Sunday, 20 February 2011

Je huu ni mwanzo wa mwisho wa Gadaffi?

Dikteta wa Libya Muamar Gadaffi amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40. Anaingia kwenye vitabu vya historia kuwa mtawala katili aliyeweza kung'ang'ania madaraka kwa muda mrefu.

Sasa mambo yamebadilika. Baada ya walibya kushuhudia madikteta na wezi wakitimuliwa katika nchi jirani za Misri na Tunisia, wameamua kuamka na kumkabili imla wao.

Taarifa zisizothibitishwa zinasema kuwa waadamanaji wameishauteka mji wa pili kwa ukubwa wa Benghazi. Al-Jazeera iliripoti kuwa vifaru vinne vimeishatwaliwa toka jeshi la Gadaffi huku makao makuu ya polisi mjini Benghazi yakiwa yanawaka moto.

Waandamanaji wameapa kutorudi nyuma pamoja na wenzao zaidi ya 200 kuuawa huku wengine wapatao 1,000 kujeruhiwa.

Habari njema ni kwamba mjini Benghazi jeshi limeamua kuwaunga mkono waandamanaji kama ilivyofanyika huko Misri. Tuzidi kuwaombea wenzetu wakati tukitafakari mustakabali wetu kutokana na kuwa katika hali mbaya kuliko wenzetu wa Maghreb.

Macho na masikio yetu yako Libya. Je mwanzo wa mwisho wa utawala zandiki wa Gadaffi ndiyo umeanza?

No comments: