How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Wednesday, 23 February 2011
Dk. Mwinyi anangoja nini kung’atuka?
KUNA usemi kuwa mtoto wa nyoka ni nyoka. Wakati mwingine si kweli. Japo si kwa sura, kuna kipindi mtoto wa nyoka anaweza kuwa kijimjusi cha kawaida tu na si nyoka kama mzazi wake.
Kwa wanaokumbuka simanzi, hasara na majonzi vilivyotokana na milipuko ya mabomu huko Gongo la Mboto ndani ya muda mfupi baada ya ile ya Mbagala, tutaelewana.
Baada ya tukio hili la kizembe na kichwa ngumu vya watendaji wetu, macho na masikio yote yameelekezwa kwa Waziri wa Ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi, ambaye silaha zake zimelipuka na kuua raia.
Wengi, kwa kujua uungwana wa baba yake, na ahadi aliyoitoa yalipolipuka mabomu ya Mbagala, walidhani siku ya pili ya milipuko Mwinyi angewajibika bila kungoja kuandikiwa tahariri na makala.
Maana aliahidi mwenyewe kuwa hili lisingetokea tena chini ya uangalizi wake. Sasa limetokea. Anangoja nini?
Kama Mwinyi ataendelea kung’ang’ania madaraka, licha ya kumwangusha baba yake anayeshimika sana, atakuwa amejiingiza kirahisi kwenye kundi la mafisadi na ving’ang’anizi.
Pili, ukiangalia idadi ya waathirika, tunaambiwa waliofariki dunia ni 39 na majeruhi 292, kama hatajiwajibisha, unagundua Mwinyi mwingine tofauti ya yule tuliyezoea kumuona.
Tatu, ikizingatiwa kuwa hii ni mara ya pili ndani ya muda mfupi, Mwinyi anajikuta hana utetezi wala sababu ya kuendelea kushikiliwa wizara inayoua wananchi.
Nne, ukirejea ahadi aliyoitoa mwenyewe bila kulazimishwa, kutoitekeleza anazidi kujiweka kwenye kundi la watu waongo na waroho wa madaraka hakuna mfano.
Tano, ukiangalia usafi, staha na faida ya kujiwajibisha kwa baba yake, Mwinyi anaonyesha dharau kwa mfano huu ambao hurudiwa kila zinapoibuka kashfa. Kwa lugha nyepesi ni kwamba anamdharau baba yake.
Kwa mwenye kujaliwa kujisuta na kuwa na huruma na utu, idadi ya waathirika bila kutaja mali ni kubwa sana. Hapa hujaongeza idadi ya waliokufa kwenye milipuko kama hii ya Mbagala.
Dk. Mwinyi anaweza kuja na wimbo ambao tumezoea kukisikia kuwa yeye si mtunzaji wa ghala la silaha. Akumbuke. Baba yake alipojiuzulu hakuwa mlinzi wala polisi waliowaua akina Nzegenuka kule Kanda ya Ziwa.
Mzee Mwinyi alijiuzulu kutokana na vifo vya watu wasiofikia hata kumi. Hii ni changamoto kwa mzee Mwinyi na mwanae.
Dk. Mwinyi atakuwa mtu wa ajabu na asiyefaa kama hataliona hili. Uko wapi na utekelezaji wa ripoti ya milipuko ya Mbagala.
Kuwajibika, mara nyingi huwakumba wenye kusimamia idara au wizara kutokana na kuguswa vibaya kwa wizara zao. Hata hivyo, tukumbuke. Kuwajibika ni hatua na njia ya wanyoofu na si wapotofu na mafisadi.
Dk. Mwinyi angepaswa kuelewa na kujiuliza baadhi ya maswali ili ajipime na kubaini anavyopwaya kwa kuchelewa kuwajibika. Kama anangoja rais amwajibishe anakosea sana. Rais wetu hana nia, silka wala udhu wa kuweza kumwajibisha yeyote kutokana na kuchafuka sana.
Hakuna kituko kilichoniacha hoi kama maneno ya Jakaya Kikwete kwenye eneo la tukio. Alikaririwa akililia vifaa badala ya watu.
Alikaririwa akisema: “Haya ni maafa ya kitaifa, kwa sababu kikosi hiki ndiyo makao makuu ya hifadhi ya kijeshi, ikiwemo silaha na mavazi yao, ambayo mpaka sasa hivi naongea vyote vimeteketea kwa moto.”
Aliendelea kusema: “Kwa taarifa nilizonazo ni askari mmoja aliyejeruhiwa, hivyo basi ninawaomba wananchi waondoe wasiwasi juu ya tukio hilo, serikali iko pamoja nao kuhakikisha kuwa hatari zilizopo zinadhibitiwa, na kwamba wananchi wanarudi katika hali yao ya kawaida.”
Huyu si mtu wa kuwajibika, wala kumwajibisha mtu kutokana na tunavyomjua. Mtu anayelilia askari mmoja na vifaa akipuuzia maelfu ya watu wasio na hatia utamuweka kundi gani?
Pia Mwinyi anapswa kujua kuwa wananchi hawajui ajali wala nini. Hata ingekuwa ajali bado haizuii sheria kuchukua mkondo wake. Madereva wengi waliofungwa magerezani wamefungwa kutokana na ajali kama hii ya Gongo la Mboto na Mbagala.
Ajali inaweza kusameheka kama hakuna uzembe nyuma yake. Swali ambalo litamsumbua sana Mwinyi ni kwanini hakujifunza kutoka Mbagala wala kutimiza ahadi yake?
Maswali mengine ambayo Daktari mwinyi anapaswa kujiuliza ni Kwanini silaha kuwekwa kwenye maeneo wanamoishi raia?
Kwanini wahusika hawakujifunza kutoka kwenye tukio la Mbagala ambalo ni la karibuni kabisa ukiacha yaliyowahi kutokea huko nyuma?
Je, huu si uzembe unaotufanya tumshauri na kumtaka Mwinyi aachie ngazi? Ingekuwa nchi za wenzetu hata rais na serikali yake wangefurushwa na kuweka watu wenye kujua kazi kwenye nafasi zao.
Tunatawaliwa na watu wasio na roho zaidi ya uroho. Kama ukijiuliza utitiri wa kashfa unaoendelea kukaliwa na serikali ya sasa, utakubaliana nami kuwa tunatawaliwa na viumbe wa ajabu wasio na utu wala nafsi zenye kufanya kazi sawa sawa.
Hebu tujikumbushe kashfa za EPA, Richmond, Dowans, kughushi vyeti vya kitaaluma, kuzagaa noti bandia, milipuko ya Mbagala, mauaji ya hivi karibuni huko Arusha, uchakachuaji na wizi wa kura na nyingine nyingi.
Watuhumiwa wamefanya nini zaidi ya genge husika kuendelea kulindana? Nani anawawajibisha? Nani anawajibika? Anyway, haya yanaandaa safari ya kwenda Tahrir kuwafurusha Mubarak wetu.
Tumalizie kwa kumpa mwana wa Mwinyi busara nyepesi. Baba yake yaani mzee Mwinyi angetaka kung’ang’ania kwa tamaa ya madaraka angeweza. Kwanza wakati huo haukuwepo ustaarabu wa kuwajibika zaidi ya kuhamishwa.
Lakini hakutaka kuendelea kupata vinono vyenye damu ya watu nyuma. Pia hakutaka kutolewa kama mfano mbovu wa uwajibikaji kama wale waliolazimishwa au waliokataa kuwajibika.
Kwake, mzee Mwinyi, cheo ilikuwa ni dhamana na si urathi wala mtaji wa kuukata kama ilivyo sasa.
Kama kuna alichoshindwa Dk Mwinyi kutoka kwa baba yake si kingine bali kusoma alama za nyakati na kujisuta ambako kulimletea heshima baba yake.
Chanzo: Tanzania Daima Februari 23, 2011.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment