The Chant of Savant

Tuesday 1 March 2016

Kijiwe chataka Kiquette ajitumbue kwanza


            









Kijiwe kilishangaa kiasi cha kukutana kama kamati ili kudurusu mantiki ya Mkiti wa Chama Cha Maulaji (CCM) kudai kuwa atawatumbua wanafiki ndani ya genge lake twawala. Wanakijiwe wameshangaa si kawaida kwa hatua hii ambayo kimsingi hasa ikizingatiwa kuwa jamaa alishindwa kuwavua magamba wenzake kutokana na kambale wote kuwa na sharubu.
            Kapende ndiye analianzisha baada ya kupiga chafya mara mbili, “Wazee mmesikia Sanaa mpya za rafiki yetu Njaa Kaya aliyedai eti atawatumbua majipu wasaliti chamani?”
            “Nawe umemwamini wakati ukijua fani yake siyo?” anauliza Mbwamwitu huku akibofya kisumsung  chake.
            Mipawa anajibu huku akimwekea muuza kahawa amuongezee kahawa, “What? Nani amtumbue nani na vipi wakati sioni tofauti yao kwenye ulaji huu wa kula kwa miguu na mikono tena bila kuosha mikono?”
            Mgosi Machungi anajibu, “Usemayo ni kwei tupu. Huyu jamaa kwa oodha hana mfano. Aisema ana oodha za wauza bwimbwi, majambazi na mafisadi akini hakuchukua hatua. Leo anakuja na ngonjea nyingine eti ana oodha ya waiosaiti chama kwenye uchaguzi uiopita. Sisi tiishamzoea.”
            “Yakhe hapa unsema kweli wallahi. Huyu bingwa wa sanaa tena za kichovu sana. Hawa ndiyo Ben Tunituni Makapi alisema wana uvivu wa kufikiri kama yeye. Kama alishindwa kuwashughulikia mafisadi na wauza bwimbwi tena wakati ule akiwa na rungu la urais leo amdanganya nani? Huyu bwana kweli kiumbe wa ajabu. Alishindwa magamba yalohitaji nyundo na shoka ataweza utumbuaji majipu uniohitaji utaalamu na ujasiri mkubwa sana?” Mpemba anajibu.
            Mchunguliaji anakula mic, “Kaka umesahau alivyodai alikuwa na orodha za majangili papa 40 akawafuga hadi juzi juzi wakamtungua mtasha wa watu tokana na uzembe wa huyu msanii? Tena unakimbusha magamba manene kama yule mzee wa Vijisenti aliyemtishia jamaa nyau naya akatishika na kuufyata alipomwambia kama ataka kuvua gambale basi awe na shoka.”
            Mipawa anakamua mic, “Nadhani hakuna jipu, sorry, busha linalopaswa kupasuliwa kama yule aliyelea haya majibu yanayomsumbua rahis Kanywaji kwa sasa. Heri wangetumbua majipu kweli badala ya kuhangaishwa na vipele! Nadhani kama majipu ni kero basi CCM ini busha linalopaswa kupasuliwa na si kutumbuliwa. Je dokta Kanywaji ana ubavu wa kupasua jibu au udaktari wake ni wa kumbua majipu na vipele tu? Ni ajabu gendaeka aliyeisaliti kaya anahangaishwa na wenzake waliosaliti genge. Kumbe kwake genge lake la ulaji ni bora kuliko kaya? Huyu naye ni busha tena linalonuka.”
            Msomi Mkatatamaa anaamua kula mic, “Nimependa analogy yako ya busha. Ni kweli kuwa hii kitu ni busha tena kubwa kuliko yote tuliyowahi kuyaona hasa ukizingatiwa kuwa majipu na vipele vinavyomhangaisha rahis Kanywaji vimeota juu ya busha kubwa tu la muda mrefu. Huwezi ukatumbua majipu kayani bila kuigusa CCM kwa namna moja au nyingine. Kwani wengi walioibia na kuhujumu kaya walijificha nyuma ya ufadhili wa busha lenyewe ili waendelee kuneemeka huku wachovu wakipigika. Wakati yote hayo yakitendeka, huyu msanii anayetusanifu atawashughulikia wenzake alikuwa akichekacheka hadi mzee Mpayukaji akamwita Chekacheka awezaye kucheka hata kwenye msiba.”
            Anageuka na kuniangalia. Nami natabasamu kwa ujiko alinipa. Niliogopa kucheka nisiitwe Chekacheka. I am a serious dude.
            Mpemba anarejea, “Mie wallahi naona kama kuna jipu lapaswa tumbuliwa si jingine bali yule Jechia alohujumu uchaguzi wa Visiwa. Huyu bwana naweza sema wazi kuwa si jipu bali busha wallahi. Ajabu waniosema wataka tumbua majipu washangaza sana kukaa kimya wakati haki haijatendekeza Zenj.”
            Kanji naye anaamua kula mic, “Nyinyi taka busa tumbua jipu. Veve zani pasua busha iko chezo? Busa iko uuma sana na iko kuba sana. Yeye natumbua jipu na pele kwa sababu iko dogo sana.”
            Mheshimiwa Bwege anakamua mic, “Ami wataka Jechia atumbuliwe nini wakati alitimiza maelekezo na maelezo ya wakubwa waliobwagwa kule Zenj? Huoni anavyoengwa engwa kwa kuwakoa jamaa? Ajabu ya maajabu amepewa fursa nyingine kusimamia uchakachuaji ambapo–naamini atavurunda kuliko wakati wowote–kiasi cha kuadhirika kama siyo kupatikana. Nyie ngoja. Wachovu wamechoka kuchezewa mahepe. Na wakiendelea na upuuzi wao, kinaweza kunuka tukaanza kulaumiana.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic, “Hata nami sikubaliani na kilichofanyika Zenj. Hii ni dhuluma ya wazi hasa wakati huu tunapoaminishwa kuwa demokrasia inaanza kuota miziz kayani wakati akina Jechia na wahuni wenzake wanang’ao hiyo mizizi.”
            “Naona dada zoezi la kubomoa mijengo ya mabondeni limekubadili kabisa kisiasa. Maana zamani tukikueleza hawa jamaa hawafai ulituona kama vile hamnazo.”
            Sofi anajibu, “Ya kale kaka hayanuki. Na lipatalo hupishwa.”
            Mheshimiwa Bwege anachomekea, “Mengine hayapishiki hasa yanapohusisha kuibia jamii.”
            Kijiwe kikiwa kinachanganya si lakapita shangingi la Njaa Kaya, wacha tulisindikize kwa kuzomea!
Chanzo: Tanzania Daima, March 2, 2016.

No comments: