The Chant of Savant

Wednesday 23 February 2011

Nilivyonusurika kulipukiwa na mibomu

MWENZENU nina bahati ya mtende. Nani alijua kuwa ndiyo nilikuwa nimehamia kwenye banda langu litokanalo na pesa niliyokwapua kwenye kijiwe?

Nani angejua kuwa nilikuwa na home pale Gongo la Mboto? Siri imefichuka. Kweli mficha maradhi kilio humfichua.

Msilaumu kwanini nilificha home kwangu. Unajua kupayuka ni kazi ya hatari sana. Unakuwa na maadui kila kona kama noti mpya zilizomwagwa na waliozitengeneza ili kuziba pengo la matumizi yao ya uchakachuaji.

Hivi kuwakalia kooni kina Njaa Kaya na mafisi wenzake unadhani mchezo?

Thubutu kama hujageuzwa past tense baada ya siku moja. Kama si kuwa janja la wanjanja, hawa mijitu wangekuwa wameishaninyotoa roho. Siri ya kwanza ni kutojua niishipo. Pili ni kutokujua sura yangu wala nichimbukacho.

Lo! Unajua ukiwa na gonjwa la kupayauka, utapayuka hata pasipohitajika kufanya hivyo kama Jamaa alivyoigiza kupayuka kwenye majonzi akaishia kuwa stori na makala ya Mpayukaji mwenyewe orijinale. Kama unadhani nchezo kamuulize mgosi Yusufu Makambale ambaye anaogopewa kwa kupayuka utadhani ushuzi!

Okey poa. Tuachane na wapayukaji uchwara waliolewa midaraka kutokana na kuweka rumenya na mafisi ahadi.

Nikiwa ndiyo nimeanza maisha mapya ya kutanua na kuitwa baba hausi au mwenye nyumba kama waswahili wa bongolalaland wapendavyo kuitwa hata kama hausi yenyewe ni ubavu wa dogi, si mibomu ikalipuka.

Kama siyo kuchelewa Kimanzichana kuuchapa ulabu na kula ndung’u na washikaji, sasa hivi mafisadi wangekuwa wanachekelea kuwa kiboko yao nimerejesha namba.

Najua akina, Ewassa, Rostitamu, shankupe la Kinsomile na gendaeka wengine wangeangusha bonge la party. Nawataarifuni kuwa wasifanye kosa mzee bado nipo nadunda baada ya kushuhudia kutimuliwa kwa mwenzao Hosni Mubarak.

Milipuko ya mibomu imenichanganya. Kwanza maelezo yanayotolewa hayakuniingia akilini. Yangeingiaje akilini wakati machozi ya majonzi ya Mbagala yalikuwa bado hayajakauka?

Baada ya kusikia milipuko na kushuhudia wapendwa majirani zangu wakiwa past tense nilikumbuka kisa cha majeshi ya Masri. Nilitamani tubinafsishe majesi yetu na kuwekeza yale ya Masri.

Wakati majesi ya Masri yanalinda uhuru na ukombozi wa kaya yao, yetu yananyotoa roho halafu yanakuja na lugha za kipuuzi!

Kabla ya kuendelea, nachukua fursa hii kuwafahamisha kuwa rafiki yangu mkubwa, Msomi Mkatatamaa, amepata msiba mkubwa. Kwani katika wale thelathini sijui mia tatu waliokufa na kujeruhiwa mmojawapo alikuwa shangazi yake.

Mie namshukuru Mungu kuwa siku ya tukio mama Kapayukaji alikuwa ngomani na Kapayukaji ndiyo alikuwa amekwenda wilayani kwetu kujiunga na shule ya kata ambazo tunapenda kuziita shule za kukata tamaa au shule za ukata wa kiakili.

Hivyo, unaweza kuona nilivyo na bahati ya mtende. Kutokana na siba hili kubwa, niliitisha kikao cha ghafla cha kijiwe kulaani uzembe huu.

Tulielekeza laana zetu kwa mkuu ambaye anaendesha kaya kihuni. Pili laana zetu zilielekezwa kwa waziri wa magesi, Hossen Muinyi na waziri wa mipango miji ambaye jina lake limenitoka.

Pia laana zetu zilielekezwa kwa wafanyakazi wa halmashauri ya wilaya ya Meteke ambao watatumia madai yetu kupachika nyumba hewa za kulipwa fidia kama walivyofanya hivi karibuni kwenye upanuzi wa uwanja wa njiwa.

Baada ya kumaliza kuomba dua, tulitoa azimio kuwa kaya yetu ibadilishwe jina toka Bongolalaland kwenda Milipuko. Maana kila siku lazima ilipuke mibomu. Kama siyo ya machozi ya kuwatwanga wanafunzi wa vyuo vikuu basi italipuka ile ya AR. Kama siyo hii basi italipuka mibomu ya kashfa kama hii ya Dowanis. Hapa hujaongea bomu la nyuklia liitwalo mgawo wa umeme. Bado hujazungumzia bomu la uhaba wa maji, ajira, maisha bora, usalama, heshima na thamani ya maisha.

Katika mibomu yote hii waathirika ni walevi na si wengine.

Kiasi fulani walevi wameanza kuota sugu ya kulipukiwa mibomu. Laiti wangekuwa wamasri mbona wangewatimua nyani kwenye shamba la bibi!

Turejee kwenye mibomu. Baada ya kushuhudia maangamizi ya Gongo la Mboto tungojee ya Kigamboni, Lugalo, Kunduchi na kwingineko ambako mibomu inatunzwa kwenye maeneo ya walevi.

Kweli walevi ni walevi. Hivi kama si ulevi unaofanana na utaahira, uliona wapi silaha zikitunzwa kwenye maeneo ya civilian?

Hapa tunaongelea milipuko. Bado ile mibomu iliyobaki bila kulipuka haijaanza kufanya vitu vyake kama tulivyoona kule Mbagala.

Bado watoto wetu hawajaiokota au kuikanyaga wakicheza chandimu na mipira yao ya kichovu.

Ingawa roho bado inauma, hakuna kitu kinaendelea kuniumiza roho nusura kujinyotoa kama maneno mbofu ya mkuu aliyekaririwa akiombolezea vifaa na si wapendwa wetu.

Sitaki nimkariri nisije nikajinyotoa roho au nikaanza kusaka mibomu ambayo haikulipuka nikamualkaida mtu mie nikaitwa gaidi bure.

Hivi gaidi ni nani zaidi ya genge linaloua watu wasio na hatia iwe ni kwa nia au uzembe? Hivi kuna ugaidi zaidi ya kunyotoa roho za watu tena wasio na hatia? Mie kusema ukweli matukio ya juzi nayaona kama September Eleven ya hapa kayani.

Hivi kama si ulevi, ugaidi na utaahira ni busara gani kwenda kwenye matanga ya watu wasio na hatia hata kama ni walevi kuanza kulilia sare na mibomu ilhali watu wamepoteza watafuta unga wao? Kuna siku nitawaleta jamaa zangu wa Masri tufanye kweli hebu nyie ngojeni na kuendelea na ukondoo na ulevi wenu.

Puuuuuu! Ngoja nitimke maana naona mibomu ishaanza. Lo! Kumbe pancha ya kweche la Gongo la Mboto Mwenge!
Chanzo: Tanzania Daima Februari 23, 2011.

No comments: