Sunday, 16 January 2011

Kombani, Mwema, Nahodha na Werema wanangoja nini?


Katika kile kinachoonekana kuwa mpito wa kupata katiba mpya ya Tanzania, mambo mengi yalitokea.

Baada ya upinzani, asasi zisizo za kiserikali, vyombo vya habari, wanataaluma na watu mashuhuri kuja juu kuwa lazima Tanzania iwe na katiba mpya inayokwenda na wakati, kulitokea mambo na kauli ambavyo usingetegemea.

Aliyefungua pazia la kufanya visivyofanywa wala kupaswa kufanywa naye ni waziri wa sheria na katiba, Celina Kombani. Bila aibu wala kuchelea jinsi mawazo yake yangepokelewa hasa kama mtendaji mkuu anayemwakilisha rais kwenye masuala ya katiba na sheria, Kombani aliamua kujiongelea kizembe kiasi cha kuamsha moto mkali.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuandikwa katiba mpya alisema kuwa haoni sababu jambo ambalo lilichukuliwa kama kutokujua mipaka ya mamlaka yake. Wengi walimshutumu na kumkosoa vya kutosha. Ajabu hakuondoa kauli yake ambaye kimsingi ilipingana na nafasi yake. Wengi walijiuliza mantiki ya kuteuliwa kwake ilhali akionyesha kupwaya kwenye nafasi husika. Wengine walikwenda mbali na kumueleza kama waziri asiye na ujuzi wowote wala kufaa kushika nafasi hii nyeti.

Wa pili kuwasha moto si mwingine bali mwanasheria mkuu wa serikali jaji Fredrick Werema ambaye alitamka kizembe, kama Kombani, alisema kuandikwa katiba mpya mwiko na ruksa kuweka viraka.

Wengi walishangaa sana kuona mtu mwenye taaluma ya sheria na wadhifa wa jaji ukiachia mbali uanasheria mkuu wa serikali kujisemea kama mtu wa mtaani. Hata alipotakiwa kujiuzulu au kuondoa kauli yake, aliporomosha matusi mengine akidai kuwa wanaomtaka ajiuzulu wana mawazo ya kitoto!

Wengi walishindwa kutofautisha utoto wa wanaomtaka atende haki na wake.

Kwa watu wenye nafsi zinazowasuta, Kombani na Werema walipaswa kuwa wamejiuzulu. Kama hili limewashinda kutokana na kutokuwa na moyo huo, inashangaza ni kwanini mamlaka zilizowateua zinaendelea kuwavumilia ilhali umma hauwataki wala kuwaamini tena!

Walioptakiwa wajiuzulu, hawakutoa uzito kwa madai haya kutokana na kujiona kama hawana kosa. Kisheria wana makosa makubwa tu. Kosa lao kubwa ukiachia mbali kuwadharau wananchi, si jingine bali kupingana na rais ambaye ni bosi wao.

Kwani wakati wakisema hakuna haja ya kuwa na katiba mpya, rais Jakaya Kikwete, kwenye hotuba yake ya kuukaribisha mwaka mpya, aliwazodoa kwa kutangaza kuwa lazima kuwepo katiba mpya.

Licha ya kupingana na rais jambo ambalo ni hatari hata kwa serikali, walikiuka kanuni muhimu ya uwajibikaji wa pamoja, yaani collective responsibility. Hali ya kuwa na misimamo tofauti baina yao na bosi wao, inawaondoa kwenye serikali yake waliyoapa kuitii na kuitumikia.

Kama Tanzania ingekuwa na utamaduni wa kuwajibika au kuwajibishana, mwaka huu ungeweka historia katika hili kutokana na watendaji wengi kujiingiza kwenye mvutano na aibu bila msingi wowote.

Mwingine aliyetia fora anayepaswa kuwajibika tena haraka si mwingine bali waziri wa mambo ya ndani Shamsi Vuai Nahodha. Hii ni kutokana na kuruhusu jeshi la polisi kujiingiza kwenye mauaji ya raia waliokuwa wakitimiza haki yao ya kidemokrasia-kuandamana. Rejea mauaji ya hivi karibuni yaliyofanywa na polisi kule Arusha ambapo watu watu walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa pia mali nyingi kuharibiwa.

Huyu sambamba na mkuu wa jeshi la polisi Said Mwema, walipaswa kuachia ngazi usiku wa tukio. Bahati mbaya wanatafuta wa kutwisha mzigo mojawapo wakiwa eti ni askari walioua. Je waliua kwa amri ya nani kama siyo hawa wakubwa wawili? Pia ukiangalia hata jinsi wanavyoshughulikia kadhia hii kwa kutaka mkutano na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) utaona jinsi wanavyojifunga moja kwa moja.

Hawa walijiruhusu kufanya maamuzi bila kufikiri na kufikiri baada ya kutokea maafa. Wengi wanajiuliza mantiki ya kuwa na mkutano na CHADEMA baada, na si kabla, ya mauaji haya ya kinyama.

Kinachosikitisha na kukera zaidi ni ile hali ya kupendekeza mkutano wa 'kuweka mambo sawa' ilhali walishindwa hata kuyalaani mauaji yenyewe. Hapa, kimsingi, kinachotakiwa si kukaa pamoja bali kuwajibika kwa kuachia ngazi ili watu wengine wenye uwezo na ustaarabu wachukue nafasi na kufanya kazi vilivyo.

Kutokana na uchafu, usugu, upofu, uroho, ubabe na kutojisuta kwa watawala wetu, wahusika wanaweza kuendelea kukaa kwenye ofisi za umma hata kama wameishapoteza udhu, kimsingi wanazidi kujidhalilisha na kumdhalilisha na kumdhalilisha rais kwa kushindwa kutumia madaraka yao vizuri.

Chadema wamefanya jambo la maana kukataa kukaa meza moja na watu waliowanyanyasa kuwaua na kuwadhulumu. Laiti hata wangelaani mauaji ndipo wakafikiria kufanya huo mkutano ambao nao si muhimu zaidi ya kuwajibika.

Hawa wanapaswa kujiuzulu ingawa walikuwa wanatimiza amri ya bosi wao rais Jakaya Kikwete aliyetamka wakati wa mvutano na wafanyakazi na baada ya kudaiwa kuchakachua kura kuwa atalazimika kutumia nguvu ya ziada na watakaoumizwa na polisi wasilaumu. Sasa yake yametimia. Hawa wanaotaka mazungumzo nao si wanapingana na nia na tamko lake?

Wengi wanaendelea kushangaa ujasiri wa wahusika tajwa na bosi wao kushindwa kujiwajibisha au kuwawajibisha wateule wake! Je namna hii tunaweza kusonga mbele kidemokrasia? Je zile tambo za amani na utulivu bado zinaleta maana au uhuni mtupu?

Kwa vile wahusika wamesiliba pamba masikioni, kuna haja ya umma wa watanzania kushinikiza watu wasiofaa kuachia ngazi. Kwani ofisi wanazotukana si mali yao wala baba zao bali watanzania.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Januari 17, 2011.

4 comments:

SIMON KITURURU said...

Mmmh!

Na ile ndude ya kitabu chako aka KRITIKI ntaipandisha pale kwenye blogu yangu!

Kilichochelewesha ni ushabiki wa niliowapa kitabu chako na waliotaka kushabikia na wengine kukitemea mate poo kwa kufikiri unaajenda tu kwa kuwa UFISADI haujakufaidisha kitu fulani bongo!.

Ni ndefu kidogo ingawa imekaa kitaalamu nikiiachia.

Nasubiri mtu mmoja tu ambaye ndiye kitabu chako kiko kwake anitumie anasema ninni!


Mtakatifu tuko pamoja!

NN Mhango said...

Nitashukuru. Si vibaya hata ukiitundika hapa hapa. Wanaosema ufisadi haujanifaidisha wako sahihi. Ufisadi hauwezi kumfaidisha mtu anayeishi kwenye kesho. Kutema mate hata kutukana ni haki yao ilmradi nao wapange kuandika vyao lau tusome mawazo yao.
Mtakatifu mwenzio

SIMON KITURURU said...

Ntafanya hivyo basi ingawa KIVIPENGELE kwakuwa nafikiri kisehemu cha comment kina vibano vyake vizuiachoo taralila ndefu kiujazo!:-(

NN Mhango said...

Basi nitumie kwa email yangu ya nkwazigatsha@yahoo.com