Sunday, 13 February 2011

Lowassa na machozi ya mamba na yaliyojiri MisriWengi wameshangaa ushupavu na mapendo ya ghafla ya Edward Lowassa waziri mkuu aliyefukuzwa kutokana na ufisadi wa Richmond.

Lowassa amewaacha wengi hoi kujitokeza mbele ya runinga kuwapongeza wamisri huku akiwaonya watawala wasiosoma alama za nyakati! Ama kweli nyani haoni nonihino lake! Ni Lowassa huyu huyu tunayemjua au mwingine? Je ndiyo huku kuanza kujisafisha ili kugombea urais 2015? Nisaidieni jamani.

Kumbuka Richmond hii ya Lowassa ndiyo ilizaa Dowans inayolisumbua taifa linaloendelea kuteketea kwa kiza na wizi wa mabilioni ya kulipa Dowans.
Wapo waliojitokeza kumtetea, kumpongeza hata kuanza kumsafisha Lowassa. Amewafurahisha wanaompigia debe kwa kukemea kilichotokea Misri ambapo rais aliyetimuliwa Hosn Mubarak anasemekana kuwa na ukwasi wa takriban Dola za Kimarekani 40 hadi 70,000,000,000.

Hili "limemkera" sana Lowassa ambaye, kwa bahati mbaya naye anatuhumiwa kujirundikia utajiri utokanao na kuuibia umma ule ule anaodai kuutetea!
Rejea madongo ya kujilimbikizia utajiri aliyorushiwa na marehemu baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere na asijibu. Rejea kuchunguzwa kwa mwanae nchini Uingereza anakodaiwa kuingiza mabilioni yasiyo na maelezo. Rejea kuhusishwa kwake moja kwa moja na Richmond hadi kutimka bila kutoa maelezo.

Lowassa anasema asichotenda na kutenda asichosema ili kumhadaa nani? Kama ni ushauri wa bure ampe swahiba yake Jakaya Kikwete na si kutafuta umaarufu wa reja reja akidhani watanzania hawajui yake.

Je Lowassa anataka kumhadaa nani ahadaike na kumwamini? Yaliyotekea Misri yako mlangoni Tanzania ambako hali ni mbaya zaidi ya Misri. Wizi unaotendeka Tanzania ni mkubwa kuliko wa Misri. Linganisha maisha ya wamisri na watanzania utajua ninachomaanisha.

Kama Lowassa anamaanisha anachosema na kusema anachomaanisha, arejeshe pesa yetu kwanza na kuomba msamaha kwa kutuingiza kwenye kiza mbali na kutuibia mabilioni nyuma ya Dowans.

Lowassa anawapongeza wamisri kwa lipi iwapo wamewatimua akina Lowassa wao?

No comments: