Wednesday, 16 February 2011

Mkuu wa kijiwe alipoikana Dowans mara tatu

HIVI karibuni nilicheka hadi mshirika wangu wa bedroom akadhani nimepata kichaa cha ufisadi. Alidhani nimechanganyikiwa hadi kugeuza kituko na kichekesho kama wale wanaodanganya mchana kutwa kuwa ni wasafi wakati ni wachafu kuliko hata chawa.

Nilicheka sana baada ya kumuona Mkuu kupitia runinga yangu ya Hi Def bomba kali, akiwadanganya wabongolalalanders kuwa haijui Dowanis wakati yawezekana ndiye mshitiri na mnufaika wake.

Nilicheka kwa hasira kiasi cha kuanza kuweweseka kutokana kupandisha mwenembago kiasi cha kutaka kwenda kuwanasa vibao walevi, kumbaffu zao.

Kitu kilichonikera ni kusema, “siijui” Dowanis. Hata hivyo, hajajinasua, na hatajinasua kwenye mtego huu uliogeuka msalaba kwake.

Alisema haijui Dowanis. Ukweli ni kwamba anaijua nayo inamjua saana tu. Kama angekuwa haijui angesema sijawahi kuijua Dowanis. Hata hivyo ungekuwa upuuzi kusema haijui Dowanis wakati li-sirikali lake ndiyo liliingia mkataba wa ujambazi na Dowanis.

Sasa tumsaidie. Kama haijui Dowanis ingawa anaijua tu, aende kwa shoga yake Rostitamu mwenye funguo na mikoba yote ya jinai hii. This goon has all damn power of attorney. Naongea kimombo mjue mie ni msomi tena wa sheria.

Wenzangu huniita our learned brother hata kama wengi wao wanakula rushwa kiasi cha kutoa elimu ya jinsi ya kuingia mikataba mibovu na kupata mipesa mingi baadaye kama yule Maregereresi wa Kagodoka. Mie nilikataa upuuzi huu nikaamua kufanya kazi ya upayukaji badala ya kutetea mibaka.

Narejea maelekezo ya Mkuu wetu kijiweni, kuijua Dowanis kwa kusisitiza aende kwa Rostitamu. Kumbuka. Hawa ni marafiki wa kufa na kuzikana. Hamuoni alivyogoma kumshughulikia ukiachia mbali juhudi zake za nyuma ya pazia kutaka walipwe haraka?

Hili halina ubishi. Dowanis imekuwa lisirikali ndani ya lisirikali. Kwanini tusiwafanyie kama Tunisia jamani?

Kimsingi, kisanii, alichosema ni “Siijui, I mean, naijua Dowanis nami ni sehemu ya jinai hii.” Period. Ni tusi la nguoni kwa walevi wote wa Bongolalaland. Ni ubakaji wa haki.

Kama haijui na hataki kuonana na Rostitamu ammegee kila kitu basi angemuuliza Nshomile Silvia Rweyependekeza ambaye aliwahi kufanya kazi ya kuisafisha Richmonduli, mama mzazi wa Dowanis mke wa Kagodoka.

Kama Nshomile amekosa kumbukumbu angemuuliza Eddie O’ Shea aliyetaka kuizima Richmonduli bila mafanikio. Kama basi wote hawa hawapatikani angemuuliza Ewassa aliyesuka mipango yote.

Ikizidi ikipungua angemuuliza Mwana wa Idd Majaala ambaye na wanasheria wengine mbwa mwitu walitoa ushauri wa janga hili la kaya.

Mkuu hata akane vipi tunajua, tunaelewa, tunafahamu na kuamini yeye anaijua na hata kiboko yake Dk. Sihala alisema yeye ndiye Dowanis,
Au tuseme kama haijui Dowanis, basi Dowanis inamjua na kumhusu hadi siku kiama maana hata walevi wanajua hakuna Dowanis nyingine isipokuwa mkuu na wenzake.

Kwa tunaomjua hatukushangaa wala hatutajisumbua na kushangaa. Kama aliweza kukwepa HEPA iliyomwingiza kwenye ulaji, atashindwa Dowanis?

Huyu jamaa si mjinga kama wengi wanaovyomchukulia. Kicheko chake kimeficha mengi.

Anajua udhaifu wa walevi wa Bongolalaland. Anajua walivyo woga na wanafiki kwa nafsi zao. Ukipandisha bei ya mkate badala ya kuingia tahrir square kuandamana wanapanga jinsi ya kudokoa kwenye ofisi za umma.

Wapo wanaojiingiza hata kwenye rushwa na hongo za ngono kwa akina mama na dada hata usenge kwa kina baba. Huu ndiyo huwa naita ukeketwaji kiakili ambao ni mbaya kuliko wa kimwili. Inaudhi najua. Lakini nitumie lugha gani mtume Mpayukaji mie nieleweke? Niwakere vipi ili mchukie na kuchukua hatua?

Najua wapumbavu wananichukia mimi badala ya kuchukua almasi ya kiakili niwapayo.

Mie sipayuki kipumbavu kama kina mgosi Makambale na Nshomile. Natema busara tena kwa lugha na ujasiri vilivyowashinda wengi.

Mafisadi wanaweza kujiridhisha kuwa yao hayajulikani, yatajulikana siku wakitoka walipo.

Narejea tena, kama huijui mbona umeshindwa kuwafungulia mashtaka kina Kagodoka, na wengine wanaojulikana wazi? Ukiwashitaki watakuumbua. Hii ndiyo siri ya Kagodoka na Dowanis kupeta ukiachia mbali maslahi yako.

Ni kituko cha mwaka eti mkuu wa kaya hajui Dowanis! Kwanini asiseme kuwa anaijua jinsi ilivyochangia kuinua mtaji wa kuula? Ningekuwa mimi, ningewambia walevi kuwa tusameheane kwa vile nao walipata mgawo wao waliokuwa wakiufakamia wakati wa kampeni ya uchafuzi ulioishia kwa uchakachuaji.

Mlichakachua benki kwa Ma-EPA na mahepe. Hamkutosheka. Achovyaye kwenye buyu la asali hachovyi mara moja.

Mmechakachua kula. Sasa mnataka mchakachue hata akili zetu yarabi? Mbona hata mijusi wanajua kuwa Dowanis ni ya nanihino? Mbona hata kunguru wanajua kuwa huu ni uhuni na wizi wa mchana unaofanywa na wale wanaoitwa waheshimiwa wakati matendo yao yanawaonyesha wa hovyo kama chawa!

Nimalizie kwa kuwaibia siri. Jamaa aliwaona nyinyi makenge kusema haijui Dowanis wakati yeye ndiye…, malizieni. Siri ni kwamba mkiamua kuingia mitaani kwa amani, kinaweza kueleweka.

Msiogope mibunduki ya majambazi yenye sare maana Mureno Okampo yuko pale kwenye nchi ya nyao. Msidhani yale ya AR yanaweza kurudiwa na Okampo akachekelea. Kazi kwenu siri zote mmepewa mkiendelea kuzubaa mtaliwa mpaka mkome.

Haloo, haloo. Huyu naona anabeep. Wabongolalalander kwa kubeep! Ngoja nifiche kibroadband changu vibaka wasije kukinyofoa kama Rostatimu anavyotaka kunyofoa njuluku za walevi. Kwaheri.

Chanzo: Tanzania Daima Februari 16, 2011.

No comments: