How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Wednesday, 26 January 2011
Dowanis ikilipwa najichoma moto
Baada ya kumaliza mazishi na maombolezo ya mashujaa wa Arusha, nilivuka mpaka na kuingia Kenya tayari kupanda ndege kuelekea Tunis kuhudhuria mazishi ya shujaa mwingine na wengine waliouawa na vibaka wenye sare baadaye.
Msiba huu ulikuwa ni wa rafiki yangu mwanafunzi wangu na mwanamapinduzi Mohammed Bouazizi ambaye baada ya kumaliza chuo kikuu na kukosa kazi aliamua kubangaiza kwa kuuza matunda na kahawa kijiweni kwake.
Serikali ilipoingilia biashara yake, Bouazizi aliamua kujichoma moto na kufariki baadaye huku akiacha ameuchoma mshale utawala wa dikteta Zine al-Abidine Ben Ali. Jamaa huyu ambaye tulikutana alipokuwa mlinzi wa hayati Habib Bourguiba alijigeuza Mungu akitawala kwa kutumia familia yake na walamba viatu.
Alijisahau. Aliiba pesa ya umma kama hana akili mbaya. Aliamuru kuuawa kwa waandamanaji walioandamana kuomboleza kifo cha Bouazizi huku wakipinga hali mbaya ya maisha. Walipinga ufisadi, matumizi mabaya ya vyombo vya dola, matumizi mabaya ya njuluku za umma, uwekezaji mbovu, kujuana, usanii na upuuzi mwingine uliofanya maisha yao yakose maana.
Hakuna mtu aliyekuwa mwizi na kuchukiwa kuliko hata Ben Ali kama mkewe kikwapuzi Leila Ben Ali (binti Trabelsi) ambaye watunisia walizoea kumwita Imelda Marcos wa ulimwengu wa kiarabu. Mama huyu habithi, kwa habari nilizopata mitaani Tunis ni kwamba ametoroka na vito vyenye thamani ya dola za kimarekani 35,000,000.
Alipataje ukwasi huu? Aliupata baada ya kumlisha limbwata rais na kumtawala yeye na ukoo wake. Kwa ufupi ni kwamba alimgeuza rais bwege na kifaa cha kujitajirisha yeye na ukoo wake bila kusahau mashoga zake.
Hasira za watunisia kwa mama huyu ungeziona kwa jinsi walivyochoma mahekalu yake na kaka yake bila kusahau kukojolea picha zao wakiapiza siku wakiwapata kuwavua nguo na kuwaamuru wanajisiane. Haya si maneno yangu. Ni maneno ya waarabu hawa wenye miili midogo lakini yenye mioyo mikubwa.
Mama alikuwa mshenzi sina hamu. Unajua kuwa baada ya kuwa mhudumu wa saluni halafu akaolewa na Ben Ali alihakikisha ndugu zake wote 10 wanatajirika kupitia mgongoni mwa shemeji yao bwege kama ilivyokuwa kwa Anna Tamaa Tunituni na sasa Shari si Salama Njaa Kaya na genge lake la majambawazi watumiao ushemeji na udugu wa jamaa kutumalizia kaya?
Ukoo huu wa mapanya watu walao kwa miguu na mikono tena bila kunawa na wakinya kama mainzi, ulikuwa ukimilki karibu kila kitu kuanzia internet café, uuzaji wa magari, hisa kwenye mabenki, shirika la ndege la taifa la biashara ya mihadarati? Je Leila habithi huyu unakupa picha gani kuhusiana na kaya yako?
Pamoja na ukuu wangu wa kijiwe msijemuingiza hani wangu mshirika wa bedroom nikanyotoa mtu roho kabla ya kujimwagia petroli na kuiaga dunia kama Dowanis watalipwa njuluku za walevi kutokana na kusababisha kiza na kupanda kwa gharama za mameme.
Nilijifunza kitu kimoja kikuu. Yale yaliyofanyika AR yangefanyika Tunisia mbona jamaa na Imelda wake na Riz-one wangekuwa historia? Mbona Kagoda Rostitamu na washenzi wenzake wangeishanyotolewa roho kama siyo kutoroka?
Siku hizi tumegundua njia nyingine ya kujikomboa na kuondoa uonevu na ufisadi.
Mbinu hii mpya ya ukombozi inalenga kutoa ujumbe kuwa hawa wanaotunyanyasa wajiulize. Kama twaweza kujichoma wenyewe, tukiwapata wao tutawafanya nini?
Turejee Tunisia. Siku benki ya Zeituona iliyokuwa ikimilkiwa na mmoja wa kaka zake Leila ilipochomwa na waandamanaji si nikaenda lau niondoke na madolari. We acha tu. Ufahari na kiburi chote cha familia hii habithi kilitoweka ndani ya dakika chake baada ya kijana asiye na kazi kuwasha moto ulioangusha vigogo. Nani alijua kuwa muuza nyanya, kahawa na mboga mboga angeweza kumuangusha rais tena aliyejiona mungu mtu? Sasa imetokea wenye akili na mikakati tieni akili. Hata wale gendaeka wanaojiona miungu watu kwa sababu ya madaraka waliyopewa na umma wakae mkao wa kuliwa.
Nani angeamini kuwa ofisi za chama tawala cha Rassemblement Constitutionel Démocratique (RCD) au Kusanyiko la Kikatiba na Demokrasia kwa kimakonde zingevamiwa na kubomolewa huku alama zake zote zikiangusha mchana kutwa? Wenye tabia ya kujiona kuwa watatawala milele nao wakae mkao wa kuliwa.
Kwangu RCD ni Ruling Corrupt Devils. Genge hili la mibaka halikuwa na demokrasia ya maana zaidi ya demokrasia ya kifisadi ambapo fisadi mkubwa huwaruhusu mafisadi wenzake, wake zake, watoto zao hata mbwa wake kuibia taifa bila kushughulikiwa. Na huwezi kuamini. RCD ilikuwa ikihubiri amani na mshikamano na kutishia watu walipoanza kuhoji ugumu wa maisha ilhali genge la majambazi na mibaka yenye madaraka na hata mbwa wao walikuwa wakineemeka tena bila kufanya kazi.
Nakumbuka mpumbavu mmoja changudoa msemaji wa rais aliyefurushwa aliwakejeli wananchi kwa lugha za mitaani kama shangingi wa kihaya afanyavyo kayani. Yuko wapi? Ameikimbia Tunisia kwa mtumbwi baada kibanda chake kupiga nari.
Huu ni ufunuo kwa wadanganyika na wadhulumiwa wote barani kuwa siku moja kama mtaamua kuacha ukondoo mtajikomboa na kuwa huru kabisa kama watunisia waliomtunishia misuli mwizi mkuu aitwaye rahisi wa ufisadi akatimka na mbweha wenzake.
Nilipokuwa nikishangaa wenzetu wanavyojijua baada ya kufanya mapinduzi ya kifikra na kimkakati, nchi nyingine zililipuka. Kule Misri jamaa mmoja ambaye tuliwahi kuwasiliana kwa mtandao aitwaye Mohcin Bouterfif alijitia nari akitaka wamisri waamke na kumkabili farao wao Hosn Mohamed Mubarak. Nchini Mauritania mke wa shujaa Yacoub Ould Dahoud alinitumia email kuwa mumewe alikuwa naye kajitia nari. Baada ya kuona wanakijiwe wenzangu wa nchi zilizoachana na ukondoo wanajitia nari, name napanga kujitia nari kama Dowanis italipwa njuluku za walevi wachovu. Nitakwenda mbele ya jumba jeupe lililojaa uoza na kujitia nari. Naona na UVsisiemu nao wameanza kushtukia dili za madingi wao!
Wache niende kununua kibiriti niwachome kabla ya kujichoma. Ngoja nijiimbie wimbo wa Sipho Makhabane aliowaimbia makaburu.
Zawelale indonga. Indonga zawelale. Ngome zimeanguka na ngome zitaangushwa. Tuimbe sote. Ngome zitaangushwa na walioko nyuma yake wataanguka na kuaibika. Indoga zawelale indonga zawelalelale.
Ziangushwe ngome ngome za ufisadi ngome za Dowanis ngome za Kagoda ngome za Njaa Kaya ngome za Ewassa ngome za za za. Nasikia harufu ya EPA harufu ya Dowanis na Njaaa Kaa na Kiama cha Mafisadi.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 26, 2011.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment