Wednesday, 26 January 2011

UVCCM mmejikanyaga na kujichanganya, wanafiki tu
Tamko la hivi karibuni la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) limefichua uoza na migongano ya ndani ya chama.

Kwanza halieleweki vizuri ukiachia mbali kujichanganya na kuparaganya mambo kiasi cha kuharibu dhima nzima ya maana na lengo walivyotaka kuwasilisha. Kwanini hawakuwatafuta wataalamu wa uandishi angalau wakawashauri kama siyo kuwaandikia rasimu nzima ya walichotaka kuwasilisha?

Hebu tuangalie matini mazima ya taarifa ya vijana kwa umma kupitia vyombo vya habari. Kwanza, wao wanaongea kama nani iwapo walishakasimisha mamlaka yao hata ya kufikiria kwa chama chao? Je vijana wameamua kuasi ingawa ni kwa njia ya kichovu?

Suala la kwanza waliloongelea na kusisitiza ni kupendana baina ya mawaziri. Kupenda au kuchukia ni suala la mtu binafsi siyo kufundishwa wala kushinikizwa. Huwezi kumfundisha mke au mme kumpenda mwenzake. Hapa wamenoa sana tu.

Huwezi kumpenda adui yako. Ni mtu gani anayechukia ufisadi anaweza kuwapenda mafisadi au maajenti wao waliojazana CCM na serikalini? Walichoonyesha kuhusiana na mawaziri kupingana, ni wao kutokuelewa demokrasia na mkinzano wa mawazo. Kwa mfano wamewashutumu mawaziri wawili Samuel Sitta na Dk Harrison Mwakyembe hadi kuwaamuru hata waachie ngazi utadhani waliwateua wao.

Sababu ya kufanya hivyo? Kwanini walipingana na waziri wa nishati na madini William Ngeleja alipotetea ufisadi na uoza wa Dowans?

Vijana hawa wanaotia kila aina ya shaka kuhusiana na usomi na welewa wao, walishindwa kujiuliza swali moja muhimu na rahisi. Kama wanachofanya hakifai kwanini aliyewateua hawatimui?Mbona sera ya CCM inajulikana-Kulindana na wao wameikiuka!

Kama wao wanasema mawaziri wanaopingana wakitoe kwa vile wanahujumu mshikamano na uwajibikaji wa pamoja, wao mbona wanapingana na chama chao na hawakitoi? Ama kweli nyani haoni kundule.

Ingawa UVCCM wamejitahidi kuficha walivyo nyuma ya upuuzi wote tunaoshuhudia kwa kujifanya wanapinga kulipwa kwa Dowans, tumewastukia kutokana na kuwashambuliwa mawaziri wale wale wanaopinga hili kufanyika. Hii maana yake ni kwamba wamechomeka hoja yao ya Dowans kufanya kile wazungu huita to get away with it. Kimsingi hawa ni watoto wa Dowans na wanufaika wakubwa wa mradi huu wa majambazi wakubwa.

Imenishangaza na kunihuzunisha sana niliposoma nukuu kuwa mpuuzi mmoja aitwaye Martin Shigela akikopi maneno ya kasuku wengine kama Tambwe Hiza na Salva Rweyemamu kusema eti katibu mkuu wa CHADEMA na mgombea aliyekuwa tishio wa urais Dk Wilbrod Slaa ni kichaa. Nilishangaa haya yanatoka wapi? Nilihuzunika kuona kijana mdogo saizi ya kumwita Slaa baba yake kujiamini na kuitisha mkutano wa waandishi wa habari kujivua nguo. Ukimtukana mwanaume anayelingana na baba yako umemtukana baba yako mwenyewe. Kama Slaa ni kichaa basi watanzania wote ni vichaa wakiwamo baba zao na mama zao.

Tatizo ni nini? Hawa vijana wamelelewa na kulewa pesa za kifisadi kiasi cha kukosa hata uwezo wa kutumia akili ya kawaida (common sense!

Hawa vijana ni wa ajabu kidogo. Hivi hawajui kuwa kulipa Dowans siyo suala la kisheria tu bali la kichama na kiserikali kutokana na maslahi ya nyuma ya pazia? Hivi hawajui kuwa Dowans wana Baraka za baba zao? Kimsingi ni kwamba wanajua ukweli wote. Ila kutokana na unafiki na kujifanya wajanja ili kuwahadaa watanzania wanajifanya hawajui na wako against the whole deal that feeds them. Shame on them.

Sasa wametoa “tishio na msimamo” wao. Kwanini hawakueleza nini kifanyike kama serikali haitaheshimu ushauri wao? Je pesa ya umma ikilipwa kwa Dowans watafanya nini zaidi ya kuzodolewa na wazazi wao wakanywea? Je kwanini umoja wa vijana umeamua kuvunja mwiko hata kwa kujichanganya? Je ni ile mitandao ya kumrithi Jakaya Kikwete imeanza kazi?

Je umoja wa vijana unadhibitiwa na nani kati ya yule fisadi rafiki wa Kikwete anayetaka asafishwe agombee mwaka 1015 na yule mwenye ushawishi kwenye UVCCM mwenye kashfa ya kughushi vyeti? Je wote wamejipima hata wakigeuziana silaha? Je umoja wa vijana hautumiwi jambo ambalo ni aibu?

Kwanini waliokuwa meza ya mbele kwenye mkutano na waandishi wa habari waliongea isipokuwa Ridhiwan Kikwete? Je amemgeuka baba yake au anatafuta ushirika mpya wa kumwezesha na kumlinda baada ya baba yake kuachia ngazi?

Nani amewatuma hawa vijana kupayuka waliyopayuka ingawa hawatafanikiwa kumhadaa mtu. je ni yule jamaa mwenye ushawishi UVCCM ambaya anajulikana alivyoghusi vyeti na kujipachika udaktari sambamba na yule aliyeua mradi wa mabasi ya wanafunzi wa Dar es salaam.

UVCCM waliongelea suala la kuchelewesha mikopo ya elimu ya juu na walihoji ni kwanini wanafunzi wanapogoma leo kesho yake matatizo yao yanatatuliwa?

Kama hawajui jibu, wakamuulize mwenyekiti wao ambaye ameunda serikali isiyowajibika kwa umma isipokuwa mafisadi. Pia huu ni unafiki baada ya kuona joto lilivyouwakia utawala zandiki wa zamani wa Tunisia. Wao wanaathirika nini iwapo wana nafasi za umma kusoma nje hata kughushi vyeti?

Kwanini kutambua tatizo hili baada ya wanafunzi kulitatua kwa njia ya migomo? Vijana waathirika wasiingie mkenge na kuhisi UVCCM inawajali. Hakuna cha kuwajali wala nini bali kutaka kuwatumia kuficha uoza wao. CCM imegeuka kila adui wa mtanzania. Mwenye mapenzi mema na watanzania na Tanzania hawezi kuendelea kuwa CCM hata alalamike na kupinga vipi.

Upuuzi na udhaifu ulioonyeshwa na UVCCM unaweza kuandikiwa hata msahafu.

Chanzo:Tanzania Daima Januari 26, 2011.

No comments: