How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 30 August 2012

Tulikataa futari na mashindano uchwara


“Hili kampuni la simu lenye kila dhambi ya ufisadi eti lilitaka kutufuturisha. Kwanini msitupe huduma bora badala ya kutuhonga vipilau na upuuzi wenu? Ukipiga simu unaambiwa ongeza salio halafu wanakata pesa yako hata kabla hujaongea,” alianza kulalamika Dk. Mzee Maneno.
Dk. Mchunguliaji: “Wakati juzi namdeep shemeji yenu si walinikata shilingi 1,000!”
Dk. Machungi: “Mgosi siyo kudeep bai kupeep.”
Mchunguliaji: “Nilisema hivyo makusudi kuona kama mnajua kimombo. Hata wewe mgosi wapitia Mombo ukienda Lushoto, lazima ujue kimombo.”
Machungi anazidi kuongeza uhondo: “Hujui kuwa kishambaa na kingeeza ni lugha moja?”
Mbwa Mwitu hakubali: “Mgosi sasa huo uongo wa mchana. Unakuwa muongo kama wanasiasa!”
Machungi anakula mic tena: “Mgosi si uongo. Hujawahi kusikia wazungu wanasema why? Wasambaa tunasema kwai.”
Kijiwe hakina mbavu kwa jinsi magwiji hawa wa vituko wanavyopeana mistari.
“Jamani mie naona tungejadili hili la mikampuni mijizi inayotoa huduma chafu na kuwaibia watu kila siku huku serikali ikiinyamazia,” alipendekeza Dk. Profesa Msomi Mkatatamaa.
“Kweli msomi umelonga. Maana walevi wamekuwa kama mataahira. Ajabu makampuni haya ya kitapeli eti nayo yanafuturisha watu! Futari au hongo tena ya pesa chafu ambazo kuzila ni ukafiri tosha.” alirai Dk. Mipawa.
Profesa Msomi anaongezea msumari kwenye madai yake: “Mimi naona kama baadhi ya watawala wetu wanafanya biashara na hii mikampuni. Maana badala ya kututumikia sisi wanaitumikia hii mikampuni yao ya wachukuaji wanaowaita wawekezaji. Uwekezaji gani wa kutupa huduma chafu na kuchukua kila kitu?”
Wakati kikao kinaendelea aliingia Dk. Shemihiyo, mdogo wake Dk. Machungi (huyu ni memba mpya aliyetokea Lushoto) akiwa anatabasamu.
Baada ya kutuamkua alitoa dukuduku lake: “Wagosi, nimepewa ujumbe na kampuni ya simu ya kuwataarifu kuwa mnakaribishwa kwenye futari Ijumaa ijayo baada ya swala laswir.”
Dk. Profesa Mkatatamaa anadakia hata kabla Shemihiyo hajamaliza: “Yale yale tuliyokuwa tukiongelea. Yaani mikampuni yenyewe mijizi na haina huruma nasi sasa huu uumini wa kutufuturisha unatoka wapi kama siyo rushwa na kutufanya majuha tena makafiri?”
“Dk. Prof Msomi unashangaa makampuni tapeli na jambazi kufuturisha! Hukusikia wanasiasa wachafu tena mafisadi wanaonuka kwa rushwa na ufisadi nao wakifuturisha na kujipiga vifua kuwa wamefanya jambo la maana wakati ni ukafiri wa kutosha?”
Dk. Mpemba ameguswa pabaya: “Yakhe usemayo nkweli. Siku hizi hata futari na dini havina maana tena wallahi. Kula mwenye fedha anafedhehesha dini kwa fedha zake. Juzi sie ntaani kwetu tulikaribishwa kwenda futuru na rahisi tukasusa isipokuwa waroho wachache.”
Dk. Mbwa Mwitu aliamua kukwanyua mic: “Dk. Mpemba, shehe na ustaadhi kama wewe ungeenda hakika, licha ya kuwa kafiri ungegeuka shehena badala ya shehe.”
“Dk. Mbwa Mwitu wasema kweli wallahi wabillahi. Siku hizi mashehe na wasomi wa dini tu-wachache. Mie nlihifadhi koraani yote na kusoma fikh. Hivo najua dini vilivo. Sikusoma popote eti mtu asokuwa nsilamu kufuturisha. Afuturisha vipi wakati yeye hafungi wala kuishi angalau kwa haki achia mbali kuwa muumin au muuminat?”
“Dk. shehe ustaadhi hafidhi Mpemba umenena. Mimi nilikuwa nashangaa sana kuona watu wasio na dini isipokuwa ufisadi eti nao wakifuturisha. Dini imegeuzwa mchezo wa kamari ambapo kila mwenye nazo hucheza. Huwezi kufuturisha mtu wakati wewe ni mchafu na wengine ni makafiiri mie sina mfano.
“Huwezi kuiba pesa ya umma au ukatajirika kwa mihadarati halafu ukafuturisha. Huu ni ukafiri ingawa mie siyo Mwislamu.”
“Allah Subhana anasema kwenye surat Kaffirun kuwa; ‘hamuabudii ninayemwabudia. Siabudii mnachokiabudia. Mna dini yenu. Nina dini yangu’.” Alikariri aya Dk. Shehe Mpemba na kuwaacha watu vinywa wazi.
Aliendelea: “Wao waabudia pesa na wizi, uchafu, rushwa na dhulma. Kwanini wataka kuwaingiza watu wema kwenye dini yao hii chafu? Ajabu watu nao wajipeleka kama vile hawana macho!”
Dk. Mbwa Mwitu alichomekea: “Kuna fisadi ambaye sitaki kumtaja anayefanya kazi serikalini ambaye anajulikana kwa wizi na uasherati wake. Eti naye alitaka kutufuturisha. Nilimpa pasonali wazi wazi.”
Akiangalia huku na huku na huko aliendelea: “Kama kawaida yangu nilimpa wazi na kumuuliza; nani kawaambia tuna njaa ya futari? Tuna njaa ya maendeleo na kutendewa haki finish.”
Huku kijiwe kikionesha wasiwasi juu ya maneno ya Dk. Mbwa Mwitu ambaye tunamjua, kama jina lake hawezi kukataa kitu na kama ana dini basi dini hiyo ni ulaji, Dk. Machungi alichomekea: “Sisi ni maskini kwei akini si maskini wa mawazo.
“Hatitumii matumbo yetu waa masabui kufikii kama wao. Yaani mmegeuza kaya yetu kuwa kaya ya upuuzi! Hatihitaji hongo bai tinataka haki na huduma safi. Hakuna ukafii kama kufutuu pesa chafu ya wizi na ujambazi.”
Akiwa anaendelea kusema, mara Mzee Maneno alinong’ona: “Huyu mwenzetu naye anataka kutufanya majuha. Pamoja na kuzaliwa na wazazi waswalihina huwa haishi maeneo ya kigogo kukamata kitimoto. Huyu hawezi kukataa futari hata kama ni ile itokanayo na pesa za bangi, miunga, bia, kamari, wizi, rushwa na ufisadi.”
Baada ya kuona mada inaanza kuharibika kutokana na baadhi ya wenzetu kuanza kuwasengenya wenzao, mzee mzima ambaye nilikuwa kimya muda wote niliamua kuokoa jahazi. Nilikohoa kidogo na kubwia kahawa yangu kidogo na kuendelea: “Jamani, naona kama mnaanza kutoka nje ya mada. Sasa nitawarejesha. Yote mliyoongea kuhusiana na dini kugeuzwa nyenzo ya kutolea rushwa ukiachia mbali kudhalilishwa, mie nadhani tutoe azimio.”
Nilikatua kashata na kuendelea: “Kwanza tulaani mchezo huu mchafu wa kugeuza dini kitu cha kuchezea. Pili tulaani uroho na upogo wa watu wetu. Tatu tuhakikishe haya makampuni ya simu yanayotuibia huku yakitupumbaza na bahati nasibu na mashindano uchwara yanafurushwa kayani mwetu. Nne viongozi wote mafisadi wanaoyakingia makampuni haya kifua tuhakikishe wanatimuliwa.
“Tano, tumrejee Mwenyezi Mungu huku tukijitahadhari na uroho, usanii kama wa wale wanaokataa kuhesabiwa utadhani hawatahesabiwa. Nasema mtahesabiwa hata mkiwa maiti. Hata mkihama nchi tutawafuata huko na kuwahesabu. Yule jamaa Mrundi anayegomesha walevi aitwaye Pondwa lazima apondwe na kunyea debe.
“Acha niishie kwenda kumzika rafiki kipenzi chetu ndugu yetu mzee Matonya. Sijui wapenda kuzika nao watakuja au kwa vile huyu alikuwa havai suti kama wao basi hafai.”
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 29, 2012.

2 comments:

Anonymous said...

Nisoma lakini hata sikufika mwisho
naina upuzi tuu bampavvv

Anonymous said...

Anonymous hapo juu umesema ukweli. Huu uandishi hauwezi kueleweka kwa wapumbavu. Hivyo kutoelewa ni ushahidi tosha kuwa wewe ni.. Malizia mwenyewe. Mpayukaji bravo hapa.