Tuesday, 8 February 2011

Wamisri si kama Wabongolala

NILIKUWA Cairo kwa wiki nzima kushuhudia dikteta mwingine anavyotimuliwa ingawa amevuta muda. Nilikuwa mgeni wa mkuu wa majeshi ya Masri, Lieutenant General Sammy Haafis Anaan, ambaye amezuia majeshi kuwashambulia waandamanaji kwa sababu madai yao ni ya haki.

Huyu gwiji ametoa mfano mpya kwa wanajeshi wengine wanaojiita wa wananchi wakati ukweli ni wa watawala wala watu.

Amewaumbua wengi. Naona lile limenuna kwenye migwanda yake. Hata unune huu ndiyo ukweli ambao sina pa kuuficha bali kuutapika mbichi kama ulivyo.

Mwenzenu ni msomi na mzalendo asiyetishwa na fedha chafu za wakubwa mafisadi. Huyu jamaa ni shujaa wa kweli. Amekataa kuwekwa mfukoni na wapuuzi wachache wasio na udhu wala akili ya kutawala bali kula bila hata kunawa.

Mungu amjalie. Kila siku namuombea gwiji huyu mwana mwema wa nchi yake. Natamani angekuwa mkuu wa ndata za Bongolalaland.

Pia nilikutana na msemaji wa jeshi la Misri, Ishmaail Etmaan, baada ya kusalimiana na waandamanaji kwenye viwanja vya Tahrir mjini Cairo ambavyo vimebatizwa jina la viwanja vya ukombozi (Liberation Square, kwa umombo).

Makazi yangu yalikuwa kwenye mitaa ya Aghouza kwa wale waliowahi kuishi au kutembelea Cairo.

Sikukaa Cairo tu. Nilikwenda kule Alexandria na kukaa siku mbili ili kukusanya story. Nako mambo hayakuwa mambo. Vijana, wazee, kina mama hata watoto walijitoa kimasomaso na kumzomea dikteta wao kiasi cha kuichapa viatu picha yake.

Katika mila za Kiarabu hasa Masri, kusigina au kupiga kiatu kitu ni dharau inayomtosha mtu kujinyotoa roho. Kwa vile watu wala watu hawana chembe ya aibu kama jamaa zangu wa Dowanis na Richmonduli, Kibaraaka hakujinyotoa roho.

Nilipita maeneo ya Kafr-El-Meselha, Monufia ambako ni nyumbani kwake Kibaraaka. Nako mambo hayakuwa mambo. Jamaa kakataliwa hadi kwao!

Kutoka pale nilipiga safari hadi Sham el Sheikh. Huku mambo yalikuwa poa. Maana walalanjaa wa kawaida hawajui kuwa kumbe kuna pepo nchini mwao. Huku ni kufuru tupu. Kuingia mjini lazima upigwe sachi kwa sana ili usiingize mabomu.

Kutoka pale nilipiga guu hadi Luxor. Nako kulikuwa kumelala kutokana na kuwa kivutio cha utalii. Nilichogundua Luxor na Sham el Sheikh ni kwamba watalii ni kama ndege. Kilipoanza kimbembe walijitimkia wakielekea airpoti ambako mataifa yao yalikwishatuma madege kuja kuwaondoa Masri.

Hili liliniletea sononeko. Maana kaya yangu ya Bongolalaland pamoja na kuwa na taarifa na habari kuwa mimi nilikuwa kwenye machafuko, haikujihangaisha kutuma hata salamu achia mbali ndege! Hili limenifundisha jambo moja. Hatuna kaya bali kusanyiko la mabalaa.

Nilejee kwenye niliyoona kwenye sakata la Masri. Niligundua kitu kimoja. Ndata ni ndata na wana roho mbaya. Baada ya kutembeza kipigo wasifanikiwe wakaambulia kuuawa baadhi yao walikitoa. Walipokuja wajeshi wakawatia kila aibu ndata kutokana na kutumia akili badala ya makalio kufikiri.

Hili ndilo jeshi la wananchi na siyo mashimboshimbo yanayotisha wananchi kwa sababu ya kulewa makombo ya ufisadi na upuuzi.

Ndata hao ndiyo usiseme. Walitimuliwa walipoua watu wakimpigania bwana wao.

Turejee kwenye kiini cha machafuko. Kwanza, ni ufisi na ufisadi, kujuana na kulindana.

Pili, ubabaishaji, usanii, ujambazi wa mchana na upuuzi mwingine.

Ukilinganisha makosa ya Kibaraak na madhambi ya hawa nyang’au wetu, Kibaraak ni cha mtoto. Alijitahidi kuijenga Masri sana. Kosa lake ni kukalia ulaji hadi akachusha na kuchosha. Vinginevyo jamaa si mbaya kama hawa nyani niwaonao wakila kila kitu kuanzia matunda hadi wadudu.

Nchi ile inavutia kutokana na walivyoipanga na kuijenga. Kila eneo lina maji na umeme. Ukitaka kiwanja hakuna kulanguana wala kuuziana maeneo ya wazi. Na miundombinu yote kuanzia maji, simu na umeme iko tele. Hakuna mgawo wala ulanguzi wa umeme. Maisha ya Wamasri yana nafuu sana ukilinganisha na Wabongolala.

Naamini kipute cha Masri kingetokea Bongolalaland hawa wahuni wetu wangekata umeme ili kuvuruga maandamano ya umma.

Kilichowasukuma wamasri kuandamana ni ile hali ya kuwa wakweli kwa nafsi zao na wengine. Bei za mkate, kwa mfano, zilipanda. Hili liliongeza mafuta kwenye moto. Wamasri si kama wabongolala. Ukipandisha bei ya vitu hata kwa senti moja wanaingia mitaani.

Maana hawana ule unafiki wa kusema bei ikipanda wataliibia taifa. Kila mtu anajitahidi kuwa mzalendo na uwajibikaji na maadili vinaenziwa. Siyo kama huku vinadharauliwa na wizi na ufisadi kuhalalishwa.

Kupayuka kwangu kulitaka kunitokea puani nilipokwenda kwenye chuo cha Assiut. Si nilijitia kujua nikawahoji wanafunzi kwanini hawavuti subira kutokana na kaya yao kuwa na ahueni ikilinganishwa na kaya zetu. Mmoja wao alinijibu tena kwa kuniita jina baya, ibn Muthnaak yaani mwanaharamu. Alinipa laivu kuwa anajua kuwa kwetu ni maiti wezi wasiojitambua. Nilishangaa alivyoweza kutengeneza jina hili, yaani maiti wezi.

Nilijifanya sikumuelewa ili kuficha hasira zangu japo roho ilikuwa ikinituguna na kunitukuta kwa hasira. Nilichopashwa ni ukweli unaouma hata kama unakera. Ni ukweli mtupu tu maiti wezi.

Tusingekuwa maiti na wezi wezi wasingetuchezea shere kila uchao nasi tukabaki kulalama bila kuchukua hatua mujarabu.

Hebu angalia kina Dowans binti Richmond wa Kagoda wanavyotuchezea akili. Rostitamu mara aseme siwajui Richmond wala Dowanis.

Mara nina Attorney Powers naweza kuandika kulipa kufuta cheki na upuuzi mwingine. Je kuna ushahidi zaidi ya huu kuwa Dowanis ni Rostitamu akimwakilisha Njaa Kaya na Ewassa? Tusingekuwa maiti na wezi si tungekuwa tumeishaingia mitaani kulianzisha na kufungua Liberation Square yetu?

Kama si sisi kuwa maiti wezi ni kitu gani kinatuzuia zaidi ya sura mbili zetu? We need to break this psychological vicious circle engulfing us. Sorry. Nikipandisha Mwenembago huongea kimombo. Nisameheni kwa kuchanganya lugha ila naamini nimeeleweka. Kwa wale ambao kimombo hakipandi, sorry sana. Kuna haja ya kwenda English School ingawa nazo ni mabomu. Hayo tuyaache. Tutafakari na kuanza kudhamiria kukata mikatale.

Naona simu yangu inaita. Kumbe ni Baraka Obama kanipigia kuomba ushauri juu ya kumaliza tatizo la Masri!

Poa. Nitamwambia akitoe hata wale wa kusini mwake. Msalimie Michelle na watoto.

Chanzo: Tanzania Daima Feb. 9, 2011.

No comments: