi tuingilie kati pale tunapoona mambo yanakwenda ndiyo sivyo tuokoe jahazi.  
Hatulipwi mamilioni kusaidia kaya kufikiri na kufanya mambo ya maana tena kikubwa na kiakilini. 
Baada ya kila mlevi wa maulaji kujiendea Dodoma kwenye bunge la ulaji la Katiba kupiga kampeni ya sera za chama au genge lake na wengine kuvuruga mambo kabisa, Mlevi ameamua kushuka kule kusafisha hali ya hewa.  
‘I’m goin’ thither to vacuum clean everything’.  Siendi kusaka ulaji wa bure, kula kuku wala kufaidi vyangu wala kulalamikia mishiko ambayo kimsingi ni kuwaumiza walevi walipa kodi.  
Kwanza, naogopa miwaya ukiachia mbali kutopenda mikuku na mibata. Nshazoea mapupu na utumbo mikuku na mibata na mishumbwengu ya nini? 
Nakwenda kule kukwamua mambo na kuepusha aibu kwa vizazi vijavyo baada ya kugundua kuwa busara imetoroka.  Kuna siku jina langu litafundishwa mashuleni kama sauti ya wasio na sauti na mtume kwa walevi. Nakwenda kutoa shule si malalamishi wala hoja za kupoteza muda na busara wala kuviziana ili kupata pwenti na credit.  
Siendi kule kijivua nguo au kutetea upuuzi kama waliofanya hivyo hivi karibuni. 
Nakwenda kuwa refa na si refa mchezaji. Nakwenda kuikomboa kaya toka kwenye mkwamo na ukosefu wa busara na uzalendo. 
Hali ya hewa mjengoni inahitaji kusafishwa baada kuchafuliwa juzi juzi na jamaa ambaye leo sitamtaja kwa vile kila mmoja anamdeku. 
Kwa vile watu wanataka kunyotoana roho wakigombea utitiri wa siri-kali, nina jibu la ugomvi huu. 
Siri, sirikali lazima iwe moja.  Itaondoa kelele zote kuhusiana na gharama za utunzaji wa utitiri wa siri tena kali zisizo na kichwa wala miguu.  
Isitoshe, kama sisi ni kaya moja, hatuna haja kuwa na vijisiri tena vikali vya kiulaji vingi bila sababu wakati ni ombaomba na kapuku wa kunuka. 
Hapa lazima niweke wazi. Hakuna cha kumeza,   kumezwa wala kumezana bali kuungana na kufanya mambo kama watu wazima wenye akili timamu au vipi? Mficha uchi hazai ati. Kila mmoja akishikilia yangu yangu kama vyura hatufiki. 
Juzi kwenye kanywaji walevi wakiwa wananiagiza kuandika utume huu na kujiandaa kutinga Dom bila kustukiza wala kuvizia ili kuua hoja za wenzangu, waliniuliza mantiki ya Tanganyika na Zenj.  
Niliwapa kuwa ukiunganisha Danganyika na Zenj na kila mmoja akabaki na identity (utambulisho) yake unapata Tanzia. Finito.  
Watawala wanawala watawaliwa na kudai idadi ya sirikali watakazo dhidi ya zile wanazotaka walevi. 
Niliwajibu tena kabla ya ulabu kupanda ‘upstairs’ kuwa kinachoendelea ni woga na uchumia tumbo ambapo watu wazima wanaogopa vitu visivyokuwepo. 
Kuna mlevi alitoa mpya pale aliponishauri nikifika Dom niwaambie hawa wapenzi wa utitiri wa serikali kuwa kama wakiendelea na ulevi wao wa ulaji basi kila mkoa ujitenge na kuanzisha sirikali yake tuone hizi mbili au tatu wanazotetea zitapata pa kukusanya kodi au kukopesheka kama alivyosema Kanali Njaa Kaya kuwa virungu na mituringa ya ndata na ndutu haiwezi kuisaidia sirikali ya mgongano kukopa.  
Sisi walevi hatutegemei kukopa bali kutunza na kutumia raslimali na fedha zetu vizuri.
Isitoshe, kama sisi ni wamoja kweli kweli tushikane haswa. Maana kama tunaogopana na kubebeshana mizigo basi tambo zetu kuwa tu wa moja tunaounganishwa na historia yetu ni urongo na sanaa tupu tena vyenye kuchosha na kuchefua. 
Wakati mwingine wale tunaodhania ni wema hutokea wakawa tofauti.  
Hebu fikiri kwa mfano mtu anayefuja zoezi la sasa la kutafuta Katiba Mpya ni mbaya kiasi gani? Hebu fikiri mtu anayekwenda pale ima kutafuta mshiko au kutetea upuuzi ‘simply because’ unamwezesha kupata ujiko hata ulaji hata kama ni kwa kuwauza wenzake ni mbaya kiasi gani? Kweli huyu si jangili anayeua na kuuza walevi?  
Philip Zembaldo’s The Lucifer Effect: Understanding How Good People Turn Evil tells us how those we think to be good people can turn out to be evil to the extent that we can’t express’. Zimbaldo says, “Evil is knowing better, but willingly doing worse.” 
Kuna siku niliwaacha wanafunzi wangu bila mbavu wakati ule nikifundisha chuo kikuu fulani ila si cha Manzese. Tulikuwa tukiongelea ugonjwa wa ‘Malignant narcissim’ ambapo mwenye kuugua hupenda ujiko na kutanua bila sababu.  
Huwa na tabia ya kuchekacheka kama aliyeugua kiharusi ukiachia mbali kuanguka anguka kama mwenye kifafa. Huwa akiambiwa kuwa anachofanya kina madhara ima kwake au kwa wenzake  huminya. 
Ilipofikia kutaja ya wale wanafunzi waliodhani kuwa na ugonjwa ule, waliwataja madingi fulani pale chuoni kiasi cha kuwasihi wasitishe zoezi hasa ikizingatiwa kuwa wengi wa wagonjwa ni watu ambao huwezi kuwategemea. Kwa ufupi ni kwamba wenye ugonjwa huu ni wabinafsi kupita kiasi. 
Wangetaka kila kitu wachukue wao ama marafiki au familia zao. 
Ulaji kwao ni suala la kifamilia au kichama au kikigwena. 
Hayo tuyaache. Nimalizie kwa kusema kuwa nitaunda tume ya walevi ya kuangalia mapendekezo ya katiba mpya. Tofauti na hizi tulizoshuhudia za akina Waryuba sitaivizia wala kuiponda wala kuizodoa tume yangu hata ikitoa mapendekezo ambayo sikubaliani nayo. 
Wakindekeza njaa wangoje walevi kuvamia ukumbi na michupa yao na kufanya vurugu.
Leo salamu maalum ni kwa mlevi afande Didi aka Mzee wa Mabao aliyeko huko…siri kubwa! 
Didi kinehe nyanda?
Chanzo: Nipashe Machi 29, 2014.

4 comments:

Anonymous said...

Nafikiri haya maneno"http://www.youtube.com/watch?v=VxA5cxdQ2uA" makini kabisa ya Kizalendo ambayo hajazungumziwa au kutekelezwa mpaka sasa alitamka na uthubutu wa hali ya juu kabisa Mchungaji Msigwa bado hayajaeleweka au ujumbe kumfikia kila Mtanzania au pengine ndiyo tatizo kuu la kudumaa akili zetu sisi wa watanzania, inawezekana ndiyo chanzo cha kutoelewa huo ujumbe.

NN Mhango said...

Anon
Shukrani kwa uzi huu wa kizalendo. Ubarikiwe na uendelee kutembelea uga huu.

Anonymous said...

Nasikia kutapika na kichefuchefu
Hali halisi ya Tanzania
Kuanzia serikali , viongozi
Ningekuwa na uwezo ningewashawishi
Wahisani waachie kusaidia Tanzania
Watu wote matapeli, tamaa kuishi maisha ya asana hayalingani na hali halisi
Nalipa kodi ulaya na nchi yangu inasaidia Tanzania naumia sana jinsi wananyoa tumia misaada yetu

NN Mhango said...

Pole sana anon ingawa hiyo nchi yako inachotoa si msaada ukizingatiwa maslahi waliyo nayo na Danganyika ambapo nchi nyingi huiba raslimali nyingi kupitia wachukuaji waitwao wawekezaji na kunufaika mara dufu ya kiduchu na cha kudhalilisha wanachowapa ombaomba wetu wenye kufikiri kwa massaburi.