Monday, 14 February 2011

Suto kwa wadini wa Tanzania ufisadi hauna dini

Picha zote toka Jamii Forums.

Hakuna ubishi kuwa mtu akijitambua na kujua haki zake za msingi huwa hana kikwazo. Yaliyotokea hivi karibuni nchini Misri ni ushahidi tosha.

Baada ya wamisri kuchoshwa na ufisadi, hawakukubali kugawanywa kwa misingi ya dini, jinsia, kabila au rangi. Wakristo na waislamu walisimama bega kwa bega kumfurusha Hosni Mubarak na waramba viatu wake.

Ajabu hawa ndiyo wenye kujua chanzo na mzizi wa dini iwe ukiristo au uislamu.
Ukiangalia watanzania wanavyogawanywa kwa misingi ya dini kiasi cha baadhi yao kuwa maajenti wa ufisadi, unashangaa.

Tatizo ni kupokea au kutojua? Maisha mabovu yatokanayo na ufisadi na utawala wa kijambazi hayajui dini ya mtu.

Ukitaka kujua nimaanishacho, jiulize: kwa sasa mgao wa umeme unawaumiza nani zaidi kati ya waislamu na wakristo kama si watanzania wote? Jiulize zaidi. Kupanda kwa mahitaji na gharama za maisha kunawaumiza nani kama si watanzania bila kujali dini zao? Jiulize tena. Wanaohangaishwa na mikopo ya elimu ya juu au kukamatwa wakiandamana hata kuuawa si watanzania wote?

Uzoefu unaonyesha kuwa waathirika wakubwa wa majanga ya kuletewa na watawala mafisadi ni vijana kuliko kundi lolote.

Wakati wenzetu wakijikomboa sisi tunajikomba na kujichelewesha kwa kujifungia kwenye udini na upuuzi mwingine. Ufisadi hauna dini. Rais akiwa fisadi hata awe wa dini yako hakusaidii zaidi ya kukuumiza. Huyu kimsingi dini yake ni ufisadi na tamaa si uislam wala ukristo. Mshenzi ni mshenzi na fisadi ni fisadi hana dini. Tutatafakari.

No comments: