How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Tuesday, 4 January 2011
Dowans na Kikwete, Rweyemamu utatukana wangapi?
Taarifa ya kihuni na jazba ya hivi karibuni ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu haiwezi kupita bila kujibiwa.
Kutokana na ujumbe ulionakiriwa kwa ufupi na magazeti, si vyema kuacha Salvatory Rweyemamu, mkurugenzi wa zamani na mmilki wa Habari Corparation aliyoikuwadia na kumuuzia Rostam Aziz muda mchache kabla ya kuanza uchaguzi wa 2005, aendelee kuwatisha watu na kuupotosha umma.
Tunajua fika Rweyemamu ni kifaa kinachotumiwa na mafisadi kuwatetea kwa kutumia taaluma yake ya uandishi wa habari ambayo ameisaliti kutokana na njaa na ukosefu wa maadili. Rejea Rweyemamu kukodishwa na Richmond kuisafisha kabla ya mabomu yake ya mwisho kulipuka na kuisambaratisha na kuwadi wake mkuu.
Baada ya Rweyemamu kushindwa au tuseme kuwaridhisha mabwana zake, alipewa kazi ikulu kwa sababu kuu mbili. Moja, kusafisha uchafu wa Richmond ambao ulimshinda hata hivyo. Pili kama malipo ya fadhila toka kwa Jakaya Kikwete na mtandao wake wa Rostam na Edward Lowassa kutokana na kufanikisha kazi ya kuwachafua wagombea wengine walioshindana na Kikwete. Ajabu ni pale Rweyemamu anaposhindwa kujua kuwa ikulu si mahali pa kihuni kiasi cha kutumia lugha ya kihuni.
Ingawa Rweyemamu kajitahidi kuonyesha jazba na uchungu anapotajwa bosi wake, ameshindwa kumsaidia. Badala yake naye amekuwa sehemu ya tatizo tena nanga. Hana mbinu wala mikakati inayoingia akilini ya kumtetea bosi wake. Vitisho vyake vinazidi kumuumbua yeye na bosi wake ambaye, kama hataki matatizo zaidi, angemfuta kazi mapema na kutafuta watu wenye busara na uwezo.
Kama hili la dokta Wilbrod Slaa kusema wazi wazi kuwa Kikwete yuko nyuma ya kampuni la kijambazi la Dowans limemuudhi kiasi hiki, mbona hakupasuka Dk Slaa yule yule alipomtaja Kikwete kwenye list of shame pale Mwembe Yanga? Mbona hili la Dowans lina nafuu likilinganishwa na la EPA ambao wapinzani wanadai ndiyo mtaji uliomwingiza Kikwete madarakani ukiachia mbali sehemu ya pesa hiyo kutumika kuwahonga waandishi nyemelezi kuwachafua wengine?
Je Rweyemamu atawatukana wangapi na mara ngapi iwapo bosi wake anaendelea kufanya madudu na kunyamaza? Mbona viongozi huru wa upinzani wanaojulikana wanajua kila kitu cha Kikwete na wanatoa madai bila woga wala kificho? Je matusi ya Rweyamamu ndiyo majibu yanayotakiwa kujibu tuhuma za Kikwete na mtandao wake kuwa nyuma ya Dowans? Kama Kikwete na mtandao wake siyo Dowans hata Kagoda mbona wanafanya wamilki wa Dowans kuwa siri? Siri ya nini tena kwa wananchi waliomchagua? Je Rweyemamu halijui hili ambalo hata kunguru wanajua?
Je Rweyemamu anaweza kutwambia bosi wake alipopata pesa ya kampeni? Awe mkweli na mtu mzima. Aeleze anachojua kuhusiana na vyanzo vya bosi wake ambaye alimwaga mabilioni kwenye mabango,picha, vitenge, fulani, kapelo, kukodi ndege na helkopta kwa ajili yake, mkewe, na mwanae upuuzi mwingine. Watanzania wote si wajinga au wachumia tumbo wanaoweza kulipwa na kila fisadi kufua nepi zao.
Rweyemamu anapaswa kusoma kazi za waliomtangulia kama vile marehemu Godfrey Nkurlu na hata Habib Halahala waliofanya kazi kwa kutumia akili zaidi ya jazba.
Pia ni vizuri Rweyemamu akafahamishwa kuwa ukubwa una mwisho. Wako wapi akina Benjamin Mkapa waliosifika kwa ubabe? Je Rweyemamu hajui kuwa ajira yake ya ikulu ni ya msimu? Je wote tutajipendekeza kwa Kikwete kama yeye ili iweje?
Kwanini Rweyemamu asiombe akapelekwa kwenye ofisi za ndogo za Makao makuu ya CCM au za wilaya ambapo makanjanja wengi wanalundikwa ili kufanya kazi chafu ya kuchafuana? Kwanini Rweyemamu anajigeuza kanjanja hata kama ana Masters ya fani ya uandishi wa habari? Hapa ieleweke. Kuwa na Masters hata PhD ni jambo moja na kuelimika vilivyo ni jambo la pili. Wengine wanazo hata za kughushi. Rejea watu kama Dk Daudi Balali (Gavana wa zamani wa BoT) au profesa George Saitoti (makamu wa rais na waziri wa fedha wa zamani) wa Kenya walivyoingizwa mkenge na matapeli wa kihindi na wanasiasa mafisadi wakataka kufilisi nchi zao.
Rweyemamu asijidanganye wala kudanganya. Yake yanajulikana. Maandishi yake yenye ukali wa ajabu dhidi ya ufisadi kabla hajajisalimisha kwa mafisadi hayajaoza. Maana imeandikwa: scripta manent yaani kilichoandikwa ni cha milele.
Rweyemamu alinukuliwa akisema: “Na kama kweli Dk. Slaa ametoa kauli hii na kusema maneno ya namna hii basi sasa Watanzania wanayo kila sababu na haki ya kuamini kuliko wakati mwingine wowote kuwa mzee huyu (Slaa) sasa amechanganyikiwa na ni mtu wa hatari sana kwa utulivu wa nchi hii.”
Hivi huyu anaishi nchi gani? Hivi aliyechanganyikiwa kati ya Rweyemamu na Slaa ni nani? Yaani hajui hao mabwana zake anaowapambana na kuwa tayari kuwafia ndiyo hatari katika nchi hii kuliko huyo Slaa anayejitahidi kuhatarisha maisha yake kupambana nao ili wananchi wetu lau wasonge mbele?
Yaani bado Rweyemamu hajui kuwa Dowans ni mradi wa wakubwa na wizi wa kawaida tu! Kwanini ahoji mantiki yaliyotumiwa na bosi wake na swahiba yake Lowassa kuingiza kampuni feki kama Richmond ambayo kimsingi ndiyo hiyo hiyo Dowans? Hivi Rweyemamu anadhani watanzania hawajui kuwa Dowans ni Richmond na Richmond ni Dowans? Kama anataka kuwa mkweli, basi aeleze anwani za Dowans zilipo kama siyo sawa na za Kagoda.
Hivi Rweyemamu hajui kuwa serikali ya bosi wake inawaibia watanzania kwa kuingia mikataba ya kipumbavu tofauti na alivyotuahidi wakati wa kampeni mwaka 2005? na kuonyesha wanavyojua sana, arejee walivyomnyima kura hadi akashinda kwa kutumia uchakachuaji jambo ambalo hajawahi kulikanusha hata Rweyemamu mwenyewe. Huyu si Rweyemamu niliyemjua zama zile. Kweli madaraka ulevya hasa yanapopambwa na ufisadi!
Rais Kikwete ana matatizo mengi kama vile kutoa ahadi za uongo, kutumia vibaya pesa ya umma, kutokuwa na sera ya kutawalia, kutetea mafisadi kama ilivyofichua wikileaks hivi karibuni. Lakini na Rweyemamu ni tatizo kubwa. Maana anajipayukia bila kujua mwangi na reaction ya watanzania itakuwa vipi.
Kama kuna mtu anazidi kummaliza Kikwete, sambamba na Yusuf Makamba katibu wa CCM si mwingine bali Rweyemamu ambaye hujijibia hoja hata bila kuzipima.
Tumalizie kwa nukuu nyingine ya Rweyemamu.
“Mheshimiwa Rais Kikwete siyo mmiliki wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Dowans. Hakupata kuwa mmiliki, siyo mmiliki na wala hatakuwa, hata siku moja, mmiliki wa kampuni hii.”
Hapa hoja si kukanusha bali kujiuliza, kama kweli ni uzushi, kwanini atajwe yeye na si wengine? Kama kweli Dk Slaa ni mzushi kama Rweyemamu anavyotaka ajulikane, kwanini asimfikishe mahakamani? Mbona Slaa amekuwa akililia hili tangu alipomtaja Kikwete na wenzake kwenye list of shame na si Kikwete wala 'mafisadi' wenzake wamewahi kwenda mahakamani zaidi ya kutisha na kunyamaza?
Kama Kikwete si mmilki wa Dowans basi anamjua mmilki wa Dowans hata kwa sababu rahisi tu kuwa serikali yake ndiyo iliingia mkataba na kampuni mama yaani Richmond na hatimaye Dowans yenyewe.
Ikulu, Kikwete na Rweyemamu waache kucheza na akili zetu, kama Kikwete si mmilki au mshirika hata rafiki wa mmilki wa Dowans basi yeye na serikali yake watutajie mmilki wa Dowans. Au wanaogopa kilichotaka kuwapata kabla ya kumtoa sadaka Lowassa? Kama Kikwete si mmilki wa Dowans, mmilki ni nani hadi aitie serikali kigugumizi kana kwamba naye ni serikali ndani ya serikali?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment