The Chant of Savant

Wednesday 30 March 2016

Kijiwe chapanga kutembelea Zenj


            Japo kijiwe hakikushiriki kwenye uangalizi wa uchakachuaji wa marudio kule Zenj–kwa  kutoridhika na jinsi mambo yalivyokwenda ndivyo sivyo–mjumbe wake, alhaj Mpema, alikuwako kule kuangalia si kupiga kula jinsi mambo yalivyokuwa yakienda ili atuletee taarifa ambazo ameziwasilisha leo.
            Baada ya kuamkua huku akiwa anaonyesha wazi kuchukia, Mpemba anakwanyua mic, “Yakhe najua kila mmoja atakajua kiliochotokelezea Zenj hasa kuhusiana na huu uchakachuaji uliomalizika. Taarifa ni kwamba kilichotokelezea kule ni wizi wa kula wa kawaida tokana na wapika kula wengi kutopika.”
            “Unataka kuniambia hizi sherehe za kupongezana na kuapishana ilikuwa ni danganya toto tofauti na ukweli wenyewe? Kama ni hivyo basi rais Joni Kanywaji Makufuli amejichagua kuushiriki ukiachia mbali kula jiwe muda wote ambapo mambo yalikuwa yakifukuta kule Zenj utadhani yeye si rais wake.” Anauliza Mijjinga huku akimkazia macho Mpemba.
            Kabla ya Mpemba kujibu Mgosi Machungi anaamua kumchomekea Mijjinga, “Kwanza yue njomba angu wa madevu yuko wapi mbona hatimsikii akitoa tamko au naye ameamua kukata pua na kuunga wajihi ii apate tena umakamu?”
            Mpemba anajibu, “Kusema ule ukweli wa Mungu kule Pemba hakuna ntu hata mmoja alopiga kula. Kama wapo waliopiga basi ni wale mamluki, mapandikizi au mazombi kama siyo maruhani walozoea kuwatumia hasa kwa kuengeza idadi ya wapiga kura wakati siyo. Hilo la bwana nkubwa kushiriki au kutoshiriki dhulma hii ni juu yake kupima na kuchagua. Hata hivo atajitofautishaje wakati chama chake ndo kinioshikilia usukani kikifanikisha kila jinai huku Zenj? Mie njuavo hapa hakuna haki ilotendeka bali dhulumaa.”
            Kabla ya Mpemba kuendelea, Kapenda anauliza, “Una maana kuwa huyu bwana hakushaini na anatawala upande mmoja kama mwenzie Kanywaji aliyeonyesha kufanya hivyo wakati wa gogoro hili?”
            Kabla ya kujibu Mpemba anatikisa kichwa na kusema, “Yakhe hilo li wazi kuwa huyu jamaa ataendelea kutawala kimabavu kama yule bazazi alojiita Komandoo wakati hakuwa chochote wala lolote. Ukimuona leo huweziamini kuwa huyu ndo alowahi jiita komandoo wakati sasa yu kama kondoo na si komandoo.”
            Baada ya kuona zinaingizwa inshu zisizoendana na mada Msomi Mkatatamaa anaamua kula mic, “Kutokana na taarifa aliyoleta alhaj Mpemba ni kwamba Zenj hakuna aliyeshinda bali kushindishwa. Kama mnakumbuka niliwaambia kuwa huyu wa kushaini atashindishwa hasa baada ya kufuta uchaguzi bila kutoa sababu za kufanya hivyo. Nadhani huko aliko Jechia Dhwalimu Jechia anachekelea kwa kufanikisha ulaji wake. Kitaalamu naweza kusema kuwa mgogoro ambao Nambari Wani wamejidanganya wameuua au kuuepuka ndiyo unaanza. Wataweza kufanikiwa kama watamshawishi Madevu na kumpa ulaji kama walivyofanya mwanzoni pamoja na mkakati huu kuwa na mashaka na matatizo yake. Je wanakaya waliogoma kushiriki uchakachuaji watakubali mtu wao kuwa kitanda kimoja na watesi wao?”
            Mpemba anakula mic tena, “Wallahi nakuaapia. Kama kuna ntu adhani anawezawatumia watu kulinda ulaji wake binafsi aota huyu. Nijuavo mimi ni kwamba wale waliogomea uchakachuaji hawatakubali lolote isipokuwa kusomewa matokeo ya uchaguzi halali wa kwanza uliovurugwa na huyu Jechia Dhwalimu Jechia. Vinginevo hapa hakuna atondanganya yoyote awe ni wa upingaji au wale wanaotula sasa.”
            Kanji aliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kutia guu, “Dugu yangu Pemba kama nasema iko kweli basi iko sida kuba sana Zaainzibaa. Kwanini sasa gagania laji kama vatu ingine hapa kuwa na tumboni ya kula?”
            Kapende anaamua kutoa jibu, “Kwani mafisadi wanaotuhangaisha wawe wa kiuchumi au kisiasa unadhani hawajui kuwa nasi tuna matumbo kama wao? Wanajua ila wanajiona kuwa wao ndio wanaofaa kula na wengine waliwe tu kana kwamba wao si watu. Huyu bwana hana cha kupoteza hata kama wachovu wakiamua kuchenchiana. Mambo yakiwa magumu atatumiwa ndata na ndutu toka Barani na watamlinda kwa kuwaumiza wapingaji kama alivyofanyiwa komandoo na mchezo unaishia pale.”
            Kabla ya Kapende kuendelea Da Sofia Lion aka Kanungaembe anamchomekea, “Mie tangu nigundue kuwa kumbe siasa ni mchezo mchafu hasa baada ya mjomba wangu kubomolewa nyumba yake sina hamu na wanasiasa. Sishangai kuona kinachoendelea Zenj. Iwavyo vyovyote Madevu anaweza kupewa chake kama alivyofanyiwa swahiba yake wa zamani Hamad Rashid Mood akatulia na wachovu wakaendelea kusota kama kawa kwani hii ni mara ya kwanza hii kufanyika?”
            Mipawa anamchomekea Sofi, “Da Safi, sorry, Sofi usemayo ni kweli tupu. Je kulalamika tu kunatosha au lazima tufanye mageuzi lau ili tuweze kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa jamii yote?”
             Kabla ya da Sofi kuendelea Mbwamwitu anachomekea, “Bwana Mipawa si useme tu kuwa kuna kitu unataka kwa Sofi hadi unamwita safi au vipi?”
             Sofi anaamua kujijibia, “Kaka hayo yako. Sisi watu wazima ati. Kama kuna anachotoka kwani kuna ulazima gani wa kuzunguka au kukuogopa wewe? Tunajadili mambo muhimu kwa kaya wewe unaleta utani. Ndiyo maana mnaliwa na hawa mafisadi tokana na kutokuwa serious.”
            Mbwamwitu anaamua kumkaba da Sofi ili amtie adabu kwa kumwambia analiwa.
Kuona hivyo tunaamua kuingilia kati. Tunawaachanisha na kila mmoja anatawanyika!
 chanzo: Tanzania Daima, Machi 30, 2016.

No comments: