The Chant of Savant

Monday 4 May 2015

Katiba pandikizi imeshindwa rejesheni ya rasimu ya wananchi

          Kwa hali ilivyo ni kwamba katiba pandikizi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeshindwa tena vibaya sana. Pamoja na watawala kujifanya hawaoni wala hawasikii na kutaka kutubambika katiba yenye kulinda maslahi yao binafsi huku ikuhujumu umma, uwezekano wa kufanikisha hujuma hii ni mdogo. Kitendo cha hivi karibuni cha Tume ya Uchaguzi (NEC) kushindwa kuendelea na zoezi chafu la kulazimisha kura ya maoni ni ushahidi tosha kuwa mbinu na harakati zao zinaanza kugonga mwamba. Tuombe, waendelee kuumbuka ili warejeshe rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa na wananchi.
Ingawa watawala wamejifanya vichwa ngumu tokana na woga wa kuumbuka kama rasimu ya Katiba Mpya almaarufu kama rasimu ya Wananchi au ya Jaji Joseph Warioba. Watake wasitake kuna siku kweli itadhihiri na wale wote waliofanya uchafu wa kuhujumu taifa wakataka kujificha nyuma ya kinga ya kisheria kwa kuhujumu rasimu mpya wataumbuka. Nadhani kama taifa, tufikie mahali tukubali kuwa kuna maisha baada yetu. Hapa ndipo ulazima na umuhimu wa kuwa na Katiba ya wananchi vinadhihiri.
Japo walitaka kutubambika Katiba yenye kulenga kulinda maslahi uchwara na ya hovyo ya wahalifu wenye madaraka, kuna haja ya watanzania, si kususia tu zoezi hili hata kama watapanga tarehe nyingine muafaka kwa hujuma yao, tunapaswa kuandamana na kupinga zoezi hili linalolenga kutuweka mateka kwenye taifa letu kwa kupitisha sheria inayolinda uovu na uoza. Tuikatae kwa sauti na matendo ili ulimwengu usikie na kujua kuwa tunatambua mbinu zote chafu.
Kama alivyosema mjumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ndugu Joseph Butiku, mambo yote yaliyonyofolewa yarejeshwe tusonge mbele badala ya kupoteza fedha na muda wa watanzania kwa kuleta Katiba pandikizi na ovu kwa taifa ambayo kimsingi haiathiri tu waliopo bali hata vizazi vijavyo. Inashangaza hata busara na uthubutu wa watawala wetu kutaka kuhalalisha haramu na jinai tena kupitia sheria mama ya nchi.
Mzee Butiku alikaririwa hivi karibuni akisema, “Rasimu ya pili ya Katiba iliyotolewa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo mimi nilikuwa mjumbe, ilikuwa imebeba mambo mengi na muhimu ya wananchi ambayo yaliondolewa, hivyo huu ni wakati mwafaka kutafakari kwa kina jinsi ya kuyarudisha.” Haya ndiyo mawazo ya kulipeleka taifa mbele, yasipuuziwe au kusababisha mzee Butiku atumiwe wahuni wa kukodisha kumtisha na kumdhalilisha kama ilivyotokea kwa Jaji Warioba. Huu ndiyo ukweli ambao hauwezi kuuawa japo unaweza kuchelewesha kwa muda.
Mzee Butiku aliongeza, “Kuna wakati najiuliza maswali mengi na sidhani kama nitampata wa kunijibu, ndiyo maana nasisitiza majadiliano. Inakuwaje unaondoa hata kipengele cha kupima uwajibikaji wa wabunge. Wabunge wana nguvu kuliko waliowachagua ndiyo maana hawaonekani majimboni, lakini wananchi kama walivyotaka kuwa wasipomuona mbunge wao wamuondoe, hili nalo linahitaji majadiliano kuliangalia upya.” Hawa wanaotaka tusiwawajibishe wabunge hawalitakii mema taifa na hawafai wala hawapaswi kuachwa waturejeshe kwenye ukoloni hata kama unatendwa na kusimamiwa na watu weusi wenzetu. Ukoloni ni ukoloni hata utendwe na malaika au wazazi wako.
Unapokuwa na wabunge wasioweza kuwajibishwa pia viongozi wakuu wasiohojiwa ujue unarejesha ukoloni mbaya kuliko hata ule wa wazungu. Ni ukale na hujuma visivyopaswa kuvumiliwa hata kwa sekunde moja. Watu wenye uzalendo, ithibati na uthubutu kama mzee Butiku wanapaswa kuungwa mkono ili kulitendea taifa letu haki. Kutendewa haki si hisani wala utashi wa kikundi cha watu bali haki ya watanzania ambayo wanaweza kuinyakua kwa maguvu pale wanaotaka kufanya hivyo wakiendelea na mipango yao michafu. Kimsingi, wahusika wanaogopa bure. Maana, kuna siku watakuwa nje ya madaraka na wenye visheni na uzalendo watachukua nafasi zao na kufumua mfumo mzima wa wizi waliouunda kwa maslahi uchwara na ya muda mfupi.
Kitendo cha kuhujumu mawazo, utashi na maoni ya wananchi ni cha kihaini. Kuengua na kuvuruga Katiba ya wananchi ni kosa ambalo halipaswi kuvumilika. Hatupaswi kuangalia cheo cha mtu au kikundi bali maslahi ya taifa ya sasa na ya vizazi vijavyo. Wakati mwingine woga na upogo vinaweza kuangamiza taifa. Woga wa watawala uwaamshe watanzania wajue kuwa hakuna mtu awezaye kutawala watu bila ridhaa yao. Haya maguvu na mbinu walivyotumia kuhujumu mawazo yetu ni dalili za woga na ushahidi kuwa tukiamua hakuna awezaye kutuzuia. Nani alitegemea watawala wakatili kama Blaise Compaore aliyemsaliti, kumpindua na kumuua rafiki yake angelazimishwa kuyatema madaraka? Nani aliamini kuwa maimla na ving’ang’anizi kama Muamar Gaddafi, Mengistu Mariam, Hosni Mubarak na Zine el Abdine bin Ali wangetimuliwa kama mbwa koko na wengine kuuawa kwa kipigo cha mwizi? Hii ndiyo jeuri ya umma pale unapochoka na kuamua kusema “Imetosha.” Nasi tufikie mahali tuseme kuwa imetosha kuchezewa hasa mustakabali wetu na vizazi vyetu. Asiyeliona hili hapaswi kuvumiliwa wala kubembelezwa bali kushughulikiwa japo aelimishwe na kuuona mwanga.
Kwa vile Katiba pandikizi imeshindwa hata kabla ya kuzaliwa, tufikie mahali tukubaliane na ukweli kwa kurejesha rasimu halali ya wananchi ili tuepuke kupotezeana fedha na muda bila sababu za msingi. Hiyo pesa na muda tunavyopoteza vinaweza kufanya mambo mengine muhimu kwa taifa na vizazi vijavyo. Tufikie mahali tusema kwa pamoja na kwa kunuia kuwa, “Ssasa imetosha’ basi rejesheni katiba yetu ambayo si yetu tu bali ya wote. Walatini husema, “Vox Populi, Vox Dei’ yaani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Basi tumsikilizeni na kumheshimu ‘Mungu’ kabla ya kupambana na hasira zake.
Chanzo: Dira.

2 comments:

Mbele said...

Ndugu Mhango,

Naafiki kila ulichosema kuhusu huu ubabe wa kushinikiza katiba pandikizi.

Ni kosa kubwa na dharau kuondoa
mapendekezo ya wananchi kama iliyofanywa na dawa iliyopo ni kuikataa hii katiba pandikizi.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele,
Shukrani kwa mchango wako. Tuwahimize watu wetu waigomee hii katiba pandikizi.Kwani haina faida kwao zaidi ya kubariki ujambazi na ufisadi wa kimfumo ili waendelee kuwa mateka wa mafisadi, mafisi na majambazi yaliyotamalaki kwenye ofisi za umma yakila kwa miguu na mikono bila kunawa yatakavyo. Tumshinde shetani huyu kwa kugomea kushiriki kiini macho hiki cha kitoto na kishenzi.