Monday, 24 January 2011

Ni Tambwe Hiza huyu anayewaita wenzie vichaa?

Tazama picha hizi uone ni nani au wapi wanaelekea kuokota makopo.

Tambwe Hiza mganga njaa na nyemelezi anayeweza kurukia chama chochote ili mkono uende kinywani ni mugumu wa kujifunza. Sijui ni kutokana uelewa na elimu ndogo au kuzidi kujipendekeza ili aongezewe malipo yatokanayo na mabaki ya ufisadi?

Hivi karibuni alikaririwa akimshambulia katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk Wilibrod Slaa. Akisema: “Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba kiongozi huyo amepandwa na wazimu, alichobakiza ni kuvua nguo tu…amechanganyikiwa na ndiyo maana anatapatapa kutafuta lolote la kusema.”

Tuwe wakweli jamani. Hivi kati ya Dk Slaa aliyemtingisha hata bosi wa bosi wake Jakaya Kikwete na kidampa kama Hiza nani anakaribia kuvua nguo? Nani hajui kuwa Hiza aliljivua nguo alipojiunga na CUF na kutimua baada ya kushindwa ubunge?

Kwanza, sijui kama haya maneno ni ya Hiza au ni Martin Shigela au Salva Rweyemamu mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ambao, sawa na Hiza, wameonyesha kuwa uhuni haumtoki mtu ukiishamuingia. Tuachane na aliyemkopesha nani uchafu huu. Maana uhuni ni uhuni hata kama anayeufanya anatetea ikulu au chama tawala.

Kuna haja ya kujiuliza ni kwanini Hiza ameteka madaraka chamani. Nadhani, ingawa CCM imekuwa ikishutumu vyama vingine kwa ukabila, Hiza anafanya hivi kutokana na kuwekwa alipo na mtu wa kabila lake Yusuf Makamba (katibu mkuu wa CCM) ambaye baada ya kumpachika mwanae serikalini na chamani ameonyesha wazi anavyotumia madaraka yake kwa ajili ya familia na hata kabila lake.

Niliwahi kumtaka Hiza hata mjomba wake Makamba wanipe vigezo vitatu tu vya kufungua ofisi ambayo hata kwenye katiba ya CCM haimo ya Propaganda. Bahati mbaya kutokana na ukweli na uzito wa hoja yenyewe waliingia mitini na kunywea.

Kwa anayejua uchu na udhalili wa Hiza, hashangai kuona akimvamia Dk Slaa. Huenda ana hasira baada ya kushindwa kusimama ubunge ukiachia mbali kuanza kustuka kuwa kadri anavyokaa kimya bosi wake anapunguza mlo. Ndiyo, mbwa ili alipwe lazima awinde au hata kubweka kama afanyavyo Hiza. Ila kwa umri wake, huku ni kuchelewa kukomaa kiakili na kisifa kama mwanaume.

Hiza na Makamba wamegeuka midomo ya mafisadi. Wanatumiwa kirahisi kutokana na uwezo wao mdogo wa kufikiri na ile hali ya kuendeshwa na tamaa.

Ningemshauri Dk Slaa na CHADEMA wasimjibu. Maana wakifanya hivyo licha ya kupata umaarufu, wanamtengenezea kitumbua kwa bosi wake. Hiza kweli ameishiwa. Anatoa tamko la kipumbavu leo, kesho yake umoja wa vijana wa CCM unakuja na kile kile. Hii maana yake ni kwamba zee hili ambalo linajiona ni kijana limewafundisha uhuni vijana.

Kwanini Hiza haoni ukichaa wa mjomba wake aliyechekelea mauaji ya Arusha asijue kila mtu atakufa? Mbona CHADEMA hawakuchekelea kuanguka anguka hovyo kwa mwenyekiti wake?

Hiza anasema CCM ina mpango wa kumfunga na kummaliza Dk Slaa. Huu ni uzushi na vitisho vya kipumbavu. Tangu lini CCM ikawa mahakama? Na kwa kusema hivi amemsaidia Dk Slaa bila kujua. Maana akifungwa tutasema ni shinikizo la CCM. Laiti angekuwa na elimu lau akatumia busara kujua hata mambo madogo ya kisheria. Lakini hakuna haja ya kumshagaa au kumuonea Hiza kutokana na shule kumpiga chenga. Na hii ndiyo maana hata hiyo ofisi ya propaganda na zile za wilaya zimejaa vihiyo wasio na usomi wala busara.

Hivi kati ya bosi wake Hiza na Slaa nani anakaribia kuokota makopo? Arejee anavyosakamwa kukisambaratisha chama kutokana kupayuka hovyo huku akiwatumia wahuni na vihiyo kama Hiza kuchafua hewa chamani.

Hiza amesahau kuwa kampeni za uchaguzi zimekwisha. Hata waganga njaa wenzake kama vile yule mtabiri muongo na mashehe wengine njaa bila kusahau hata maaskofu njaa wamejua kuwa wakati wa kugeuzana miradi umepita na anachoongea kinafuatiliwa kwa makini!

Je kwanini CCM wanapenda kumtumia Hiza na si watu wenye akili angalau na mashiko hata kama ni mafisadi? Je wanajua anavyodharauliwa, hivyo kutoweza kushitakiwa? Maana wangewatumia watu wenye mashiko nadhani kesi ingefunguliwa haraka. Lakini nani yuko tayari kumpeleka mahakamani mtu ambaye ni karibu na hayawani?

Hata kama Hiza anasumbuliwa na njaa na hawezi kula bila mafisadi kumtumia makombo baada ya kujikomba, inabidi aanze kukomaa na kujifunza. Asisahau kuwa alipokuwa CUF alikuwa akitamka mambo ambayo kwa sasa anayaramba kuonyesha alivyoharibikiwa kiakikili. Je mtu wa namna hii si kichaa? Je tabia hii ya mbwa ya kuramba matapishi yake inamfaa mwanadamu?

Wengi wanajua. Hiza baada ya kuukosa ubunge na kuwa na kisomo kidogo kiasi cha kutoweza kufaa kuajiriwa, alijirejesha CCM kama mbwa koko afanyavyo baada ya kudokoa kwa aliyemfuga. Siku zote nimekuwa nikitahadharisha kuhusiana na siasa za ukuku, ufisi na umbwa. Kuku hula asichozalisha na kuzalisha asichokula. Hiza anazalisha migongano na kula pesa ya walipa kodi.

Kwa vile Hiza ameridhia kufugwa kama kuku, basi aachane na kanga wanaojitafutia kwa heshima hata kama wamekondeana. Asiwacheke wakati wao ndiyo wapaswao kumcheka ingawa hawafanyi hivyo.

Wengi wanaomjua Hiza wanamjua kama mtu wa kuhurumiwa ambaye hali hadi achochee wenzake. Wanamjua alivyo na uchu wa fisi jambo ambalo linamfanya ashindwe kujitofautisha na changudoa awezaye kulala na yeyote ilmradi ale. Hii siyo sifa inayomfaa mwanadamu tena mwanaume.

Kama tungekuwa hatuna adabu kama Hiza basi tungemshambulia mwenyekiti wake kutokana na sasa kuishiwa hadi hata umoja wa watoto wa chama chake kuanza kutoa matamko makali baada ya kumuona kimya na hafai hata kidogo. Lakini bado tunamstahi ingawa ni wa hovyo kiasi cha kutumia watu wa hovyo kama Hiza hata yule msemaji wake ambaye naye alimshambulia Slaa kwa staili hii hii. Hata hivyo hatuwashangai hawa kutokana na kujulikana wanavyoishi kwa kujikomba hata kwa kukiuka kanuni taratibu na maadili. Huko leo si mada.

Kwanini Hiza asimwambie mwenyekiti wake aache kuwaangusha na kuwadhulumu watanzania? Ametimiza ahadi gani na ngapi tangu aingie madarakani zaidi ya kutumia muda mwingi kufikiri jinsi ya kuua kashfa zinazomkabili, watu wake, chama na serikali yake?

Kwanini Hiza hashupalii Dowans? Hawezi kukata mkono unaomlisha yeye na bosi wake na yule mhuni mwenzie wa ikulu.

Sijui kama Hiza hununua magazeti. Maana watoto wake au mkewe wakisoma, watavunjika moyo na kujilaumu kwa kuwa na mume au mzazi kama yule hata kama aibu yake inawalisha.

Bwana Hiza kama propaganda zimeisha si uende Lushoto ujifunze lau uganga kuliko huo uganga njaa? Hivi mjomba wako siku akitimuliwa utaondoka naye kama mwana wa kufikia au utadandia chama gani?

Watanzania mdharau na kumpuuzia Hiza kwani mnajua njaa ikipanda kichwani matokeo yake ni kuwa tayari kutumiwa na kila atakaye wa kutumia kama mtumwa Hiza anavyofugwa na CCM. Isitoshe angekuwa amekwenda jando kichwani na si kukeketwa basi tungemchukulia kwa uzito wa ziada. Je wanaomtumia nao hawajaishiwa kama yeye? Je huyu ni Tambwe Hiza yule nyemelezi nimjuaye? Simba na mbwa aina ya chiwawa wapi na wapi?

Chanzo: Dira ya Mtanzania Januari 24, 2011.

1 comment:

Anonymous said...

Mpendwa Mpayukaji,

Msamehe sana Tambwe Hiza kwasababu hajui alifanyalo.

Amekuwa akihaha kutafuta maisha through siasa, sikatai kuwa siasa ni ajira pia lakini yeyote atakaye kujihusisha na siasa imempasa kujitafiti kama anazo sifa yakini za kuwa mwanasiasa.

Wengi sana (hata wewe unawafahamu) hutumika kama vinywa vya wazandiki, wahafidhina na mafisadi katika kuyasema watakayo.

-Mpingo