Saturday, 22 January 2011

Nawalilia mashujaa wetu Arusha
MWENZENU juzi nililia kama kichanga kutokana na uchungu na nyomi ya watu iliyoujaza mji wa AR. Nilikuwa kule kuwaaga mashujaa waliouawa wakipingana na kupigana na ufisadi.

Hawa ni mashujaa wa kweli dhidi ya ufisadi. Siyo sawa na wale mashujaa njaa waliopewa vipande vya vyeo wakasaliti mapambano na kuwa sehemu ya maadui. Sam Six na Mwakiwembe mnanipata?

Nasikia mkipiga kelele na kuangusha machozi ya mamba eti Dowanis isilipwe. Kama kweli mnamaanisha kufanya kweli, jitoeni huko mje huku na kujiunga na makamanda na mashujaa wa kweli wakiongozwa na Daktari Slaa.

Kwa ufupi, ni kwamba tuliwaaga kwa heshima zote mashujaa waliouawa na majambawazi wenye sare. Niliona wale majambawazi wa sare wakitumbuatumbua mimacho kwa aibu kama panya aliyenaswa kwenye mtego.

Tuliwazomea na kuwasomea ili wajue jinsi wanavyotumika kama nepi kuzoa uchafu wa wakubwa fisidi waliowaamuru kuua mashujaa wetu.

Juzi nilifurahi niliposikia lisirikali likiwakana hawa jamaa zangu kusema eti walikurupuka. Kwa wenye akili, hili zaidi ya kuwa suto, ni somo kuwa waache kujirahisi na kutumiwa kama mbwa au vifaa vya mafisadi hawa.

Huwa najiuliza kama hawa jamaa wana ubongo na kama wanao kama una akili au matope. Maana yenyewe yakiamriwa, hata bila kutumia busara yanaangamiza yasijue waathirika ni ndugu, mama zao, dada zao hata wenzao!

Hivi haya yakistaafu yatakuwa nani kama si raia wa kawaida? Kuna haja ya kuyafundisha haya majamaa kutumia akili badala ya matumbo.

Najua Njagu mkuu Saidia Wema anapresha kwa sasa kutokana na kutakiwa aachie ngazi yeye na bosi wake Chemsha Vurumai Nahodhi. Mie nshawasiliana na madevu Mureno Ocampoe kuja kufanya vitu vyake dhidi ya kikundi hiki cha magaidi kayani.

Hata leo nasema tena bila kufumba. Kitoeni wahalifu nyie hata kama mna vyeo vikubwa.

Sasa nasema tena kwa kinywa kipana na herufi kubwa Njaa Kaya na wauaji wenzako kaa mkao wa kula. Tutaandamana hadi kieleweke. Tumechoka na usanii, ufisadi, uchakachuaji wa kila kitu na upuuzi mwingine.

Hatutishwi na tutaandamana hadi kuku, kenge, fisi, mijusi na wanyama wengine watuunge mkono kama hawa wanaopaswa kutusikia wamejigeuza hayawani.

Tutapinga ufisadi kuanzia Dowanis hadi HEPA. Tutaliandama liserikali na mafisadi wake hadi kieleweke.

Kaya nzima lazima iamshwe kabla hawa majambawazi hawajatuuza na roho zetu.

Wameuza madini, mashamba, ardhi, mbuga za wanyama. Hawajatosheka wanatuuzia hata giza na ukame! Wanatuuzia matusi kiasi cha kutuua tunapowapa ukweli.

Wanatumia kodi ya walevi kuwaua na kuwadhalilisha! Hivi hawa wana roho kweli? Wana akili kweli hawa? Hivi hawajui kuwa maulaji yana mwisho na mwisho wake huwa mbaya hasa kwa wale waliokula bila kunawa tena kwa miguu na mikono kama wanavyofanya sasa?

Hapa najua wataajiri machangudoa wa kimaadili kama yule shangingi wa kihaya kutukana watu ili kutetea mabwana zao.

Juzi nilimpaka hadi akalalamika. Alijua mie gari kubwa. Angejitia kujibu ningemuumbua kuanzia afya yake hadi nyumbani kwake. Hayo tuyaache yana siku na mahali pake.

Sasa natangaza mafisadi na mbwa wao wanaotumika kuua na kuonea walevi wajue na kujiandaa. Wamelikoroga. Tutaandamana hadi kwa jamaa wa nyayo ambao nao walipoteza ndugu yao aliyekuwa amebatizwa na majambazi kuwa Mkurya wakati ni Mgikuyu wasikie.

Si mlizoea kuwaita manyang’au wakati manyang’au ni nyinyi wenyewe. Tutawaandama mafisadi hadi wajue hii kaya ni yetu si yao.

Jamaa hawa waajabu kweli. Wanaomba msamaha mabalozi badala ya sisi utadhani waliouawa ni mabalozi na si wadanganyika! Baada ya kushtuka kuwa wamefanya makosa mengine, eti wanakanusha kwa kutishia kufunga magazeti ya umbea.

Sumu ishasambaa kuwa mlikurupuka kama mbwa wenu na kuomba msamaha mabalozi badala ya walevi. Huu nao ni ulevi wa madaraka na matumizi mabaya yake.

Mtashitaki wangapi? Bwana Ben Mende nadhani ananipata. Utashitaki wangapi ndugu yangu? Thubutu.

Umma wa walevi lazima uelimishwe kuhusiana na hawa magaidi wa kayani. Hata wakiomba misamaha mia tena uchi bado ni mafisadi na wauaji wanaopaswa kuteketezwa kabla hawajaiteketeza kaya.

Wasivyo na bongo eti wanaamua kuua kwa vile waliambiwa ukweli. Kama wasingekuwa mafisadi si wangekanusha badala ya kunyotoa roho za wachovu wasio na hatia?

Hivi waliouawa wangekuwa watoto au jamaa zao wangefanyaje? Wakijibu swali hili watapata jibu la wanachopaswa kufanya kuhusiana na familia za marehemu mashujaa wetu.

Kwanza, wangewalipa fidia wathirika wote. Pili, wangehakikisha ujambazi huu haufanyiki tena. Tatu, wangeanza kuwaandama hata kuwaua mafisadi badala ya wanaowaambia ukweli. Nne, waliotoa amri waachie ngazi na kupelekwa Segerea au wapigwe mawe kama vibaka. Tano, walaaniwe. Sita, walipaswa kutubu na kuomba msamaha walevi.

Saba, walipaswa kuachana na malipo kwa Dowanis. Nane, wawataje wamilki halisi wa Dowanis hata kama wakubwa wenyewe. Yote tisa lamia waache mgao wa kiza tena wa kulangua.

Kwa vile walevi wangi wanataka kujua Dowanis ni nani na mali ya nani, na wenzao hawataki kujitaja, mie nitawataja.

Nina sababu nzuri tu ya kuwataja. Kama wahusika wasingekuwa wadowans wenyewe si wangetaja majina ya wamilki wa Dowanis badala ya kuja na majina ya wamachinga wa Kizungu kama walivyofanya.

Wanadhani hatujui kuwa hawa wanaowataja ni vidampa wao wa kawaida hata kama ni Wazungu?

Sasa natoboa. Dowans ni Rostitamu, Ewassa, Endelea Chenga na Ziro Kadamage na wengine ambao wasomaji nanyi malizieni kutaja.

Kijiwe cha leo ni kwa heshima na kumbukumbu ya mashujaa waliouawa wakipambana na ufisadi. Walaaniwe mafisadi wote. Walaaniwe wauaji wote. Wote washindwe na walegee. Aaaamina.

Naona Andengenyeke anakuja na vibaka wenzake wacha nikitoe nisije nkauawa bure. Ngoja niwafundishe kukimbia!

Chanzo: Tanzania Daima Januari 19, 2011.

No comments: