How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 6 January 2011

Hatuna tofauti na mende waishio gizani


JUZI nilisikia baadhi ya viherehere na hamnazo wakilalamika kuwa mgawo wa umeme uliokumba kaya ni kitu mbaya! Tena wanasema eti tuandamane kupinga kupanda kwa bei za umeme! Wapumbavu sana tena wa mwisho.

Hawajui mgawo na kupanda bei ya umeme vinakuza uchumi kwa kuongeza raslimali watu kutokana na kupatikana fursa safi ya kutengeneza vitegemezi? Mie mwaka huu, mpaka mgawo uishe, si haba, naweza kutengeza lau vitano.

Maskini hawajui mgawo unapunguza kutumia sana umeme kiasi cha kukausha mito yetu izalishayo mvua kwa ajili ya wakulima! Hawajui maji yakipungua wanyama kama vile mamba na samaki wanaathirika, jambo ambalo si zuri kwa ecosystem ya dunia?

Kuna ubaya gani kuzaliana hasa wakati huu wa mgawo? We fyatua kama huna akili nzuri. Watasoma vipi au kupata wapi matunzo safi usiniulize. Kila mtu anakuja na riziki yake ati. Isitoshe, riziki ya mchovu si kubwa kiasi cha kuhangaisha vichwa. Ukipata khanga kwa ajili ya mama wakati wa uchaguzi, fulana na ofa mambo yananyooka na neema ndiyo hizo hata kama za msimu.

Mambo ya watasoma vipi yasiwahangaishe hasa ikichukuliwa kuwa hawatakwenda kusoma Ulaya kwenye elimu ghali na feki inayopendwa na malaya.

Watasoma hapa hapa hata kama ni kwa kukaa juu ya mawe kama nyani. Huu ndiyo uzalendo uliotukuka. Nani mpumbavu apeleke watoto wake Ulaya kwa wakoloni kama malaya?

Kukaa chini si ajabu wala hawatakuwa wa kwanza. Mbona nyani wanakaa juu ya mawe na wanafundisha watoto wao unyani na wanafanikiwa? Kwani kuna kosa kujaribu maisha ya wajomba zetu wa karibu yaani nyani? Kwani sisi na nyani kwa sasa tuna tofauti gani iwapo hata nyani ni bora kuliko sisi kutokana na ukweli kuwa hawachakachuani wala kugeuzana majuha zaidi ya kuheshimiana?

Nyani hawana vibaka wala mafisadi. Hawana wasanii wala wabangaizaji. Nyani ni nyani wala hawatamani kuwa viumbe hovyo kama binadamu japo binadamu sasa anatamani na kufanya kama nyani asifanikiwe.

Nani kawadanganya kuwa giza ni baya? Kama muda wote ungekuwapo mwanga tungelala lini? Kutokuwapo umeme kunanifanya nitononoe usingizi kwa sana. Hakuna mikelele ya ibada za mabaa, vibanda na vigari vya kuuza kanda, mihadhara na upuuzi mwingine.

Na isitoshe, kuja kwa mgao kumeleta muziki wa kizazi kipya ambapo kaya yetu ni ya kwanza kwa teknolojia hii ya kutumia majenereta kutumbuiza. Napenda sauti nyororo ya tutututu za majenereta ukiachia mbali wawekezaji wanaoingiza majenereta kupata soko na kulipa kodi ya haja kwa serikali.

Hata wawekezaji maalum kama Dowans watatengeneza mabilioni kwa kuwezesha kuwepo giza tunachohitaji.

Ukisikia maendeleo katika karne ya 21 ndiyo hayo. Isifiwe sirikali kwa kuwezesha hili. Pia mgawo unaleta usawa baina ya wenye nyumba na wapangaji. Nashukuru Mungu vishoka watakula mafi yao.

Mie napingana vikali na viherehere wanaotaka watu waingie mitaani kudai upuuzi uitwao umeme. Kwanza, nani anataka umeme usawa huu wakati umeme wenyewe nasikia kumbe maana yake ni ukimwi? Nani anataka ukimwi kwa hiari yake hata kama ukimwi wenyewe ni wa kisiasa kama uchakachuaji?

Kuna tatizo gani walevi kunyimwa...sorry.... kukosa umeme wakati ndicho walichochagua? Hivi walitegemea nini waliporidhia uchakachuaji na kuushangilia ili wasivuruge amani ya kijiwe? Hawa viherehere hawajui kuwa imani ya amani ina gharama! Wapuuzi sana. Kwanza, watu walishaambiwa 'raha jipe mwenyewe'. Wakakubali kujipa raha wenyewe.

Sasa wanamdai nani umeme iwapo raha ni kujipa mwenyewe? Dowans wanajipa raha. Sirikali wanajipa raha. Hata mafisidunia wanapata raha ingawa wao wanapewa na lisirikali. Kwa vile lao moja na wao ni wamoja tunaweza kusema: wanajipa raha wenyewe.

Wapuuzi hawa wanaodai umeme wasisikilizwe. Nashauri wanyongwe au wauawe kwa kupigwa mawe na maiti zao kuburuzwa mitaani ili liwe somo kwa wengine. Eti wanasema watu waingie mitaani kuhakikisha kinaeleweka! Lol! Angalia kilivyoumana pale Ivory Coast. Hawa ndiyo watu wenye akili ¦...sorry wasio na akili...... achia mbali misukule na mafisadi wenu.

Kwa sasa hatuwezi kumlaumu Mungu wala serikali bali walevi wetu ambao wengi ni kama kondoo waliochanganyikana na mafisi halafu wakaaminiana kondoo wasijue ni kiama chao!

Kwa vile walichagua giza, basi tusiwalazimishe kutaka mwanga. Kwa vile walikula chao mapema kupitia takrima na upuuzi mwingine, acha na mafisadi wachukue chao mapema kwa kulipana kupitia Dowanis. Pia wanataka atajwe mwenye Dowans! Kwani hawamjui au woga tu wa kumtaja?

Kuna ubaya gani shamba la bibi kuchumwa hata na mabwege? Hivi mlitegemea nini msanii anapoaminiwa na wapwakia udoho udoho? Hivi unategemea nini mwizi anapoaminiwa fweza? Mambo ya mchawi mpe mtoto alee yalishapitwa na wakati. Siku hizi ukimwachia mwana anamramba nawe unabaki kutapeliwa na waganga na wachungaji njaa ukitaka kulipiza kisasi usifanikiwe.

Tuseme ukweli. Japo kwa jamu au siyo? Hapa hakuna anayemdai mwenzake. Kama ni kupata au kuingizana mkenge wote wametoka droo hasa ule mwezi wa kenda jumlisha mosi. Kwani, Tapeli kawapa ahadi feki nao wamempa imani feki. Sasa wanalia nini?

Ngoja tuseme ukweli hata kwa chati. Soma taratibu wasikusikie wakaninyotoa roho bure kwa kuwapa ukweli laivu ingawa unauma na hawautaki. Ila walevi wawe wakubwa hata wadogo kumbuke.

Katika upuuzi huu, vizazi vijavyo vinazidi kuwekwa pakanga kiasi cha siku moja kukojolea makaburi yao wasipoangalia. Mie sitakuwamo.

Kaburi langu litapambwa kwa vito na dhahabu kama maneno yangu. Historia nshaiweka sawa. Walatini husema scripta manent-lililoandikwa ni la milele. Amini nawaambie enyi walevi mliolaaniwa. Maneno haya nayapiga muhuri wa utukufu si ukufu na hakika yatadumu na dahari.

Kwa vile nyumbani kwa mfalme hata nyumba zake ndogo wanapata umeme, tatizo liko wapi kwa mende kulala kizani wakazaane na kuzaana hadi wawe kero? Shauri yenu. Kwani nyinyi mna tofauti gani na mende iwapo wote ni mahuluku wa Rabana?

Kwani mende mwawazidi nini iwapo wote mwaishi gizani na kufanya uchafu wenu? Msijeanza kusema natukana. Watumende ni bora kuliko mendewatu. Mende hasa wabakao hata uchumi na maendeleo ni wabaya sana hata kama wana sura za binadamu. Hivi mwenye kosa kati ya mmedeaji na anayemendewa nani nijulisheni?

Nawatakieni mwaka mpya wenye kila heri hasa kiza. Acha niwahi home kabla mibaka na vibaka hawajaninyotoa roho na giza hili.
Chanzo:Tanzania Daima Januari 5, 2011.

2 comments:

Jaribu said...

Shida ni Waswahili tuna uoga na shauku ya kuabudu. Kila mtu anavunga kufa mpaka jamaa wamepata fursa ya kutengeneza hati za kusajiliwa Dowans. Eti Dowans SA ya Costa Rica, (mailbox address no doubt), Singapore, Mhindi Mmoja na Mkenya. Hao serikali ndio waliona wana uzoefu wa kuzalisha umeme. Halafu wanasema kuwa watawalipa anyway. The arrogance na unmitigated gall ya hawa jamaa ni inexplicable. Ni kama wanawathubutisha wananchi, "Sasa mtatufanya nini?"

Anonymous said...

I agree with you Jaribu. Ivi at what point do people in Tanzania say basi inatosha!!! Kweli tunanyanyaswa kiasi hiki na watu wachache?? Hakuna njia kabisa ya kustop hawa watu. When do we say enough is enough? Itafika mahali mtu unauzwa na familia yako mkiwa ndani ya nyumba. It is time tutafakari how did we get here and where are we going from now.Oh Tanzania what a lost nation!