Friday, 4 March 2016

Mlevi kuwa wakili wa kujitolea kesi za mafisadi

  • Vampire Lawyer Cartoon Stock Photo 95619346 : Shutterstock
            Tokana na baadhi ya wanasheria na wataalamu kutumiwa na mafisadi kama nepi na  kuingia mikataba michafu kama ule wa IpTL na TANISCO, Mlevi, kwa akili zangu timamu, bila kulazimishwa na mtu yeyote wa kitu chochote zaidi ya kanywaji na bangi, nikiwa nimehiari, kwa mapenzi na uwezo wangu, bila kutegemea kupata faida yoyote wala kusababisha hasara yoyote, kwa mapenzi kwa taaluma na taifa, kwa kutambua udhaifu na mianya iliyopo kwenye mfumo wetu mfu, napanga kuomba kuwa wakili wa asiyelipwa chochote wa serikali kwenye kesi za mafisadi hasa ile ya Escrew.  Zifuatazo ni sababu zilizonisukuma kupanga kuwa wakili wa ubwete au kwa kisheria tunaita pro bono:
            Mosi, kama nilivyodokeza hapo juu ni nguvu ya bangi na kanywaji vinavyonipa ujasiri ukiachia mbali hasira za kutaka kunyotoa majizi roho. Unadhani nikikutana na mijambazi ya Escrew–iwe ni barabarani au kwenye magazeti–nafurahi? Kwanini nisitumie stimu zangu kuwatia adabu hawa kama kweli serikali ya dokta Kanywaji imepania kuwashikisha adabu gendaeka hawa majambazi.
            Pili, ni ujuzi wangu wa sheria. Kwa wasionijua vizuri, mimi si mtaalamu wa sheria tu bali mwalimu wa sheria kwa ngazi ya univesiti ya chuo kikuu. Japo wengi hawajui, Mlevi ni bobezi la sheria kiasi cha kutumiwa na umoja wa mataifa kutoa ushauri mbali mbali kwenye migogoro dunianio. Ila huwa nafanya hii siri. Hivyo, utakaposoma naomba ufanye siri ili watu wasianze kuniogopa nakuabudia bure kama ninavyoona wengi wakimfanyia Dokta Kanywaji kama yule mtoto wa Kigogo aliyelelewa na serikali iliyopita tokana na jina la mgosi baba yake kuitupia madogo serikali hiyo hiyo iliyomuangua kama kifaranga cha kuku. Naamini hapa rafiki Jan Makambale amepata salamu au vipi?
            Tatu, nimepanga niwe wakili wa kujitolea hasa baada ya kugundua kuwa kama tutawaachia vibaka wanaoweza kusaliti na kuuza taaluma zao, majambazi na mafisadi yanaweza kuwapa chochote kitu yakaishia kushinda kesi na kutaka serikali iyalipe fidia badala ya kuyarambisha shaba au kuyatundika kitanzini kama Sir Damu Hussein au kuruhusu walevi wayasulubu kama Mwamali Gaddafi.
            Nne, nataka niwe wakili wa kujitolea ili kuwanyima ulaji wanasheria mbwa mwitu wanaotumiwa na mafisadi kama diaper au tampon. Naona yule anatikisa kichwa akidhani natukana. Kwani hii mikataba ambayo mzee wa kutumbua majipu ameshindwa kugusa au kuongelea unadhani waliingia akina nani? Unadhani akina Singasinga na Jimmy Rugemalayer ni wasomi wa sheria?
            Tano, nataka kuwaonyesha wachumia tumbo na walaramba makalio kuwa kuna maisha hata bila ufisadi au kuramba makalio ya mafisadi au kufanya kile watasha huita to do their dirty laundries. Kwanini kuuza nchi yetu nasi tukajiuza wenyewe? Huoni akina mzee wa Vijisenti wanavyotembea vichwa chini pamoja na kunyimwa aibu na kujisuta?
            Sita, nataka kumsaidia dokta Kanywaji kuhakikisha mkakati wake wa kusafisha kaya unafanikiwa. Pia, nikimalizana na mafisadi wa nje ya chama, lazima niombe kuwasulubu wale wa chamani kama yule kigogo mwenye kampuni inayotuhumiwa kufanya hujuma bandarini ukiachia kutuhumiwa kusafirisha nyara za serikali hasa pembe za ndovu. Huyu lazima nimtumbue jipu mahakamani. Nikimalizana naye nafufua kesi za UdA, Kagoda, Meremeta, Mwananchi Gold, RITES, NBC,SUKITA, EPA, Richmonduli, Dowans na nyingine nyingi zinazowahusu vigogo waliotangulia. Loo! Nilitaka kusahau kashfa ya Kiwila ya Ben Tunituni Makapi ambaye naye–kama Njaa Kaya–siku hizi amegeuka kiguu na njia kwenda Ikuu kuomba asitumbuliwe. Kwa taarifa yenu Ben na Njaa Kaya kaeni mkao wa kuliwa. Lazima mlevi niwatumbue wima wima na chap chap bila huruma wala kulindana au vipi? Loo! Nshasahau Loliondo ya mzee Ruxa na Muhunidini Ndorangara! Lazima nifanye kweli ili mafisadi wanaopanga kuanza kuliibia taifa washike adabu na adabu iwashike. Ukitaka kumukong’ota nyani usimwangalie usoni.
            Saba, nataka kuwa wakili na rafiki wa mahakama ambaye kitaalamu huitwa amicus curiae ili kuhakikisha nakomesha kitu hii once and for all. Fursa hii itanisaidia kuweza hata kutumia ushahidi wa mashahidi wangu kuwamaliza mafisadi.
            Nane, nataka kumwonyesha Dokta Kanywaji na Wabongo wote kuwa bado kuna watu wenye uzalendo ukiachia mbali kuwaonyesha kuwa hata walevi si wa kudharau au kupuuza.
            Tisa, nataka kuhakikisha naacha historia au precedent kwa lugha ya kipilato ambayo majaji wajao miaka mingi ijayo watatumia kuwakaanga mafisadi. Najua wachovi wengi hawajui kuwa tuko wazalendo kibao tena wenye uwezo, sababu, nia na uwezo wa kukomesha ufisadi nchini.
            Kwa ndugu zangu mawakili waliozoea kupata mshiko kwa kuuza ujuzi na kusaliti taaluma naomba mnisamehe kwa kutia kitumbua chenu mchanga. Tufikie mahali tufikirie kama jamii ya watu na si kila fisi binafsi hadi tukatumiwa kama nepi za mafisadi kusafishia uchafu wao. Makosa ya serikali iliyopita iliyofanya yanatosha. Tubadilike.
Chanzo: Nipashe, March 5, 2016.

No comments: