The Chant of Savant

Tuesday 13 November 2012

Waishiwa tajaneni haraka vinginevyo tutatia guu



BAADA ya msimu wa sanaa na abracadabra kuanza kule Idodomya, juzi tulishuhudia vituko ambapo wahishimiwa waliendelea na mchezo wa kuvuana na kuvalishana nguo.
Kituko cha kwanza ilikuwa ni kufichwa na baadaye kuachiwa ripoti ya uchunguzi dhidi yaaibu za wahishimiwa kudai rushua toka kwa katibu mkuu aitwaye Maaswi.
Kwa vile wahishimiwa walikuwa ndiyo watuhumiwa, wapelelezi na waendesha mashtaka, kila mlevi alijua ambacho kingetokea kama kilivyotokea.
Pamoja na Takokuru kusema jamaa ni wala rushua, kamati yao haikuwakuta wao wakiwa na hatia ya kudai rushua toka kwa bwana Maasi au Maaswi kwa kiarabu.
Kituko kingine au sema scene ni pale Mzito Kabwela alipokuja na hoja ya kutaka walioficha njuluku kule Uswisi washughulikiwe.
Hata kabla ya kutulia si Mzito alibanwa ataje majina akaishia kujikanyaga huku mwenzie Mtundu Lissu akiwataja Endelea Chenga, Grey Mgonjwa na “marehemu” Dadi Balaahili.
Mwenzenu nilingoja kwa makini kusikia majina hasa yale yaliyotajwa kwenye the so-called List of Shame ya Dk. Silaha. Kwanza, tujiulize. Hata hao wezi na majambazi wakubwa walioficha njuluku zetu nje wakitajwa unategemea nani awachukulie hatua wakati wote wameoza? Hivi unategemea kambale amnyoe mwenzie sharubu? Thubutu yako!
Ziko wapi tambo za Takokuru kuwa ingewasiliana na mamlaka za Uswisi? Mgosi Machungi niliyemtuma kufanya upelelezi kwenye ofisi ya Eddie Washea aliripoti kuwa hata barua ya kuonyesha nia ya kudai njuluku zirejeshwe haijaandikwa! Hiyo ndiyo Bongolalaland inayoweza kuliwa na kila jizi jambazi na tapeli.
Hiyo ndiyo Bongolalaland ambayo imegeuka shamba la bibi chizi. Ndiyo hiyo Bongolalaland ambayo mzee Mchonga aliipiga laana baada ya kugundua kuwa patakatifu pa patakatifu paligeuka kuwa pango la wezi mchana kweupe huku walevi makondoo wakichekelea kama si kulalamika lalamika.
Hawa wanaodai watu watajane majina wanaonekana kuwa watu wabaya kuliko hata shetani mwenyewe. Hivi kama watatajana majina ukakuta hata majina ya watakatifu na watoto na wake zao tutafanyaje? Sisi kijiweni tunasema tajeni hata kama kuna jina la Mungu mwenyewe.
Tajaneni tuwaone wajanja vinginevyo tutaendelea kuwaona wanafiki waongo na wababaishaji wa kawaida. Tuchukue fursa hii kumshukuru na kumchakatiza Mzito Kabwela aende hatua nyingine kwa kutaja majina. Maana ashataja majina ya wizara walimotoka walioficha njuluku nje.
Kwa kumbukumbu ni kwamba Mzito alitaja mawaziri wote wakubwa walioshika madaraka kuanzia 2003 hadi 2010. Hii maana yake ni kwamba watajwa hapa ni Freddie Tuwahi Sumae.. we koma! Wengine ni Eddie Ngonyani Lowasir, na mzee Mizengwe iliyoPinda. Kitaalamu huita ushahidi kama huu circumstancial evidence yaani ushahidi uliojikunja kunja kimazingira.
Wengine waliotajwa ni waliowahi kuwa madingi wa shirika la Wese yaani (TIPIDICI). Hapa namkumbuka rafiki yangu Jona Kilaganane nawe msomaji ongezea mwingine ili tuwavue nguo. Wengine waliotajwa ni wale walioshika wadhifa wa waziri wa madini 2003 hadi 2010. Hapa rafiki yangu Niziro Ka-damage, Willy Ngeeja na Dan son of Jonah, hamuwezi kuponyoka. Rejesheni njuluku zetu haraka kabla hatujawapiga na albadiri.
Nasikia pia kuwa Mzito Kabwela alikuwa anataka kuwataja wengine wakubwa zaidi akatishwa na kuibiwa karatasi yake alipokuwa ameorodhesha majina yao. Hata hivyo rafiki yetu Profesa Msomimkatatamaa alifanikiwa kuyanyaka majina ya majizi hawa wazito.
Waliopaswa kutajwa walikuwa ni wote waliowahi kukaa patakatifu pa patakatifu baada ya kuondoka mzee Mchonga bin Musa. Hapa rafiki yangu Alie Hossein…nyi, Bendangerman Mkapu na Njaa Kaya hamuwezi kuchomoka. Najua leo hamuwezi kufanywa lolote. Ila huenda kuna siku ya siku mtajikuta mkinyea debe kule lupango kwa wakati wenu na madhambi yenu.
Kabla ya jamaa kuanza kuwashiana taa za kutaka kutajana, nani angeamini kuwa kaya hii ni ya mibaka ingawa siyo siri? Wahishimiwa wanakamua kwenye ujumbe wa kamati huku mawaziri wakiiba wanapomwagwa wino kwenye mikataba kama alivyofanya Ni Ziro Ka-damage alipokwenda London kusaini mkataba wa Uzwaagi hotelini na akapewa njuluku zake alizokimbizia Uswisi.
Kwa vile sasa habari zinakuja mdomdo, kijiwe kina mpango wa kukaa kama kamati na kutoa shinikizo kwa wahishimiwa kutajana kabla hatujaandamana hadi mjengoni na kuwafanyia kitu mbaya. Leo sitasema ni kitu gani mbaya tutawafanyia. Tutawafanyia kitu mbaya kuliko hata hicho wanachofanyiwa na huyo mama Microphone bint Speaker.
Yeye anawadhalilisha ili kuwaridhisha mabwana waliomsimika hapo halipo. Sisi hatutawadhalilisha. Badala yake tutawaadhibu kama watoto wadogo ili kila mtu hata kunguru wawacheke kila watakapopita. Hivi fikiria tukiingia mjengoni wanakijiwe wote halafu tujinyotoa roho akitakuwa kitu mbaya kwa waishiwa sorry wahishimiwa?
Lakini hatutafanya hivyo kutokana na kuwa hii mijitu haina huruma hata mkijinyonga itaendelea kuiba. Heri kuinyonga yenyewe badala ya sisi. Tunaweza kuingia mjengoni na kukaa kwenye viti vya kabla hawajaingia na wakiingia tunatangaza rasmi kuwa mjengo ni wetu na sio wao.
Tunaiambia dunia kuwa tangu siku hiyo tumeamua kujiwakilisha baada ya kugundua kuwa kumbe wenzetu wanawakilisha matumbo yao na vyama vyao badala ya sisi waliotuingiza mkenge. Unadhani hii ni kitu ya mchezo? Tutakuwa wa kwanza duniani kuwatimua waishiwa kwa kuingia mjengoni na kuchukua nafasi zetu. Maana vile vigoda wanavyokalia ni mali ya majimbo siyo matumbo yao.
Tukishaingia mjengoni tunatangaza kuwa hata mashangingi na mashumbwengu ya waishiwa ni mali yetu. Hivyo, tutawaamuru waondoke pale kwa miguu wakapande dala dala na baadaye treni kuelekea kwao kwa aibu yao. Pia tuwaamrisha warejeshe mshiko wote uliopo hapa kayani na Uswisi haraka sana kabla hatujachukua hatua nyingine kama vile kuwa-Gaddafi kama siyo kuwa-Mubaraka tena haraka.
Utani kando, hivi walevi tukiamua kuvamia ule mjengo na kuchukua nafasi yetu kuna mtu anaweza kutuzuia? Hii meseji ni ya mshirika wa Bedroom. Acha niende tukapange jinsi ya kuitana waheshimiwa baada ya kuwatimua wale wezi wanaoshindwa kutajana. Sisi tutawataja piga ua tukishafika huko.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 13, 2012.

No comments: