The Chant of Savant

Tuesday 6 November 2012

Kikwete pambana na ugaidi badala ya kutoa pole


Hakuna ubishi kuwa vitendo vya kigaidi vinavyoendelea nchini ni matokeo ya ulegelege na uzembe wa serikali. Ingawa rais Jakaya Kikwete amekuwa mwepesi kuwahi kwenye matukio ya waathirika wa vitendo vya kigaidi, hii ni sawa na machozi ya mamba. Je lipi muhimu, kutoa pole au kupambana na vitendo vya kigaidi. Serikali imeonywa mara nyingi kupiga marufuku vikundi vinavyoeneza chuki baina ya watanzania. Imeonywa juu ya mihadhara ya kidini inayoendeshwa na wachumia tumbo wasio na hata elimu ya dini imedharau. Sasa tazama madhara ya ujinga huu ambapo watu wanaanza kuathiriwa kama ilivyotokea kule Zanzibar ambapo katibu wa Mufti wa Zanzibar Fadhil Soraga ( Pichani)amemwagiwa tindikali.
Tunadhani waathirika hawahitaji "machozi na pole" vya rais bali kushughulikia chanzo cha kadhia hii. Ingawa waliofanya kitendo hiki cha kinyama hawajajulikana, kuna haja ya vyombo vya dola kuwasaka na kuujulisha umma ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Hali ikiendelea hivi bila kudhibitiwa, kunaweza kuibuka hatari ya kulipiziana visasi hata kwa watu wasiohusika. Je amani anayoimba Kikwete na wenzake siku zote bado ipo? Tafakarini umma umechoka kutapeliwa kwa usanii wa kisiasa.

No comments: