Wednesday, 19 March 2014

Kijiwe chapendekeza kaya iwe ya kifalme

BAADA ya kushuhudia wanene wakishindana kurithisha vitegemezi vyao maulaji, Kijiwe kimekuja na pendekezo moja la kuwasaidia wasionekane wanafiki na waongo.
Kinapendekeza tubadili katiba na kutangaza kuwa kaya hii ni ya kifalme chini ya ufalme uitwao kurithishana.
Msomi anaingia akiwa na nakala ya gazeti la The Mail on Sunday toka kwa mama a.k.a Ukamerunini ambao wako tayari kuwabania misaada ombaomba wa kimakonde kwa vile eti wamekataa kukameruniana.
Anaamkua na kukaa kwenye angle yake tayari kufanya vitu. Akiwa anakunja mikono ya shati anasema: “Waheshimiwa mmesoma mauzauza ya mfukunyuku na mrejesho wa ufalme kupitia kwenye sanduku la kura?”
Wote wanapigwa butwaa isipokuwa mimi ambaye ni profesa wa kweli wa kila kitu. Hivyo, naamua kuingilia kati: “Msomi umefumba sana bila ulazima. Si useme wazi kuwa unaongelea uteuzi wa Princes Riz Kiquette na Godfreeey Mgiiiimwa kugombea ulaji.”
Msomi anajibu: “Kumradhi jamani. Nina manja na huu uhuni tunaofanyiwa tukazugwa eti ni demokrasia wakati ni ufisadi na ulafi na ufisi.”
Mgosi Machungi ambaye amekuja kula wikendi na wanakijiwe ili arejee Dodoma Jumatatu ijayo anakwanyua mic: “Sisi tinaona titangaze wazi kuwa hii kaya sasa ni ufaume kama Saudia, Kuwait, Swaziland na kwingineko.”
“Umesema vyema mgosi.  Hakuna haja ya kuendelea kugeuzana mabunga kuitisha uchaguzi na kupoteza mabilioni ya njuluku kuhalalisha ufalme uchwara na wa kijambazi na kurithishana maulaji kwa wazito.”
Mpemba aliyekuwa anaweka tasbihi yake kando na kulonga: “Yakhe mie nahisi kichefuchefu wallahi. Hivi hawa watu wana akili au matope? Yaani warithishana ulaji kana kwamba wengine hatuna matumbo!”
Kanji leo karauka kweli kweli. Anakwanyua mic: “Mimi hapana ona baya. Kama toto ya rais nafaa basi chagua yeye. Yaweza tumia zoefu ya baba yake na kuleta endeleo.”
“Go tell it the birds Kanji. Kwani uongozi ni ufalme au unataka kuingiza mfumo wenu wa Kihindi ambapo uongozi unashikiliwa na familia zenye nacho?” Msomi anang’aka.
Kapende hangoji Kanji ajitetee.  Anakula mic: “Kanji hajakosea. Kwao wao wanataka wale wale waliozoea kula nao kwa miaka nenda rudi ili mazabe yao yasifichuke. Zimwi likujualo ati. Unadhani ikiingia serikali ya upinzani mafisadi wengi watanusurika?”
“Mimi haiko fisadi. Hata kama mimi hindi siyo hindi yote fisadi dugu yangu. Mimi sikini kama veve.”
“Kanji unataka kumdanganya nani? Sikini gani anaishi kwenye jumba ya sajili mwaijumba?”
Kama kawaida yake Bi Sofia Lion a.k.a Kanungaembe anaamua kumhami mshirika wake Kanji. Anakatua mic: “Tusipende kuhukumu watu kwa asili yao. Hata wewe ukitaka kuishi kwenye nyumba za msajili unaishi ilmradi uwe na pesa au siyo?”
Mijjinga aliyekuwa akibukua gazeti la The Mail on Sunday anaamua kutia guu. Anasema, “Kumbe Sofi unajipinga. Inakuwaje nyumba ziwe za msajili tena zitake wenye pesa kama si rushwa?”
“Bila rushwa usawa huu unaweza kupata kitu wewe au unaendelea kujidanganya kuwa kuna haki bila pesa? Penye udhia penyeza rupia kaka.”
“Hapo nimekupata,” Anajibu Mijjinga.
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anaingilia, “Umempata wapi Mijjinga hapo?”
Mijjinga anajibu, “Hapo hapo unapotaka.” Kijiwe hakina mbavu jinsi wanavyobadilisha maneno kwa maana ya maanawia.
Msomi amegudua kuwa kijiwe kimeacha mada. Hivyo, anakirejesha kwenye mada. Anabwia tangawizi yake na kudema, “Hebu jamani tuongelee hii aina mpya ya ukoloni ambapo vigogo wanatubambikia watoto wao kwa kuwarithisha ulaji kana kwamba sisi hatuwezi kutawala tena bila kuwala watu kama wao.”
Bi Sofi hakubaliani na madai ya Msomi. Anaamua kumvaa, “Jamani watu wengine hata kama mmesoma sana, msitumie elimu yenu kupotosha umma. Kuteuliwa watoto wawili tu wa wakubwa imekuwa nongwa?”
Msomi anamuuliza Sofi, “Umemaliza bi mkubwa?”
Sofi anatingisha kichwa kukubali kuwa amemaliza.
Msomi anaendelea, “Kwa vile Sofi amenituhumu kutaka kupotosha umma japo ndiye anafanya hivyo, acha nimpe ushahidi aone ukweli wa madai yangu.”
Anamgeukia Sofi na kusema, “Ngoja nikupe orodha ya wateule watoto wa vigogo ili ujue kuwa si hao wawili tu kama unavyodai. Wamo Daktari shaka Hussssein Mwwinyi, Emmmanueeel Nchiiimbii, Januaaaare Makaambaaa, Wars Kawawa, ZayB Kawawa, Violent Mzidikaya, Adaaam Maaalima, Godfreeey Mgiiimwa, Sioiiii Suuumari,”
Kabla ya kuendelea, Mipawa anachomekea, “Msomi tosha umeua mwanangu.”
Huku akitabasamu Msomi anasema, “Akitaka nimpe zaidi nitampa tu.”
Mbwamwitu anachomekea, “Wewe! Umeua.”
Mgosi Machungi anamgeukia Sofi na kuuliza, “Bi Sofi bado unataka zaidi ili akupe dozi nyingine uidhike?”
Mijjinga analalamika, “Jamani imetosha. kwa usawa huu nangoja kupelekwa India kwa presha.”
Msomi anachomekea akitabasamu, “Asipate tabu nitampa tu. Maana wapo wengi ninaowajua kuanzia kwenye balozi zetu ughaibuni Uhamiaji, Mapato au TRA.”
Anakunywa tangawizi yake na kukatua kashata na kuendelea, “Wanene watuzunguka kwa tamaa na upofu wao. Wamejaza watu wao karibu kila mahali kuanzia kwenye siasa kama vile ukuu wa wilaya hadi bandarini, viwanja vya ndege na mipakani kwenye kupitisha bwimbwi, Banki kuu, Hazina ili kuhakikisha njuluku za wazazi wao hawatokei wahuni wakazifanyia kitu mbaya kama wao wanavyowafanyia wachovu.”
 Kapende anachomekea, “Hali hii inatisha na kuchukiza. Si ya kuvumiliwa vinginevyo tujirahisishe kuliwa zaidi.”
Mgosi kashikwa pabaya. Anaamua kula mic, “Huwa sipendi kusema eti tinaliwa. Jamani unatiumiza ukisema hivyo.”
 Mzee Maneno aliyekuwa akinong’ona jambo na mzee Ndomo huku wakimtazama Sofi anachomekea, “Naona kama hali yenyewe hivi basi watangaze ufalme ili tujue. Huu si ulafi.  Ni balaa!”
“Watangaze ufalme mara ngapi?” Haja ya mja kunena muungwana vitendo. Kimsingi, tukubaliane kuwa wamezidi tamaa. Maana waliyokwisha kutuibia nadhani ingewatosha.” Anachomekea Mijjinga anayemaliza kusoma gazeti la The Mail on Sunday.
“Yakhe hawa wala si watu. Hawatoosheki ati. Wala kila kitu wataka watule hata sie wallahi.”
“Hatiliwi. Titawala wao nao waone raha ya kuliwa.  Tena nikitoka japa nakwenda zangu Bumbui kumshughulikia huyo mtoto wa fisadi Januai.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kimechangamka si likapita shangingi la Prince RizOne akiwa na waramba matalio wa baba yake. Wacha tulitoe mkuku kama hatuna akili nzuri!
Chanzo: Tanzania Daima Machi 19, 2014. 

No comments: