Tuesday, 8 February 2011

Kwanini JK hataki kujifunza kutoka kwa Mkapa?


KABLA ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa kuachia ngazi, hakuna aliyejua siri zake kuhusiana na kujitwalia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira. Hata kama alikuwepo, aliogopa kupatilizwa. Hakuna aliyejua kuwa mgodi wenye thamani ya sh 4,000,000,000 ungeuzwa kwa bei mchekea ya sh milioni 70. Pia, kabla ya Mkapa kuachia urais, hakuna aliyekuwa na ubavu wa kusema ukweli kuwa alijitwalia Kiwira yeye, marafiki zake, watoto wake na hadi wakwe zake.

Vyombo vya habari vilipojaribu kumkosoa tu kwa ujumla,baadhi ya wakubwa wake walitangazwa kutokuwa raia wa Tanzania huku wakiulizwa walipopata mtaji wa kuvianzisha bila kuwa fisadi.

Hakuna ubishi, licha ya kuyatumia vibaya madaraka, Mkapa alijua jinsi ya kuyamilki akifanya alivyotaka kama mfalme. Ilifikia mahali Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake wakaanza kumuabudia bila kujua.

Walianza kuandaa maandamano ya kumpongeza kwa kila alilofanya au kusema hata kama ilikuwa ni wajibu wake au lenye walakini. Gonjwa hili limeendelea hadi kwenye utawala wa sasa ambapo rais Jakaya Kikwete anaabudiwa. Sijui kama yeye anajua hili. Ila kimsingi, kuanzia Mkapa hadi Kikwete hawakuabudiwa kwa sababu walipaswa au walikuwa miungu zaidi ya wahusika kuwatumia kupata kula yao.

Anayebishia hili arejee tukio la kutia aibu na simanzi lililofanywa na wanaojiita wazee wa Dar es salaam kuitisha mkutano kulaani madai ya katiba mpya wasijue watawageukwa waaibike kiasi cha kuonekana ‘mtu mzima hovyo’. Maskini eti walimpongeza rais kwa kukubali kuandikwa katiba mpya utadhani kufanya hivyo ni hisani na si haki ya Watanzania!

Je, wazee wa namna hii hata wasiotaka kufikiri na badala yake wakajirahisi kutumiwa na wababaishaji, wezi na mafisadi wanaweza kuheshimika katika jamii? Je, hawa wana Mungu kweli zaidi ya njaa zao?

Turejee kwenye mada ya leo. Kwanini Kikwete ni mgumu wa kujifunza na hataki kujifunza kwa Mkapa? Leo watanzania wana uchu wa kujua nani mmilki wa Dowans ingawa anajulikana kuwa ni mshirika mkuu wa Kikwete. Wanataka kumjua Kagoda ambaye ni yule yule. Je huyu yuko pekee?

Ukiangalia Daniel Yona alivyokuwa na Mkapa huwezi kuhoji Rostam ni nani na Kikwete ni nani katika hili. Nani amesahau tambo zake kuwa mwenye ubavu aende mahakamani? Ziliishia wapi kama siyo kutokea mbele ya mahakama akiwa amelowa kama jogoo aliyenyeshewa mvua? Hata jogoo ana nafuu maana anaponyeshewa huwa hainamishi kichwa kwa aibu na butwaa kama ilivyotokea kwa mlevi huyu wa madaraka.

Nani aliamini mtu mbishi na mjivuni kama Mkapa kukaa kimya huku akitegemea ulinzi wa aliyewahi kuwa mtumishi wake yaani Kikwete?

Leo tunaongelea ya Mkapa. Kesho tutasimulia ya Kikwete baada ya madaraka kumponyoka. Na hakika haya ni majaliwa ya kila mtu. Muhimu si kulewa na kupuuzia bali kujifunza. Asiyejifunza huzidiwa hata na hayawani ambao yajapo majira ya baridi huandaa makazi yao.

Nani alijiona na kujigamba kama Saddam Hussein au Mobutu Seseseko? Wako wapi zaidi ya kufa vifo vya aibu. Je, yote haya si madarasa tosha kwa wenye akili?

Mkapa alishutumiwa kwa kuendekeza ziara za ughaibuni na kulifilisi taifa. Ajabu Kikwete anafanya yale yale tena akizidisha hadi kufikia kubembezwa kama kichanga alipokuwa Jamaica akitoa mapendekezo ya ajabu kuhusiana na mambo ambayo si muhimu.

Mkapa alisifika kwa kuendeshwa. Alifikia kuamuru polisi wawapige wafanyakazi wa TANESCO pale walipokataa menejimenti ya ulaji iliyokuwa ikipigiwa debe na shemeji zake.

Alisifika kwa kunyamazia biashara ya NGO ya mkewe. Ajabu ya maajabu Kikwete amerudia kosa lile lile hadi kwenda mbele na kuwafanya wanafamilia wake wabia katika serikali yake.

Mkapa alisifika kwa matumizi mabaya ingawa kwa kiasi fulani alifanikiwa kuficha hili kwa kubana mzunguko wa pesa. Kikwete amekwenda mbele hatua mia.

Hasikii wala haambiwi. Amepanua baraza la mawaziri na kuongeza wilaya na mikoa bila kujua athari zake. Mkapa aliongeza mkoa mmoja. Kikwete ameongeza mitatu.

Mkapa aliwakumbatia akina Suleish Vithlani na Jeetu Patel ambao Kikwete amewarithi akiwapa hata nafasi ya kuingiza Ikulu magari yao ya fahari kuonyesha walivyo nazo. Hata hivyo nafasi ya kufanya dili kali na kubwa hawana tena. Kama Mkapa angekuwa madarakani bado, Rostam angejulikana wapi wakati hakuwa karibu naye?

Kikwete amemkumbatia Rostam Aziz kiasi cha kuwa hata tayari kuhatarisha madaraka yake. Laiti angejifunza kwa yaliyotokea hivi karibuni kule Tunisia, huenda angenusurika aibu hii ya uzeeni na kwenye ustaafu.

Siku zote la kufa halisikii dawa. Leo Kikwete ana chiriku wa uharibifu kama vile Yusuf Makamba na Salva Rweyemamu wakimburudisha kwa pambio za sifa kwa kila afanyalo liwe halali au haramu, bora au dhaifu.

Ila anasahau kitu kimoja. Ulaji ukimponyoka ni wale wale watakaokuwa wa kwanza kumuumbua. Wasipomuumbua wataendelea kumshika mateka ili wasitoboe siri zake. Je ni kwanini Kikwete hataki kujifunza kutoka kwa Mkapa?
Chanzo: Tanzania Daima Feb. 9, 2011.

No comments: