The Chant of Savant

Thursday 13 January 2011

Kijiwe chatoa medali za mwaka 2010

KWA heshima na taadhima, nichukue fursa hii kuwafahamisha wasomaji wa safu hii ya muda mrefu kuwa, kwa niaba ya Kijiwe, tunatoa medali kwa watendaji wa serikali, watu binafsi na mashirika walioonyesha utendaji uliotukuka mwaka uliopita na kabla ya hapo.

Tulitaka kutoa medali hizi mwaka 2008 wakati shujaa Eddy Ewassa, waziri mkubwa aliyetimuliwa... sorry... aliyejitoa mhanga kwa ajili ya kuokoa siri-kali lakini hatukuwa na uwezo.

Tulitambua mchango wake katika kuleta mvua na umeme nchini. Tulitambua juhudi zake za kukuza uchumi kupitia uwekezaji ambao wengi hawakuuelewa hadi Dowans ilipojishindia kesi ya kitita cha shilingi 185,000,000,000 bila jasho. Hii ni sayansi ya hali ya juu inayopaswa kufundishwa mashuleni.

Pia Ewassa alililetea heshima taifa letu kwa kuliondolea aibu ambayo ingelikumba kama sirikali nzima ingetimuliwa na kufumka.

Tulijiwekea mikakati na maazimio kuwa miaka miwili baadaye tufanye hivyo. Sasa kwa heshima na utii wa hali ya juu, ninayo furaha, kama mwenyekiti wa Kijiwe, kuwataarifuni wapenzi wote kuwa mwaka huu tumetimiza ahadi yetu.

Sisi si wasanii wala wabangaizaji. Tukisema humaanisha tunachosema kama ambavyo tumekuwa tukifanya kile tusemacho.

Bila kupoteza muda, kwa niaba ya Kijiwe kitukufu ambacho kimsingi ni serikali na nchi mbadala napenda niwaleteeni washindi wa tuzo ya juu sana ya Kijiwe iitwayo The Buring Spirit of the Nation au BSN.

Hii ni tuzo ya kijiwe daraja la kwanza ambayo haijawahi kutolewa kwa yoyote na kama ingetolewa basi ingekwenda kwa mashujaa wa bara hili ambao hawakutambulika kama vile Mfalme wa Jean-Bedel Bokassa, Idd Amin, Sani Abacha na Mobutu Sese Seko kutokana na uzalendo wao kwa bara letu. Kwa vile waliishakufa, hatutawapa. The dead tell no tales.

Waliofuzu kupewa tuzo hii ya juu sana ya heshima ya BSN mbali na Ewassa ni mkuu Njaa Kaya ambaye ametimiza ahadi zake zote na kuwapeleka walevi Kanani tena kwa muda mfupi.

Ameahidi katiba mpya na kufanya walevi wafurahi. Hata isipopatikana. Maana kwao ahadi inatosha kutokana na ulevi wao wa milele.

Najua wapuuzi watabisha. Hivi kama hakukuza uchumi, jiulize. Hii pesa yote iliyotumika kwenye kampeni hadi kukodi madege na mahelikopta tena kusafirisha wana ukoo na familia kwenda kwenye kampeni wangeipata wapi?

Pia rejea serikali kuwa na pesa nyingi hadi kuweza kutoa shilingi 185,000,000,000 tena bila kujihangaisha na kukata rufaa. Kuna neema zaidi ya hii jamani?

Hapa lazima nisisitize. Sisi siyo kama wale matapeli wanaotoa shahada za udaktari ili wawatumie wahusika kufanikisha ulaji wao.

Sisi si kama wale watabiri, wachungaji, mashehe na manyang'au uchwara na wezi wanaoabudia cheo, ukuu, utukufu, kufu na mambo ya kipuuzi. Sisi hatujipendekezi zaidi ya kuwa wazalendo wa kweli.

Mwingine aliyepitishwa kupata tuzo hii ni Benny Makapu Tunituni kutokana mchango wake katika kuelimisha umma juu ya ujasiriamali. Rejea kujitwalia na kuendeleza mgodi wa Kiwira.

Anayefuatia ni Mgosi Joseph Makambale ambaye aliweka rekodi ya kuwapayukia wapingaji hasa wale wanaodai tuandike katiba mpya wakati hii iliyopo inalinda ulaji wetu.

Pia Riz Kitweke ametunukiwa tuzo hili kutokana na mchango wake wa kumsaidia mzazi wake kiasi cha kuonyesha ukomavu wa kuweza hata kumrithi.

Sambamba naye ni Roasttamu Laziz ambaye alisimamia makampuni mengi ya uwekezaji yaliyoliingizia taifa faida kubwa hasa kuwezesha kiama kushinda kwa kishindo.

Petero No-nii hakusahaulika hasa mchango wake wa kubuni mpango endelevu maarufu kama EPA au Empowering the Party on Agenda (hidden one).

Salima na Rahama Njaa nao walionyesha ukomavu katika matumizi ya majukwaa wakati wa kampeni. Nao wametunikiwa tuzo hii ya juu sana.

Bila Ninrod M-hand kupewa tuzo hii ingekosa maana. Mchango wake katika EPA hauna kifani. Did-us Masamburiri, Makorongo Muhanga, Emmy Nchimvi na Samuel Chitaahira hawakusahaulika kutokana na ubunifu wao katika kukuza taaluma na kudhibiti uhalali wa vyeti vya kitaaluma.

Annae Makidamakida anapewa tuzo hii kutokana na kutumiwa vizuri kuwakomesha wakorofi waliotaka kuingilia ulaji wetu kwa kimbelembele walichokiita viwango.

Genero Hamnaamani Shimbombo anapewa tuzo kutokana na kuwatisha wakorofi waliotaka kutuzuia kuula.

Orodha haiwezi kukamilika bila kumtaja Shehena Ubwabwa Njaa Yahya Hossein kwa kuwatisha pia wakorofi akiwafunga kamba na kuwatabiria maafa na maanguko kabla ya kuchakachuka.

Lewisi Ukame na Rajab-abu Kiravuitu wanatunukiwa tuzo hii kutokana na kuwezesha uchakachuaji ambao ulizalisha kura nyingi kiasi cha kutokuwa na mambo ya mseto ambao mara nyingi ni uchuro.

Wa mwisho katika category ya watu binafsi ni Nshomile Rweye-pendekeza-'mu ambaye amefanikiwa kutumia taaluma ya uandishi wa habari kuwa uhandisi wa habari hata kama wengi wanasema ni za uongo na kujipendekeza kama jina lake.

Kwa upande wa makampuni na mashirika, tuzo hii haiwezi kukamilika bila kampuni ya Richmonduli kupata. Hawa walikuja na ubunifu wa hali ya juu. Waliweza kujipenyeza na kuzoa tenda kiasi cha watu wenye roho mbaya kuwazushia kuwa walikuwa feki. Kama walikuwa feki waliingiaje? Je, hapa feki ni Richmonduli au walioiingiza?

Kampuni nyingine ni binti Dowans bin Richmonduli. Hii imechaguliwa kutokana uwezo wake mkubwa wa kutunza siri. Kushindwa kujulikana wamilki wake kumekiacha kijiwe hoi kiasi cha kuamua kuwapa tuzo hii.

Kampuni nyingine zilizotunikuwa tuzo hii ni Kagodoka, ambayo sawa na Dowans, imefanikiwa kutunza siri ya wamilki wake. Pia kampuni ya Mageresi Chembazi imepata tuzo kutokana na kusimamia vizuri mradi wa EPA.

Makofi milioni moja toka kwa walevi kwenda kwa washindi.

Kwa vile sasa katiba mpya imegeuka gea ya kuwaliza tena walevi, acha niishie haraka kwenda kuandika katiba mpya ya familia yangu ili kuhalalisha ubaradhuli wangu. Mke na watoto wangu wakae mkao wa kuliwa. Hakuna cha katiba mpya bali sanaa. Naona minjago inakuja wasije wakani Arusha.

Chanzo: Tanzania Daima Januari 12, 2011.

No comments: