Wednesday, 23 March 2016

Kijiwe kupinga amri za Dk Kanywaji


            Amri za rahis Joni Kanywaji Makomeo zimekichefua kijiwe kiasi cha kupanga kwenda kwa pilato kuzipinga. Haiwezekani turejeshewe utawala wa kindavandava wakati twaambiwa sisi ni kaya ya kidemokrasia.
            Mpemba ndiye anaanzisha mada kuhusiana na amri hatari za Dk Kanywaji ambaye Kijiwe kilikuwa kimetokezea kumwaminia. Anachonga, “Jamani mmezisikia hizo amri alozitoa rahis Kanywaji hivi karibuni baada ya kuapisha geshi lake la wakubwa wa mikoa? Wallahi mie zankata kweli kweli.”
            Mgosi Machungi anakatua mic, “Hata mimi simielewi huyu jamaa hasa pae aipoamua kuajiii wageshi wastaafu kuwa wakubwa wa mikoa huku akiwaamuu watiweke ndani hasa sisi tinaoshinda Kijiweni baada ya kukosa ajia.”
            Mipawa anaamua kumchomekea, “Kumbe ulikuwa hujui kuwa huu mchezo wa kuajiri wageshi ni wa zamani tangu zama za mzee Mchonga? Kwa nijuavyo mimi, tumekuwa tukitawaliwa kigeshi kwa mlango wa nyuma. Hivyo, alichofanya Dk Kanywaji ni kuwa muwazi tofauti na waliomtangulia.”
            Msomi Mkatatamaa leo anaingia mapema. Anakwapua mic, “Hii ndiyo hatari na kasoro za kutokuwa na sera za kutawalia. Kimsingi, wanashindwa kitu kidogo yaani kufumua mfumo mfu tuliourithi toka kwa wakoloni na kuufuma upya. Kaya haiwezi kuondokana na matatizo iliyomo kwa nguvu ya zima moto. Ningeshauri waka chini wafanye utafiti na kubaini chanzo cha matatizo yetu ambacho kimsingi si kingine bali kuondokana na maadili ya utumishi wa umma. Wanakula umma wakidai wanautumikia wakati wanautumia.”
            Kabla ya kuendelea Mijjinga anachomekea, “Usemayo Msomi ni kweli. Bila kubadili mfumo wanajisumbua. Hukumsikia Dk Kanywaji akiwaambia wakubwa wake wa mikoa kuwa ndani ya siku 15 wafute majina ya wafanyakazi misukule? Ajabu ya maajabu, wengi tulidhani mojawapo ya maagizo ya rahis yangekuwa kuwakamata wote walioajiri misikule na kujipatia njuluku na kuwasweka lupango then wapelekwe kwa pilato. Lakini jamaa hili halikumhangaisha. Mie naona anatoa maagizo kana kwamba kaya yetu ni shamba lake binafsi.”
            “Yote tisa, mie aliniacha hoi alipowapa ulaji wageshi ndata waliostaafu jana tu. Hakuwapa hata nafasi ya kwenda uraiani wakajifunze jinsi ya kuishi kama wastaafu. Sijui kaya yetu inapelekwa wapi? Unawezaje kuwapa madaraka makubwa watu wasio na uzoefu tena waliostaafu jana kana kwamba kaya haina wachovu wengine wanaoweza kuwatawala wenzao?” anachomekea Kapende huku akibofya kiSumsung Galaxy 6 chake.
            Mheshimiwa Bwege anakatua mic, “Mie hata sishangai. Kinachonishangaza ni ile hali ya kuua muungano kwa kuwagawia watu wake mikoa yao wakajifanyie watakavyo. Hamkumsikia akiwaagiza wafanye maamuzi hata kama ni ya kipuuzi ili warekebishe baadaye badala ya kuogopa kufanya maamuzi? Huu ni nini kama siyo uimla unaorejeshwa kwa mlango wa nyuma kwa kisingizio cha kutatua matatizo ya wachovu? Nadhani, badala ya kuwasaidia wachovu, watawakwaza zaidi. Unawezaje kupiga marufuku vijiwe wakati wenzetu wanakutana Idodomya, wanaitwa wahishimiwa na kupewa mshiko kwa kupiga gumzo mjengoni? Kama ni hivyo basi na spika wa mjengo awa mgeshi. Nani anaongelea kuwashughulikia mafisadi papa kama vile Kagoda, EPA, Escrew au Kiwira? Who wants to fool another here?”
            Mzee Maneno anamchomekea Mheshimiwa Bwege, “Mheshimiwa huna haja ya kulalamika. Hao unaotaka washughulikiwe hawatashughulikiwa. Kinachoendelea hapa ni kutumbua vijipu uchungu huku majipu yenyewe yakiendelea kuzaliana. Unaweza kunieleza ni kwanini–kwa mfano–wadokozi wa bandarini waliswekwa lupango ilhali wale wafanyabiashara wakubwa waliokuwa wakishirikiana nao wakipewa muda wa kurejesha fedha waliyoihujumu kaya? Ama kweli Chama Cha Maulaji (CCM) ni chuo cha sanaa!”
            Kanji hataki kubaki nyuma. Anakatua mic, “Mimi sangaa sana witu nafanya Dokta Kanyaji. Yeye ikosema kuwa geshi takamosha valo vote naharibu amani hasa kwenye koa ya pakani. Kama vatu nakaa kule nakaribisha geni tena jambazi nayokuja na bunduki nategemea nini?”
            “Wallahi Kanji hapa wankata. Wankumbusha yule ngeni aliyepewa ardhi awekeze kule Kagera akaamua lima bange na asiguswa na ntu. Je wako wangapi wanofanya mambo ya hovyo kama haya na waitwa wafanyabiashara tena mashuhuri wakati ni wezi mashuhuri? Je huyu Singasinga wa Escrew ana tofauti gani na wale waniochukua bunduki wakafanya ujambazi unaoleteleza matatizo huko mikoani? Wankamate kwanza ndipo ntajua kuwa wataka sasa fanya kweli vinginevo yote hii danganya toto nawaambia.”
            Da Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kutia timu, “Mie jamaa amenichefua hasa pale alipoamua kuteua warume tu huku akiwatia akina mama kiduchu katika hilo jeshi lake la wakubwa wa mikoa. tunataka uwiano wa kijinsia bwana.”
            Mgosi anarejea, “Mie hakuna aipontisha kama kumpa ungu Makondakta. Napanga kuejea Ushoto ii kuepuka kunyanyaswa na huyu dogo ambaye aiwahi kuwatia ndani wahishimiwa na wafanyakazi wengine wa haimashaui ya Kinondo. Hapa azima titegemee utawaa wa kigeshigeshi, na kindavandava kama siyo uimua.”
            Msomi anarejea, “Hapa lazima tutegemee vurugu zisizo na sababu. Kwa mtu mwenye nia njema na Kaya, alipaswa kuwaasa wasifanye mambo hovyo ili kumfurahisha yeye badala ya wachovu.”
            Akiwa anataka kuendelea mara shumbwengu la Makondakta lilitia breki Kijiweni. Jamaa alishuka na kuanza kutuuliza tunafanya nini kijiweni badala ya kwenda kuchapa mzigo. Acha tumzomee. Kama siyo kuwahi na kujongomea kwenye mchuma wake huenda historia ingekuwa nyininge!
Chanzo: Tanzania Daima, Machi 23, 2016.

No comments: