KWA MUDA mrefu sasa, jamii na vyombo vya habari vimekuwa vinashinikiza serikali imtaje mmiliki au wamilki wa kampuni ya Dowans ambayo ilishinda kesi hivi karibuni dhidi ya serikali na kuamriwa ilipwe Sh. Bilioni 185.
Kwanza, hiki ni kiwango kikubwa cha pesa hasa kwa nchi maskini, ombaomba na tegemezi kama yetu. Pia ni kwa ukubwa wake, kiwango hiki, kwa akili za kawaida, hakipaswi kulipwa bila maelezo.
Tunataka tujue tunamlipa nani. Nitashangaa kama wafadhili hawatapiga kelele au hata kusitisha misaada na michango yao kwa serikali isiyojali pesa ya umma. Vinginevyo nao wawe na faida na chumo hili la wizi.
Pili, kwa namna serikali ilivyojiandaa kulipa pesa hii, si bure. Kuna dalili zote kwamba kuna mkono mtu au watu, tena wakubwa.
Je, hii iliandaliwa wakati wa kufunga mkataba, huku wahusika wakijua mwisho wa siku watashinda kiulaini kutokana na kufanya makosa ya kisheria kwa makusudi?
Nitoe mfano. Kama wewe ni hakimu ama uliyekula rushwa au kuwa na maslahi na kesi iliyo mbele yako na unataka kumsaidia mshitakiwa, unaweza kufanya makosa ya kisheria ili akikata rufaa ashinde kesi.
Unaweza kumfunga kifungo kikubwa kuliko kinachotamkwa na sheria au kupuuzia baadhi ya masuala muhimu katika kufikia hukumu.
Hivyo basi, ieleweke kuwa walioingia mkataba na Dowans walijenga mazingira ya kuweza kushinda kesi kupitia kuvunjwa mkataba. Na hii yaweza kuwa mojawapo ya sababu zilizopelekea mkataba husika kukatizwa siku 90 kabla ya mwisho wake.
Hii haihitaji kujua sheria. Kwanini wavumilie muda wote walipotekeleza mkataba, halafu wauvunje siku chache kabla ya kufikia mwisho wake?
Je, kwanini mkataba wa Dowans ulikatishwa kabla ya siku 90? Na aliyefanya uzembe huu atachukuliwa hatua gani? Je, Dowans ni nani na mali ya nani?
Je, ilikuwaje Dowans kupata uhalali wa haraka kuchukua kazi ya kampuni ambayo ilitimuliwa kutokana na kuwa ya kitapeli?
Haya ni baadhi ya maswali ambayo umma unajiuliza, ingawa serikali haitaki kuyatolea majibu zaidi ya kuwashawishi wakubali kuingizwa mkenge; kuibiwa mabilioni ya shilingi kulipa kampuni yenye kila alama ya utata ukiachia mbali mtangulizi wake.
Je, Dowans si Richmond? Kwanini serikali haitaki kushughulikia maswali rahisi lakini muhimu kama haya na badala yake inakurupukia kulipa pesa ya umma kwenye dili zenye kila aina ya dalili za ufisadi na ujambazi?
Je, serikali ya namna hii itatuvusha kweli? Richmond walikuja wakachota. RITES nao walikuja wakachota. Na sasa Dowans ikiwakilisha mama yake Richmond inachota kwa mara nyingine. Hii imekuwa nchi ya matapeli na mafisadi kujichotea ilhali umaskini unazidi kuongeza makali yake?
Je, ni kweli kuwa wamilki wa Dowans, kama Kagoda, hawajulikani? Tutawapa mbinu rahisi ya kuwajua.
Ili kuwajua, waweza kuwauliza waliowaingiza hadi kuwawajibikia. Mmojawapo wa watu wanaoweza kutusaidia ni Edward Lowassa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, Lowassa aliibeba saba Richmond (akiwa waziri mkuu), na taarifa zinasema alipofika mahali akaona mambo yangekuwa mabaya kwa serikali na wahusika wengine, akaamuru ifukuzwe; akakataliwa.
Na kwa kuwa tunajua kuwa Richmond ilijivua mzigo na kuuvalisha kwa Dowans, serikali itakuwa inalinda siri za Dowans kama itasema kwamba haijui Dowans ni nani.
Ajabu ni kwamba serikali hii hii inayoficha kuwataja wamilki wa Dowans, bila aibu, inataka kuwalipa Dowans hao hao fedha ya umma!
Kama Lowassa atasema hajui kitu kuhusu Dowans, kitu ambacho hawezi kufanya, basi waulizwe waliosaini mikataba ya Dowans. Katika hili, ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali haina ujanja.
Kama na hawa nao watasema hawajui kitu, basi benki zilizowadhamini ziulizwe, ingawa zitasema hili si jukumu lake. Kama benki zitakataa, basi rais aulizwe kwani serikali yake ndiyo ilisaini mkataba na Dowans.
Ikishindikana, basi umma uamue kuiwajibisha serikali; maana pesa inayolengwa kulipwa si ya wamangimeza hawa wanaokataa kuwataja watu wao.
Haiingii akilini. Iwe serikali au mtu binafsi, huwezi kuingia mkataba na mtu usiyemjua au asiyejulikana. Kwenye sheria za mikataba hili ni jambo la lazima, na lisipotimizwa mkataba huwa batili.
Wanaogopa nini na kwanini? Kimsingi, serikali inajua wamiliki wa Dowans, bali inaogopa ucahfu wa kile ilichokifanya na Dowans.
Kama Dowans ni “mtoto” wa Richmond tunayoijua, maana yake ni kwamba serikali yetu si makini au ina ushirika na mafisadi.
Je, haya yanathibitisha madai ya muda mrefu kuwa serikali ya awamu ya nne iliingia madarakani kwa mtaji wa fedha za ufisadi wa EPA, madai ambayo hayajawahi kukanushwa kikamilifu?
Nani yuko tayari, kwa mfano, kutoa maelezo ya CCM ilikopata mabilioni yaliyoingizwa kwenye uchaguzi uliopita? Jikumbushe fulana, mabango, khanga, kapero na upuuzi mwingine uliosambazwa nchi nzima, bila kusahau msururu wa helikopta za mgombea urais, ndege za serikali na za kukodisha.
Je, upenyo huu unaweza kutuelekeza na kutafsiri maana ya serikali kutaka kuilipa Dowans kirahisi?
Tuhitimishe kwa kusisitiza kuwa wamilki wa Dowans wanajulikana ila kinachogomba ni washirika wao waliomo serikalini kuogopa sura zao halisi katika ufisadi kujulikana.
Mficha maradhi kilio humfichua. Kuna siku watajulikana na kuaibika, ukiachia mbali kuadhibiwa hasa ikizingatiwa kuwa mamlaka yana mwisho.
Tuwakumbushe. Rais mstaafu Benjamin Mkapa alifanikiwa kuficha kashfa yake ya Kiwira. Alipoondoka madarakani ilifichuka na akaaibika. Analindwa tu na rais aliye madarakani.
Je, serikali inayojidai ni ya wananchi inawaficha wananchi shughuli zake ili iweje? Je, na wananchi wataendelea kugeuzwa majuha na kuibiwa kila uchao wasichukue hatua?
Tufanye kila liwezekanalo, serikali iwataje wamiliki wa Dowans na isipofanya hivyo tugomee pesa yetu kuibwa mchana kweupe.
Chanzo: MWANAhalisi Januari 12, 2011.
No comments:
Post a Comment